Tuesday, April 11, 2017

SHIHATA ASISITIZA WELEDI NA MAADILI KWA WANAHABARI ZANZIBAR

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
KAMATI ya Maendeleo ya Wanawake, Habari na Utalii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar  imevitaka vyombo vya Habari nchini kuendelea kutekeleza majukumu yako kwa kufuata misingi ya weledi, maadili na miiko ya fani hiyo ili viweze kujenga uaminifu wa kudumu kwa jamii.

Wito huo umetolewa wakati  Kamati hiyo ilipotembelea Bahari Fm Radio,  na kukagua shughuli za kiutendaji na uendeshaji ndani ya taasisi hiyo, na kushauri taasisi hiyo kuandika na kutangaza habari za kudumisha Amani na Utulivu wa nchi sambamba na kupinga vitendo vya kuhamasisha vurugu.  

Akizungumza baada ya kutembelea maeneo mbali mbali ya redio hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ali Suleiman Shihata ameupongeza uongozi wa Bahari fm na watendaji wake kutokana na kazi nzuri wanayoifanya ya kuelimisha na kuburudisha umma.

Alisema  chombo hicho kimekuwa ni miongoni mwa taasisi bora za kihabari Visiwani Zanzibar, kutokana na umahili wake wa kuandaa vipindi bora vinavyoendana na wakati wa sasa kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Shihata, alifafanua kuwa maendeleo ya Zanzibar yametokana na mchango mkubwa wa vyombo vya habari, vinavyotoa taarifa sahihi za maendeleo na kuimarisha uchumi wa nchi.

“ Nakupongezeni kwa kazi nzuri mnayoifanya kwa jamii, kwani mmekuwa ni nguzo imara ya kuhubili amani na mshikamano wa nchi huku mkielekeza jamii kupitia vipaza sauti vyenu kukataa kwa vitendo utengano na uchochezi wa vurugu za kuingiza nchi katika migogoro isiyokuwa na maana.”, alieleza Shihata ambaye ni Mwanasiasa Mkongwe visiwani Zanzibar wa tiketi ya CCM.

Pia alitoa wito kwa watendaji wa chombo hicho kutumia vizuri kalamu zao na kufanya kazi za kihabari kwa kuzingatia weledi, maadili, miiko na misingi ya fani hiyo ili taasisi hiyo iendelee kuwa na heshima na kuaminiwa na jamii.

Mapema  Mkurugenzi wa Bahari FM Bw. Yusuph Omar Chunda kupitia ziara hiyo aliwashauri    wajumbe wa kamati hiyo kudumisha ushirikiano uliopo baina ya serikali hasa baraza la wawakilishi na vyombo vya habari.

“ Baraza la Wawakilishi likiwa na ushirikiano mzuri na waandishi wa habari, tunaamini hata serikali yetu itakuwa mstari wa mbele kuwa karibu zaidi na sisi hivyo tunakuombeni ushirikiano huu usiishie Bahari FM tu, bali hata kwa taasisi zingine zinazofanya kazi sawa na sisi kwani sote tunafanya kazi moja ya kupigania maendeleo ya nchi.”, alisisitiza Chunda.

Chunda ambaye pia ni Gwiji wa fani ya habari, aliahidi kuyafanyia kazi kwa vitendo maelekezo na ushauri uliotolewa na Kamati hiyo ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji ndani na nje ya taasisi hiyo.

Ujumbe huo ulioongozana na Naibu waziri wa habari, utalii, utamaduni na michezo, Mh. Chuom Kombo Khamis, mbali na bahari FM pia wametembelea vituo kadhaa vya habari vya kibinafsi.
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.