LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 2, 2017

RC PWANI AAGIZWA APIGE KAMBI MIONO BAGAMOYO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa (pichani kulia) akiwa ameongozana na Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Eng. Evarist Ndikilo alipofanya ziara ya kikazi mkoani humo.
*Waziri Mkuu amtaka amalize migogoro ya wakulima, wafugaji

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Eng. Evarist Ndikilo apige kambi katika kata ya Miono wilayani Bagamoyo na kuwasaka wafugaji wanaopiga wakulima.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo wakati akizungumza na wakazi wa kata hiyo ambao walisimamisha msafara wake wakati akienda kukagua miundombinu ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani iliyoko wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.

Akitoa kero za eneo hilo, Diwani wa Kata ya Miono, Bw. Juma Mpwimbwi alisema kata hiyo inakabiliwa na tatizo la wakulima kupigwa na wafugaji na wakipelekwa kituo cha polisi hawachukuliwi hatua yoyote.

“Wafugaji wanatupiga lakini wenzetu hawachukuliwi hatua na hata ukienda kushtaki polisi, hawakai kwa sababu wanadai wao wana fedha,” alisema diwani huyo.

Pia alisema mbali ya kero sugu ya maji, waliahidiwa barabara ya lami tangu miaka saba iliyopita lakini hadi sasa hawana hata kipande kidogo tu cha barabara hiyo.

Naye Bw. Shabani Mkwimbi ambaye alipewa nafasi ya kuzungumza kwa niaba ya wananchi wenzake, alisema kata hiyo ina kituo cha polisi na mahakama lakini utendaji kazi wa viongozi waliopo hapo unatia shaka.

“Waziri Mkuu tunataka ukimaliza kuongea na sisi, uondoke na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Miono, Bw. Maro na msaidizi wake Bw. Rashidi pamoja na Hakimu wa hapa, kwa sababu hawa watu habari yao ni nyingine. Mkulima akienda polisi au mahakamani hashindi kesi hata siku moja, lakini mfugaji akienda anashinda,” alisema huku akishangiliwa.

“Hawa watu wanadai wana hela na wanafanya chochote wanachotaka, na ndiyo maana hawalali polisi hata kama wameua mtu,” aliongeza.

Akijibu kero zao, Waziri Mkuu aliwahakikshia wakazi hao kwamba Serikali iliyopo madarakani ni yao na hakuna hata mtu mmoja ambaye yuko juu ya sheria.

Alisema suala la polisi wa kituo cha Miono litashughulikiwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, ambaye alikuwepo katika msafara wake. “Tena Mkuu wa Mkoa yuko hapa na yeye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huu, atasimamia hilo.”

Akifafanua kuhusu suala la wafugaji kuwapiga wakulima, Waziri Mkuu alisema msimamo wa Serikali ni kuwaona wakulima wanafanya kazi zao kwa uhuru na wafugaji nao wanafanya kazi zao kwa uhuru. “Hakuna mfugaji anayeruhusiwa kupeleka ng’ombe wake kwenye mashamba yenye chakula. Hili haliruhusiwa hata kidogo,” alisisitiza.

“Mkuu wa Mkoa hili ni agizo. Njoo upige kambi hapa na watu wako, na usake  wahusika hadi wabainike. Ni lazima tuwajue ni akina nani wamehusika na hili,” alisema.

Aliwataka maafisa mifugo wa mkoa huo waende kwa wafugaji na kutambua mifugo waliyonayo na kama kuna maeneo wahakikishe wanapatiwa maeneo rasmi ili waweze kupatiwa matibabu kwa ajili ya mifugo yao.

Aliwataka wafugaji wanaokata mabomba ya maji ya mradi wa maji wa Chalinze (CHALIWASA) ili kupata maji ya kunywesha mifugo yao, waache tabia hiyo mara moja na akaonya kuwa watakaokamatwa, wachukuliwe hatua za kisheria mara moja. Katika ziara hiyo fupi, Waziri Mkuu alikuwa amefuatana na Mkuu wa Mkoa wa Mkoa pwani, Eng. Evarist Ndikilo, viongozi wa wilaya ya Bagamoyo na Mbunge wa jimbo hilo, Ridhiwani Kikwete.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages