Saturday, April 15, 2017

CCM YATOA POLE KWA RAIS DK. MAGUFULI KUFUATIA VIFO VYA ASKARI WANANE, YAMPONGEZA KUANZISHA UJENZI WA RELI YA KISASA, DAR-MORO

 IKULU, DAR ES SALAAM
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetoa salamu za pole kwa Mwenyekiti wa C CM Rais Dk. John Pombe Magufuli kufuatia kuuwawa kwa askari Polisi wanane  kwa kushambuliwa na watu wenye silaha katika eneo la Jaribu Mpakani, Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani.

Salamu hizo zimewasilishwa kwa Rais Magufuli na Katibu wa NEC  Itikadi na Uenezi Humphrey Polepole, Ikulu jijini Dar es Salaam, jana.

Akiwa ameambatana na Naibu Katibu Kuu CCM Tanzania-Bara Rodrick Mpogolo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania Amina Makilagi,   Polepole amesema kwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM ndio Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, hivyo ndio maana CCM imeshtushwa na tukio hilo na kutoa pole hizo kutokana na kuuwawa kwa askari hao ambao wamekuwa na jukumu kubwa la kulinda usalama wa wananchi na mali zao.

Amesema askari hao wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu wakati wote kuhakikisha watanzania wanakuwa salama pamoja na mali zao hivyo tukio la kuuwawa kwao ni jambo la kusikitisha sana.

Polepole amesema wamekutana na Rais na pamoja na kumpa pole wamemueleza mchakato wa Uchaguzi wa ndani wa CCM ambao unaendelea nchini kote kuanzia ngazi ya mashina hadi taifa.

Aidha amesema CCM inampongeza Rais Dk.Magufuli kwa kitendo cha kizalendo cha serikali ya awamu ya tano  kutumia fedha zake za ndani katika ujenzi wa Reli itakayokuwa na kiwango cha kimataifa yenye urefu wa kilomita 300 kutoka Dar es salaam hadi Morogoro.

Polepole amesema ujenzi wa reli hiyo yenye kiwango cha kimataifa itakayotumia treni ya umeme inadhihirisha jinsi CCM inavyojishughulisha na shida za watu.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, (CCM), Rais John Mgufuli, akiagana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), Amina Makilagi. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Bara Rodrick Mpogolo na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Humphrey Polepole.
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Bara na Katibu Mkuu wa Jumuia ya Wazazi Tanzania Amina Makilagi wakiondoka Ikulu
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.