Saturday, April 22, 2017

BALOZI SEIF ALI IDDI AONGOZA MAZISHI YA ALIYEKUWA KATIBU WA CCM WILAYA YAKUSINI UNGUJA, LEO

Waombolezaji wakienda kuzika leo
Na Mwandishi Wetu
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameongoza mamia ya waombolezaji wakiwemo viongozi, wanafamilia na wanachama wa Chama Cha mapinduzi, katika maziko ya Katibu wa CCM Wilaya ya Kusini Unguja Marehemu Hamdan Haji Machano yaliyofanyika leo katika kijiji cha Donge Mkoa Wa Kaskazini Unguja.

Akizungumza kwenye maziko hayo, Balozi Ali Seif Iddi, amesema , Chama cha Mapinduzi na Serikali wamepokea kwa mshtuko mkubwa sana msiba huo, ila ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu na kilichosalia ni kumpumzisha marehemu na kuongeza kuwa marehemu alikuwa na mchango mkubwa sana hasa katika wakati ule wa chaguzi mbalimbali hususani katika uchaguzi mkuu.

"Hatusahau kazi kubwa aliyoifanya na niwahakikishie familia tutaendelea kuwa nanyi katika kila hatua ili kuenzi mchango wake" Alisema Balozi Seif wakati akiwasilisha salamu za rambirambi kwenye maziko hayo.

Marehemu Hamdan Haji Machano alizaliwa tarehe 16 Octoba 1963 katika kijiji cha Donge wilaya ya Kaskazini B na alipata elimu na kumaliza kidato cha nne mwaka 1968- 1979, na pia aliweza kupata nafasi mbalimbali katika Umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kijijini kwao Donge hadi alipoajiriwa rasmi na Umoja Wa Vijana wa CCM kuanzia tarehe 1/6/ 1996 kwa uteuzi katika cheo cha katibu wa UVCCM wilaya.

Katika nafasi ya katibu wa wilaya ameweza kufanya kazi katika wilaya za Tanga mjini, Kusini Unguja, Mkinga, Kaskazini Unguja, Mjini Unguja na baadae Mwaka 2012 aliteuliwa kuwa katibu wa Vijana Mkoa wa Magharibi kisha kuhamishiwa afisi kuu ya UVCCM Zanzibar kama afisa idara ya Usalama na Maadili ambayo aliitumikia mpaka mwaka 2014 alipoteuliwa kuwa katibu wa CCM wilaya ya Kusini Unguja kazi aliyoitumikia mpaka umauti ulipomkuta Jana mchana katika hospitali Kuu ya Mnazi mmoja Zanzibar.

Viongozi wengine walioshiriki maziko hayo ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wa CCM Zanzibar Dk Abdalla Juma Sadalla,
Kaimu Katibu Mkuu UVCCM Shaka Hamdu Shaka, Wajumbe Wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa, Wenyeviti wa mikoa CCM, Wenyeviti wilaya Chama na Jumuiya zake na watendaji wa chama na jumuiya zake kutoka mikoa ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara. Marehemu ameacha watoto saba na wake wawili.Share:

KUCHAGUA LUGHA

IDADI YA WATU AMBAO HUTEMBELEA BLOGU HII

KUMBUKUMBU ZA POSTI ZOTE

JISAJILI UPATE TAARIFA KWA EMAIL

Jisajili ili upate taarifa kwa email

Google+ Followers

Powered by Blogger.