Thursday, March 30, 2017

RAIS DK. MAGUFULI APONGEZWA KUIWEZESHA TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE

Frank Mvungi-Maelezo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amepongezwa kwa kuiwezeshaTaasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kufanya upasuaji wa kihistoria tangu kuanzishwa kwake.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo na Daktari Bingwa wa Moyo Dkt. Bashir Nyangassa wakati wa hafla fupi ya kuwaaga madaktari bingwa wa moyo kutoka Hospitali ya Saifee ya Mumbai nchini India waliosaidia kufanikisha upasuaji huo wa kuvuna  mishipa ya damu mguuni na kupandikiza katika mishipa  ya moyo iliyoziba (CABG-Coronary Artery Bypass Graft) kwenye moyo .

Upasuaji huu uliwahusisha madaktari 6 toka Hospitali ya Saifee umesaidia kuwaongezea ujuzi wataalamu wa Taasisi hiyo na kuokoa fedha nyingi ambazo zingetumika kuwasafirisha nje wagonjwa ili waweze kupata matibabu.
“Kama wagonjwa hawa wangeenda kutibiwa nchini India Serikali ingelipia zaidi ya shilingi bilioni 2.1 kama gharama za matibabu” Alisisitiza Dkt. Nyangassa. “

Akizungumzia upasuaji mwingine uliofanyika  kwa wagonjwa 8 Dkt. Nyangassa amesema kuwa ni upasuaji wa milango miwili hadi mitatu ya moyo ambayo ilikuwa na matatizo kwa kuibadilisha.

Kwa upande wa upasuaji wa bila kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa Cath Lab tumetoa huduma mbalimbali za matibabu ya moyo bila kufungua kifua (catheterization) kwa wagonjwa 12 ambao tumezibua mishipa ya damu ambapo mgonjwa mmoja mshipa wake ulikuwa umeziba kwa asilimia 100” Aliongeza Dkt. Nyangasa.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo  kutoka  Hospitali ya Saifee ya nchini India Dkt. Yunus Loya amesema kuwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete umeonyesha mafanikio makubwa na utakuwa wa kudumu.

Aliongeza kuwa Taasisi ya Moyo ya Kikwete ina wataalamu wazuri na siku za usoni watakaobobea zaidi na hivyo Tanzania itanufaika sana na uwepo wa Taasisi hiyo.

Tangu kuanza kwa mwaka huu Taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau wake wa nje ya nchi imefanya upasuaji bila kufungua na kufungua kifua kwa wagonjwa 79.

Mwaka 2016 Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Bohara Duniani Mtakatifu Dkt. Syedna Aliqadr Mufaddal Saifuddin alifanya ziara yake hapa nchini na katika ziara hiyo kiongozi huyo alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Dkt. John Magufuli na kumuahidi kuleta madaktari wa moyo. nchini watakaoshirikiana na Madaktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na kufanya matibabu kwa wagonjwa.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo kutoka Hospitali ya Saifee, ya Mumbai nchini India Dk. Aliasgar Behranwala (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo wa JKCI Dkt. Bashir Nyangasa na Mkurugenzi wa Upasuaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge (katikati) mara baada ya kumaliza kambi ya siku tatu ya upasuaji wa Moyo katika Taasisi hiyo leo Jijini Dar es Salaam, ambapo madaktari wa JKCI walishirikiana na Madaktari 6 kutoka nchini India. Madaktaria hao wamekuja nchini kufuatia ahadi ya Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Mabohora Duniani Mtakatifu Syedana Muffadal Saifuddin Saheb kwa Rais Dkt. Magufuli alipomtembelea Ikulu Jijini Dar es Salaam mapema tarehe 13, Oktoba 2016.
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.