Tuesday, March 21, 2017

PLAN INTERNATIONAL YAADHIMISHA MIAKA 80 YA KUZALIWA

 Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
 Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Plan International limeadhimisha miaka 80 tangu kuzaliwa kwake Mwaka 1937 likiwa na lengo la kutetea na kusimamia haki za Watoto pamoja na usawa wa kijinsia.

Maadhimisho hayo yamefanyika jana Duniani kote katika nchi ambazo shirika hilo linafanya kazi, kwa Tanzania maadhimisho yamefanyika katika Mikoa yote ambayo ina ofisi za shirika ambapo wafanyakazi waliofanya kazi zaidi ya miaka 20 walitambuliwa.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo- Tanzania, Jorgen Haldorsen amesema shirika la Plan limesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha maisha ya Watoto na wasichana wengi duniani tangu kuzaliwa kwake na litaendelea kutimiza malengo yaliyowekwa ya kuhakikisha haki za watoto zinalindwa na usawa wa kijinsia unapatikana ikiwa ni njia moja wapo ya kuchochea maendeleo ya nchi husika.  

”Leo shirika letu linatimiza miaka 80 tangu kuanzishwa kwake, ni safari ndefu tena yenye mafanikio makubwa ingawa bado kuna mengi ya kufanya ili kuhakikisha haki za watoto na wasichana zinalindwa ulimwenguni kote kama yalivyokuwa malengo ya John-Langdon-Davies ambaye ndiye muanzilishi wa shirika hili,”Alisema Haldorsen.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa ingawa shirika hilo linakua na kubadilika kulingana na muda lakini lengo la kuhakikisha watoto na wasichana wanayafikia malengo yao waliyojipangia haliwezi kubadilika kwani wanatambua kuwa unyanyasaji wa watoto wa kike na uvunjwaji wa haki za watoto ndiyo sababu moja wapo ya kukithiri kwa umasikini katika nchi nyingi.

Haldorsen amefafanua,ili kutatua changamoto hizo wamejikita katika kutoa Elimu na ulinzi kwa watoto ambapo amekiri kuwa kazi hiyo imewezekana kwa sababu ya ushirikiano mkubwa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wafadhili pamoja na wadau mbalimbali. 

Aidha, mnamo miaka ya 1980 wakati shirika likiadhimisha miaka 50 ya kuzaliwa kwake ilikuwa ni mwaka muhimu kwa shirika kwani ndio siku ambayo walitambuliwa rasmi na Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) kama moja ya shirika la Kimataifa linaloshughulikia Watoto na Wasichana.

Kwa Tanzania shirika hilo limenza tangu mwaka 1991 likisaidia watoto pamoja na jamii nzima katika kuboresha Afya, Elimu Ulinzi na Ajira.Mwaka 2000 shirika lilianzisha Ofisi katika Wilaya tano za Vijijini na moja ikiwa mjini na mwaka 2011 shirika lilianzisha shughuli zake za kupeleka misaada katika Mikoa 14 Tanzania Bara na Visiwani.

Mikoa hiyo inajumuisha Dar es Salaam, Mtwara, Lindi, Ruvuma, Morogoro, Dodoma, Iringa, Rukwa, Kigoma, Geita, Mwanza, Mara na Visiwa vya Zanzibar
Share:

KUCHAGUA LUGHA

IDADI YA WATU AMBAO HUTEMBELEA BLOGU HII

KUMBUKUMBU ZA POSTI ZOTE

JISAJILI UPATE TAARIFA KWA EMAIL

Jisajili ili upate taarifa kwa email

Google+ Followers

Powered by Blogger.