Tuesday, March 14, 2017

MAKAMU WA RAIS APOKEA TAARIFA YA AWALI YA UTEKELEZAJI WA UAMUZI WA KUHAMIA DODOMA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na  Viongozi na Wadau wa mkoa wa Dodoma kwenye mkutano wa kazi ambapo Taarifa ya Awali ya mkoa wa Dodoma na utekelezaji wa uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma iliwasilishwa katika ukumbi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

Na Mwandishi Maalum


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Samia Suluhu Hassan ameuagiza uongozi wa mkoa wa Dodoma uhakikishe unaondoa vitendo vya ukiritimba kwa baadhi ya watendaji wa serikali ambavyo vinaweza kusababisha ucheleweshaji au kukwamisha ujenzi wa miji mipya mikubwa mitano ya kisasa katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dodoma.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo 14-Mar-2017 wakati akifanya mazungumzo na viongozi wa mkoa wa Dodoma baada ya kupokea taarifa ya Kikosi Kazi kilichoundwa na serikali kwa ajili ya kuratibu shughuli mbalimbali za Serikali kuhamia Dodoma.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema ni muda muafaka sasa hivi kwa uongozi wa mkoa wa Dodoma kujiimarisha na kujipanga ipasavyo katika kupokea wawekezaji wenye nia njema ya kuwekeza kwenye sekta mbalimbali mkoani humo hasa wakati huu ambao serikali inahamia Dodoma.

Ameonya kuwa wawekezaji matapeli kamwe wasipewe nafasi ya kuwekeza Dodoma na ametaka uongozi wa mkoa wa Dodoma kuwa makini makundi hayo ili wasije kuvuruga mipango ya serikali ya kujenga Makao makuu ya kisasa katika Manispaa ya Dodoma.

Makamu wa Rais pia ameuagiza uongozi wa mkoa wa Dodoma kulinda na kuendeleza maeneo yote yenye uoto wa asili ili yasije yakaharibiwa kutokana na uwekezaji utakaofanyika mkoani humo.

Amesema amefurahishwa na kasi ya uongozi wa mkoa wa Dodoma jinsi unavyojipanga katika kuhakikisha azma ya serikali ya kuhamia Dodoma inafanikiwa kwa haraka ikiwemo utengaji wa maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda na huduma za kijamii.

Kuhusu maeneo ya wafanyabiashara wadogo, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa mkoa wa Dodoma wahakikishe wanatenga haraka maeneo maaluma kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo ili nao waweza kunufaika na mpango wa Serikali kuhamia mkoani Dodoma.

“Ni muhimu maeneo yote yatakayotengwa kwa ajili wafanyabiashara wadogo  yawe huduma zote za msingi ili kusaidia wafanyabiashara hao waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi “Amesisitiza Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa ni muhimu kwa uongozi wa mkoa wa Dodoma kuwashirikisha viongozi wa wafanyabishara wadogo kuhusu maeneo yatakayotengwa ili kuondoa malalamiko kutoka kwa wafanyabishara hao kupewa maeneo yasiyofaa wa ajili ya shughuli zao.

Awali kabla ya kumkaribisha Makamu wa Rais kuzungumza na viongozi wa mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Dodoma Jordan Rugimbana alimweleza Makamu wa Rais mipango na mikakati ya mkoa huo kuhusu azma ya serikali ya kuhamia Dodoma ikiwemo uimarisha wa huduma za msingi ikiwemo afya, miundombinu, maji na elimu.

Mkuu huyo wa mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana amesema mpaka sasa kazi ya kuainisha maeneo mbalimbali kwa ajili ya uwekezaji, makazi na mahali ambapo ofisi za serikali na za mabalozi zitajengwa umeshakamilika.

Amesema uongozi wa mkoa wa Dodoma utaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali, mashirika ya kimataifa na mabalozi ili kuhakikisha maeneo  yaliyotengwa yanaendelezwa haraka.

Ameeleza kuwa ujenzi wa miji Mitano mikubwa mkoani Dodoma na ujio wa wawekezaji mbalimbali utaufanya mkoa huo kuwa na uhitaji nishati ya umeme ya uhakika hivyo amehimiza ujenzi wa bomba la gesi asili kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma ukafanyika haraka.
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

CCM Blog. Powered by Blogger.