Tuesday, March 21, 2017

MAKALA YA CHARLES CHARLESKingunge asidhani kuwa Kikwete, Mangula au Kinana 'watachafuka' kwa kuwatungia uongo 


Na Charles Charles
JUZI, Jumapili, mwanachama wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kingunge Ngombale - Mwiru alinukuliwa na gazeti moja la kila siku nchini, akidai kuwa hatua ya karibuni ya kuadhibiwa kwa baadhi ya waliokuwa wanachama,  ni mwendelezo wa makosa yaliyofanywa mwaka 2015 yakiongozwa na viongozi wakuu watatu wa chama hicho kilichopo madarakani. 

Viongozi aliodai kuwa kimsingi ndio wanaopaswa kubeba dhamana ya usaliti ndani ya CCM ni Mwenyekiti Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete; Makamu Mwenyekiti (Tanzania Bara), Philip Mangula na Katibu Mkuu, Komredi Abdulrahman Kinana. 

Alidai kuadhibiwa kwa viongozi kadhaa ikiwemo kufukuzwa uanachama kati yao, kusimamishwa uongozi ama kupewa onyo kwa makosa ya usaliti siyo jambo jipya, badala yake ni mwendelezo wa makosa yaliyotokea wakati wa mchakato wa kutafuta mgombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho mwaka 2015.

Kingunge ambaye mwaka huo alijivua uanachama wa CCM kwa kuzingatia Ibara ya 13(1)(f) ya Katiba ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 1977 Toleo la 2012 iliyokuwa ikitumika hadi siku tisa zilizopita, alidai kwamba Kikwete, Mangula na Kinana kwa pamoja, walifanikiwa kuishawishi Kamati Kuu ya CCM kuvunja Katiba na Kanuni zake. 

Kutokana na hali hiyo, mzee huyo ambaye sasa ni mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema Kamati Kuu ilishindwa kufanya kazi zake kama inavyoelekezwa na Katiba na Kanuni na kujikuta imekataa kuwaona, kuwasikiliza ama kuwahoji wana CCM 38 waliokuwa wameomba uteuzi wa kugombea nafasi ile ya urais.

"Hawa waliohukumiwa, wamehukumiwa kwa usaliti wa kuendana na mchakato wa kumpata mgombea urais (mwaka 2015). Sasa swali linalokuja hapo ni je, nani aliyesalitiwa? Ni CCM ndiyo imesalitiwa au kuna mgombea fulani maalum (wa urais) ndiye amesalitiwa?" Alihoji. 

Akizungumzia utaratibu, Kingunge pia alisema kuwa Kamati ya Maadili ni kitengo kilichopo ndani ya Ofisi ya Katibu Mkuu, hivyo haitambuliwi ndani ya Katiba ya CCM, lakini alificha ukweli kwamba michakato yote ya chaguzi katika chama hicho huzingatia Katiba na Kanuni. 

"Kwa hiyo, Kamati ya Maadili haina majukumu ya Kikatiba ya kuwa na kauli juu ya nani awe au asiwe mgombea, lakini inaweza kuishauri CC (akimaanisha Kamati Kuu) na NEC (ama Halmshauri Kuu ya Taifa) na Kamati hiyo haiwezi kutoa ushauri wa kuvunja Katiba na anayeshauriwa ndiye mwamuzi ", alisema. 

Lakini wakati mzee huyo akidanganya hivyo kutokana na chuki zake za sasa za kisiasa katika upande wa kwanza, na pia kutokana na mahaba yake makubwa kwa aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa aliyehama naye kutoka CCM mwaka 2015 anajua, tena kwa usahihi kuwa kuna Kanuni za Uongozi na Maadili Toleo la Februari, 2010 ambazo alishiriki kuzitunga na bado zinaendelea kutumika hadi sasa. 

"Katiba ya Chama ndiyo sheria kuu ya Chama Cha Mapinduzi inayoonyesha Organaizesheni ya Chama, Malengo na Madhumuni ya Chama. Vilevile inaainisha Haki, Wajibu wa Mwanachama, Sifa, Miiko, Majukumu ya Utendaji, Uongozi na Vikao vya Chama", kinasema Kifungu Kidogo cha Nne cha Utangulizi cha Kanuni za Uongozi na Maadili kinachozungumzia Katiba ya Chama Cha Mapinduzi na kuongeza:

"Utekelezaji wa Katiba ya CCM umefafanuliwa pia katika Kanuni mbalimbali za Chama kama zilivyotolewa na kusimamiwa na Halmashauri Kuu ya Taifa. Kufuata na kutii Katiba ya CCM na Kanuni zake ni wajibu wa kila mwanachama wa CCM".

Mbali na kifungu hicho, Ibara ya 2(2)(i) inayozungumzia "Muundo wa Kamati ya Usalama na Maadili" inasema:

"Ni dhahiri kwamba kazi za Kamati za Usalama na Maadili zitakuwa muhimu sana katika kipindi hiki (cha uchaguzi), na kwamba kazi hizo zitaongezeka. Lakini haitawezekana kuzisimamia kwa ufanisi kazi zote hizi kutoka Makao Makuu; lazima usimamizi wa Maadili ufanywe na kila ngazi ya uongozi kutoka taifa hadi tawi la CCM.

"Kwa hiyo, Kamati za Usalama na Maadili zitaundwa katika kila ngazi, na kwa jinsi kazi zenyewe zilivyo, Kamati hizo lazima ziwe ndogo ili kutunza siri. Kwa hiyo, Muundo wa Kamati hizo utakuwa ufuatao:

"(i) Ngazi ya Taifa 

(a) Mwenyekiti wa CCM - Mwenyekiti
(b) Makamu wawili wa Mwenyekiti wa 
      CCM - Wajumbe
(c) Katibu Mkuu wa CCM - Katibu 
(d)  Makamu wa Rais - Mjumbe
(e)  Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara na 
       Zanzibar - Wajumbe
(f)  Wajumbe wanne wa Kamati Kuu, 
       wawili kutoka Bara na wawili kutoka
       Zanzibar, (jinsia ikizingatiwa) - 
       Wajumbe" (mwisho wa kunukuu). 

Tukizingatia ushahidi huo, Kingunge anakujaje na uongo kwamba Kamati ya Usalama na Maadili ni kitengo tu cha ndani ya Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM? 

Hivi kwa mfano hivi sasa maana yake ni kuwa Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli; Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar),  Dk. Ali Mohammed Shein; Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Philip Mangula au Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Samia Suluhu Hassan ni watumishi wa Kitengo cha Maadili ofisini kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana? 

Kuhusu Majukumu ya Kamati ya Usalama na Maadili, Ibara ya 3(1) - (2) ya Kanuni za Uongozi na Maadili inasema, na hapa ninanukuu:

"Kikao chenye jukumu la Kikatiba la kusimamia mwenendo mzima wa nidhamu ya Chama ni Halmshauri Kuu ya Taifa, lakini madaraka ya utekelezaji yamo mikononi mwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa. 

"Kwa hiyo, wajibu wa Kamati ya Usalama na Maadili ya kila ngazi ya Uongozi wa Chama ni kuiwezesha Kamati Kuu kutekeleza kwa ufanisi zaidi kazi zake za siku kwa siku za kusimamia nidhamu ya wanachama na viongozi wa CCM ndani ya mfumo wa vyama vingi. Kamati Kuu ndiyo itakayoamua jambo gani lifikishwe Halmashauri Kuu ya Taifa na lifikishwe (kwa) namna gani".

Aidha,  Ibara ya 3 ya Kanuni za Uongozi na Maadili inayohusu kazi za Kamati hiyo katika kila ngazi, Kifungu Kidogo cha (vii) kinasema ifuatavyo:

"Kwa sababu hiyo, Kamati za Usalama na Maadili zitachambua kwa makini ubora wa wanachama wanaoomba uongozi, ama viongozi wanaoteuliwa katika ngazi mbalimbali za Chama, kabla vikao vinavyohusika havijatoa idhini ya kuwaruhusu wateuliwe kugombea uongozi huo au wateuliwe kushika nafasi zilizokusudiwa".

Je, mpaka kufikia hapo Kingunge bado ana nyongeza gani kuhusu upotoshaji wake kuwa eti Kamati ya Usalama na Maadili ni kitengo, tena ambacho kimo ofisini tu kwa Katibu Mkuu wa CCM? 

Ni kweli kuwa kwa ushahidi huo wote kuhusu Kanuni za Uongozi na Maadili kwa kunukuu Ibara ya 1(iv), 2(1) - (2)(i)(a) - (f), 3(1) na (3)(vii), Kingunge bado ana swali ama uongo mwingine kuhusu uwepo, uhalali na majukumu ya Kamati ya Usalama na Maadili? 

Kuhusu madai kuwa Kikwete, Mangula na Kinana walifanikiwa kuishawishi Kamati Kuu ya CCM kuvunja Katiba, Ibara ya 109(6) ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 1977 Toleo la 2012 iliyokuwa inatumika wakati huo inasema, na hapa pia nanukuu:

"Unapofika wakati wa uchaguzi, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa itashughulikia mambo yafuatayo", kisha Kifungu Kidogo cha (b) ndipo kinabainisha kuwa:

"Kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmshauri Kuu ya CCM ya Taifa juu ya majina ya wanachama wasiozidi watano wanaoomba kugombea kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania".

Katika kutimiza jukumu lake hilo mwaka 2015, Kamati Kuu ilipendekeza majina matano ya aliyekuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) anayesimamia Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe.

Wengine ni Balozi Mstaafu wa Umoja wa Afrika (AU) katika Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, Amina Salum Ali; aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli na aliyekuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba. 

Je, mpaka hapo Kikwete, Mangula na Kinana wanawezaje kuingizwa katika uongo huo kwamba eti walifanikiwa kuishawishi Kamati Kuu ya CCM kuvunja Katiba na Kanuni zake?

Au, kama ni kweli walifanya hivyo na Kamati Kuu kuteua majina hayo matano badala ya sita, saba, nane, tisa au zaidi na kupelekwa NEC kwenda kuchujwa na kubaki matatu yaliyopelekwa kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa, kule ambako hatimaye alipatikana mgombea urais huo ni usaliti au ni kukidhi matakwa ya Katiba?

Nafahamu pia kuwa Kingunge alikuja na shutuma kuwa Kamati Kuu haikuwaita ili kuwaona, kuwasikiliza ama kuwahoji wana CCM 38 waliokuwa wakiomba uteuzi wa kugombea urais kwa sababu kubwa moja tu: kukatwa kwa jina la rafiki yake aliyetaka awe ndiye Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Edward Lowassa. 

Kama huo ni uongo kama inavyoweza kudaiwa na baadhi ya wapambe wake mwenyewe, wapambe wa Lowassa na hata vinginevyo, mbona hakuonyesha ibara ama kifungu cha Katiba au Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM kilichokiukwa?

Jambo la mwisho ninalotaka kulitolea ufafanuzi hapa ni madai kuwa, wana CCM ambao wameadhibiwa "wamehukumiwa kwa usaliti wa kuendana na mchakato wa kumpata mgombea urais" mwaka 2015.

Sitaki kuwataja wale waliovuliwa uanachama, kusimamishwa uongozi au kuonywa kwa sababu kila mfuatiliaji wa masuala ya kisiasa anawafahamu, lakini sikubaliani na madai eti kwamba wameadhibiwa kutokana na kumuunga mkono "mgombea fulani maalum ambaye ndiye aliyesalitiwa" au kuporwa haki yake!

Swali linalokuja hapa ni je, ni ibara gani ya Katiba au Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM inayogawa makundi wagombea urais, kwamba kuna wengine ni maalum na hata vinginevyo? 

Ingawa sitaki kusema undani kuhusu jambo hili, lakini waliovuliwa uanachama ni baadhi ya wasaliti walioihujumu CCM kutaka ishindwe uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2015.

Hawakuadhibiwa kutokana na sababu nyingine yoyote isipokuwa hiyo. Wapo ambao wakati huo walikuwa "wana CCM mchana", lakini ikifika usiku hubadilika na kuungana na wapinzani kwa kuwasaidia washinde. 

Wapo waliofanya hivyo na kujitanda kwa baibui kusudi wasifahamike sura zao, na pia kuna wengine waliokuwa wakivujisha siri zote za mikakati ya CCM kwenda Chadema, Civic United Front (CUF) au vyama vingine vya upinzani nchini. 

Wapo wana CCM waliowapigia kampeni wapinzani, na pia kuna wengine waliotoa mpaka raslimali fedha, watu au magari yao na kadhalika ili mradi tu washinde na kukamata madaraka ya dola. 

Hapo ndipo nahitimisha kwa kusema Kingunge asidhani kuwa Kikwete, Mangula au Kinana anaweza 'kuwachafua' kwa kuwatungia uongo.

Kidumu Chama Cha Mapinduzi!
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.