HABARI MPYA

Your Ad Spot

Mar 26, 2017

HUMPHREY POLEPOLE AFAFANUA KWA KINA MAGEUZI YA CCM

Mabadiliko ya Katiba ya CCM 2017 yamegusa maeneo gani?
Hivi karibuni kumekuwapo maneno ya upotoshwaji juu ya Mabadiliko ya Katiba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yaliyofanyika tarehe 12 Machi 2017. Napenda kufafanua kwa uchache maeneo ambayo yamefanyiwa Mabadiliko ili kuanzia sasa ieleweke bayana kwamba msingi wa Mabadiliko haya ni Mageuzi Makubwa ambayo yanafanywa na Chama chetu ili kuongeza tija, ufanisi, uwajibikaji, kupunguza gharama za uendeshaji, kupiga vita rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.

Mageuzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yanalenga kutizama Uongozi (Leadership), Muundo/Mfumo (Structure/System) na Utawala (administration). Chama chetu kimetimiza miaka 40 mwaka huu (2017) tangu kuanzishwa kwake na kipindi hiki tumeazimia kwa kauli moja kukiimarisha, kukijenga na kukifanya madhubuti. Kazi hii ya Mageuzi ya CCM ilianzishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM iliyokaa katika Mkutano wake wa mwenzi Desemba 2016 na baadaye kupitishwa kwa sauti moja na Mkutano Mkuu Maalum wa Machi 2017.

Ikumbukwe kwamba mabadiliko haya ya Katiba yangaliweza kupendekezwa na kuanza kutumika pasina ya kuitisha Mkutano Mkuu, lakini hekima ya Uongozi wa Chama chini ya Mwenyekiti Ndugu Magufuli na Katibu Mkuu Ndugu Kinana ikatuongoza kwamba Mabadiliko haya ambayo yanajenga msingi wa Mageuzi ya Chama chetu lazima yashirikishe wanachama wetu.

CCM kama chama cha siasa ili kifanye kazi yake vizuri na yenye matokeo makubwa chanya, ilikusudiwa lazima kihuishwe ili kiweze kwenda na wakati na kutekeleza matakwa ya wanachama, kwa kuzingatia ukweli kuwa lengo kuu la chama chochote cha siasa ni kushika dola.

Mabadiliko ya Kikatiba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yana lengo la kukiimarisha chama chetu ili kuziteka hisia, mioyo na fikra za watanzania wengi, kwa nia ya kukiunga mkono katika lengo lake la kushika dola na kuleta maendeleo endelevu kwa watanzania.

Katiba ya CCM imekuwa ikifanyiwa marekebisho mara kwa mara tangu ilipotungwa mwaka 1977, kwa madhumuni ya kuiboresha ili iendane na wakati uliopo. Kwasababu hiyo, yamekuwepo matoleo 12 ya Katiba hii hadi mwaka 2012. Katiba ambayo imepitishwa na Mkutano Mkuu Maalum tarehe 12 Machi 2017 jijini Dodoma, inakuwa toleo la 14.

Mabadiliko haya yanalenga kurekebisha Muundo, Mfumo, Uongozi, Utendaji na mengineyo.

Mambo muhimu ambayo yamezingatiwa katika marekebisho haya ni yafuatayo; -

MFUMO WA CHAMA
Mfumo wa Chama, una sura ya serikali na utawala na kuwa na ngazi nyingi ya vikao vya uamuzi. Hali hii inafanya gharama ya kukiendesha Chama kuwa kubwa, vikao haviitishwi na maamuzi ya chama hayawafikii walengwa. Hivyo basi yafuatayo yanazingatiwa,

Kupunguza wingi wa vikao vya nadharia na badala yake kuwa na vikao vichache vinavyofanyika, vyenye maamuzi yenye tija na kujenga uhai wa chama.

Kupunguza idadi ya wajumbe au wawakilishi ili wawe wachache lakini wenye umakini na uwezo wa kusimamia sera, itikadi, maamuzi ya chama pamoja na kuondoka urasimu na kupunguza gharama za uendeshaji pasina kuathiri ubora wa uwakilishi.

Muundo wa Wilaya za Chama uendane na uundo wa sasa wa wilaya za Serikali

Uztio mkubwa umewekwa katika kuimarisha chama katika ngazi ya shina, eneo ambalo ndilo waliko wapiga kura. Kwa kufanya hivyo, chama kitakuwa karibu na watu na watakiona kuwa ni chama chao.

Uendeshaji wa shughuli zote za jumuia za chama na mali zake uwe chini ya usimamizi wa Chama cha Mapinduzi na Baraza la Wadhamini la Chama cha Mapinduzi.

VIONGOZI

Viongozi wachache wamekuwa na tabia ya kujilimbikizia nafasi nyingi za Uongozi, utendaji na uwakilishi katika Chama na Serikali. Hali hii hushusha ufanisi na kupunguza tija. Nafasi nyingi kwa mtu mmoja ni kushindwa kuleta ufanisi katika vikao husika.

Hapa imezingatiwa kuwa; ukiacha wale wanaolazimishwa kikatiba kuwa na nafasi zaidi ya moja kwa mujibu wa mamlaka yao, kuanzia sasa nafasi za Uongozi katika chama zitakuwa si zaidi ya moja.

KURA YA MAONI
Mfumo wa kura za maoni hukusudia kuimarisha demokrasia ndani ya chama na kuashiria nafasi ya mgombea anayeonekana kukubalika zaidi. Hata hivyo, eneo hili limekuwa na matokeo mabaya ya kukithiri kwa rushwa na kupata viongozi wasio na imani ya kweli ya chama wanaosaka maslahi, wafanyabiashara wenye malengo binafsi na mamluki.
Mapendekezo ya kuimarisha udhibiti wa kura za maoni; -

Katiba ya CCM ya Mwaka 1977 Toleo la 2012 Ibara ya 61A(1-3) inaelekeza kura za maoni za ubunge na uwakilishi zitapigwa kwenye mikutano mikuu ya jimbo na si kwa wanachama wote matawini kama ilivyofanyika mwaka 2015.

Imependekezwa ili kudhibiti taratibu za kura za maoni jimboni, kuepusha migawanyiko, kuziba mianya ya rushwa na kuepusha wapiga kura mamluki, inapendekezwa kufanya mabadiliko ya upigaji kura za maoni za ubunge na uwakilishi pamoja na kufuata utaratibu ufuatao wa kuwajadili wanaogombea;

Wagombea ubunge/uwakilishi watachukua fomu na kurudisha kwa Katibu wa CCM wa Wilaya inayohusika. Fomu zote za wagombea ubunge/uwakilishi zitajadiliwa na kutolewa mapendekezo katika ngazi ya wilaya, mkoa na Taifa kabla ya kupigiwa kura za maoni.

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa itateua majina yasiyozidi matatu ambayo yatawasilishwa mbele ya Mkutano Mkuu wa Jimbo kwa ajili ya kupigiwa kura za maoni. Mkutano Mkuu wa Jimbo utapiga kura za maoni kumpendekeza mwanachama mmoja awe mgombea wa ubunge/uwakilishi katika jimbo hilo.

Mara ya baada ya kura za maoni, mapendekezo ya uteuzi yataanzia kwenye Kamati ya Siasa Jimbo (kwa Zanzibar), Kamati ya Siasa ya Wilaya (Tanzania Bara), Mkoa, Kamati Maalum (Kwa Zanzibar), Kamati Kuu na hatimaye Halmashauri Kuu ya Taifa itafanya uteuzi wa mwisho.

Utaratibu huu hautawapa fursa wagombea kutengeneza makundi na kutoa rushwa kwasababu hakuna anayejua kama atakuwepo kwenye orodha ya wagombea. Wale wana CCM wenye tabia ya kujiandaa na vyama zaidi ya kimoja, kwa utaratibu huu hawataweza kujiandaa mapema kuhamia vyama vingine. Utaratibu huu pia utasaidia kuondoa urasimu na migawanyiko isiyokuwa na sababu.

Aidha, utaratibu huu utahakikisha anapatikana mgombea mwenye msimamo thabiti wa Chama na ni utaratibu halisi kwa chama kuusimamia ipasavyo.  Itaendelea…

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages