Wednesday, March 8, 2017

DC GONDWE APOKEA MSAADA WA MBEGU KUTOKA WORLD VISION

Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe (wa kwanza kushoto) pamoja na  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. William Makufwe wakipokea mbegu za mahindi ya njano kutoka kwa Msimamizi wa mradi Bw. Kelvin Metta wa World Vision.
  Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondweakiwa ameshikilia mbegu za miche ya Viazi, kushoto ni Mkurugenzi  Mtendaji, kulia Kaimu Afisa kilimo Bi. Rosemary Bughe,Wakuu wa Shule  na Maafisa ugani  wakipata maelekezo mafupi kuhusu mbegu.
Kaimu Afisa kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bi. Rosemary Bughe  akiwa ameshikilia kifurushi kimojawapo cha mbegu za miche ya mihogo.


Halmashauri ya Wilaya ya Handeni imepokea mbegu za mhogo, mahindi na viazi lishe katika kuhamasisha kilimo cha mazao yanayostahimili ukame na kuboresha kiwango cha elimu kwa kuwapatia chakula wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Mbegu hizo zilizotolewa na shirika lisilo la kiserikali la World Vision kwa Tarafa za Mkumburu na Kwamsisi katika wilaya ya Handeni mkoani Tanga na zitasambazwa kwa shule 20 za msingi na nne za sekondari zikiwa ni juhudi za shirika hilo kuunga mkono juhudi za serikali za kuhamasisha kilimo cha mazao yanayovumilia ukame na kuboresha kiwango cha elimu kwa kuwapatia chakula wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Akipokea mbegu hizo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe alilishukuru shirika la World Vision kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Wilaya ya Handeni za kuhamasisha kilimo cha mazao yanayoendana na mabadiliko ya tabia nchi. 

“Mbegu hizi zitakuwa mfano kwa watu wa Handeni na kubadilisha fikra za wakulima kwa kulima mazao yanayovumilia ukame ili kuendana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo ilikuwa kampeni kubwa ya wilaya ya Handeni ya kuhamasisha watu kulima zao la mhogo, viazi na mazao mengine yanayostahimili ukame” alisisitiza Gondwe.

Aliongeza kuwa mbegu hizo zitasaidia kupata chakula kwa wanafunzi na kusaidia kuboresha afya na kuinua kiwango cha taaluma. “Mashamba yatakayolimwa mbegu hizi yatakuwa mfano bora kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya shule. Halmashauri itaweka mfumo mzuri ambao utakuwa utakuwa ni mkataba baina ya Mkurugenzi na walimu wakuu na wakuu wa shule kuonesha kuwa wanawajibu wa kuhakikisha mbegu hizo zinakuwa” alisema Gondwe. 

Mkuu huyo wa wilaya alielekeza shughuli za kilimo katika mashamba ya shule kufanyika katika muda wa elimu ya kujitegemea ili kuwawezesha wanafunzi kupata elimu yao kwa mujibu wa ratiba. Aliwataka maafisa ugani kuzitembelea shule zote zitakazonufaika na mbegu hizo na kutoa elimu bora ya upandaji wa mbegu hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Handeni, William Makufwe alisema kuwa Halmashauri yake inachangamoto ya watoto kutohudhuria vizuri darasani kutokana na njaa na kudidimiza kiwango cha ufaulu. “Juhudi hizi za wadau zinaunga mkono juhudi za Halmashauri za kuboresha afya na kiwango cha taaluma kwa wanafunzi wetu. Halmashauri imeagiza mbegu za mhogo ambazo zitasambazwa kwenye kata” alisema Makufwe.

Mratibu wa mradi katika Tarafa ya Mkumburu Kelvin Metta, alisema kuwa World Vision wametoa mbegu za mahindi ya njano aina ya seed SC40 inayokomaa kwa muda mfupi itakayopandwa kwa shule za msingi 13 na sekondari 2 kwenye ekari 32 katika ADP Mkumburu. Miche ya viazi lishe kwa ajili ya ekari 16 za shule za msingi na sekondari katika Kata ya Kwamgwe na Kwedizinga. 

Kwa upande wa mratibu wa mradi katika Tarafa ya Kwamsisi Bw. Nicodemus Fadhili alisema kuwa shirika limetoa mbegu za miche ya mhogo 660 itakayolimwa kwenye ekari 20, mbegu za miche ya viazi lishe 9,500 zitakazopandwa kwenye ekari 36 na mbegu za mahindi ya njano kg 270 aina ya CP201 zitakazopandwa kwenye ekari 27. 

Alda Sadango

Afisa Habari

Halmashauri ya Wilaya Handeni
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.