Sunday, February 5, 2017

NIIONAVYO CCM MPYA, TANZANIA MPYA


Nianze kwa kuitakia heri ya kumbukizi ya miaka 40 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi, chama kinachoendelea kushika dola ya Tanzania toka kiasisiwe mwaka 1977 ambalo ni zao la vyama vya TANU na ASP.

Misingi mizuri iliyojengwa na waasisi wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Nyerere (Tanganyika- Bara) na Abeid Amani Karume (Zanzibar - Visiwani) imesababisha Wananchi wa Tanzania kwa muda mrefu kuishi kwa amani na utulivu huku wakifanya mambo yao kwa uhuru bila ya kuingiliwa na mtu yeyote Yule.

Tofauti na mataifa mengine Watanzania wako huru zaidi kwenda kokote kule ndani ya nchi na hata kuishi au kufanya kazi ama biashara bila ya bughudha yoyote endapo taratibu na sheria zitazingatiwa vyema.

Hali hii ni tofauti na nchi nyingine zikiwemo za jirani kama vile Kenya , Kenya Rwanda, Burundi, Kongo na hata Uganda ambapo ukabila umetalaki kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa lakini kwa Tanzania hakuna ubaguzi wa rangi,dini wala kabila.

Hiyo inatokana na uongozi imara, sera safi, upendo na kila aina ya ubora uliotukuka ndani yake kwa jamii ya kitanzania. Jambo linaloendelea kutia faraja ni kuwa tangu ianzishwe CCM imeendelea kuwa ni chama kinachotawala na kuongoza nchi. Na siri yote ya mafanikio hayo ni kutokana na kuwa nguzo imara ambazo ni Wanachama, Ilani ya chama, na Viongozi wake.

Wanachama wake ambao ndio mtaji wa chama ambao ni zaidi ya milioni nne na nusu na mashabiki wapatao ama zaidi ya milioni 10. CCM ni.....
chama kisichozingatia uwepo au hata harufu ya ubaguzi wa rangi, kabila au dini ya mtu.

Hatua hio imewafanya Watanzania wengi kuanzia vijana kwa wazee, wake kwa wanaume kujivunia kuwa wanachama makini wa chama chenye mtazamo chanya wa kuwavusha kwenye neema. Ili kuhakikisha CCM inapata makada wa aina tofauti bila ya kujali umri, jinsia ilianzisha jumuiya za wazazi, wanawake (UWT) na vijana (UVCCM) ambazo ni viungo muhimu vya chama katika kuwaweka watu wote pamoja na karibu na hivyo kuendelea kuwa chama cha kishujaa katika kuwakomboa watu wake.

Pia kuna suala zima la uwepo wa ilani ya uchaguzi ambayo ni mkataba baina ya chama na wananchi au viongozi na wananchi ambao ndio wapiga kura wenyewe kupitia ilani, CCM inatoa ahadi zake mbalimbali za kutekelezwa katika muda uliopangwa wa miaka mitano.

Ni wazi kwamba ahadi hizo zimekuwa zikitekelezwa kwa kiwango kikubwa na cha kuridhisha kiasi cha kufanya Watanzania waendelee kuwa na imani nayo kila uchaguzi unapowadia. Hii inajidhihirisha wazi katika chaguzi kuu mbalimbali zilizofanyika mara tatu 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015 ambapo CCM iliibuka na ushindi wa kishindo

Nguzo nyingine kuu ya CCM ni viongozi wake. Ndani ya CCM wenye dhamana ya chama ni wanachama wenyewe na wala si viongozi. Hali hii imesaidia kutokuwa na hata chembe au harufu ya umini wa mtu kujiona kuwa ana haki miliki ndani ya chama au ni kiongozi wa maisha. Ikumbukwe kuwa CCM ina haki zote kwa kiongozi yeyote yule aliyetokana na CCM.

Hiyo ni ishara kwamba ni chama chenye misingi imara ya uongozi na ndio maana kumekuwa na mabadiliko ya mara kwa mara ya uongozi kwa kufuata misingi ya katiba ya chama. Kila baada ya mitano hufanyika uchaguzi wa viongozi wa mashina hadi Taifa na katika uchaguzi huo ndipo watu huingia na kutoka.

Aidha hali hii ni tofauti na vyama vingine nchini ambavyo walivyoviasisi ni viongozi wa kudumu hadi hii leo. Wanapoambia kuna uchaguzi baadhi ya viongozi hao kufanya mizengwe kwa wale wanaonyesha nia ya kuleta mabadiliko na hata kuwafukuza.

Kwa sasa CCM ipo chini ya Uenyekiti wa Rais Dk. John Pombe Magufuli ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha inaendelea kuongoza kupitia ridhaa ya Wananchi.

Ridhaa hii inatokana na CCM kuendelea kuwa na uongozi imara, sera safi, maendeleo bora na hivyo kuendelea kuwa tegemeo la kila Mtanzania anayependa haki na maendeleo pamoja na ustawi uliopo.

Hakuna binadamu aliyemkamilifu kwa kila kitu isipokuwa Mungu pekee. Kwa kulitambua hilo CCM iliona si vizuri endapo wataendelea kuwa peke yao. Mwaka 1990 uliletwa mswada na mwaka 1992 walio wachache (20%) wakapatiwa ushindi wa uletaji wa mfumo mpya ule wa vyama vingi.

Hivyo CCM ndiyo mkunga na mwanzilishi wa mfumo wa vyama vingi nchini. Tangu kuasisiwa kwake CCM imeendelea kuwa mkunga na kinara ndani ya utiriri wa vyama mbalimbali takribani 20 vya kisiasa vya hapa nchini.

Pia CCM hii imeendelea kuwa chama cha kimaskini kinachowakumbatia watu maskini na hii inajidhihirisha zaidi kupitia shughuli za kimaendeleo zinazofanywa na serikali za CCM zinazokuwa madarakani ambazo zote zina walenga watu maskini na watu wote kwa kuwa ujumla bila ya kujali rangi, dini wala kabila la mtu.

Lengo la kuanzishwa kwa CCM kulikuwa na malengo ya kumkomboa Mtanzania haswa Mkulima na mfanyakazi (kupitia nembo ya jembe na nyundo) ili kumfanya aweze kupiga hatua kimaendeleo. Hivyo hatutakosea endapo tutasema kuwa CCM ni chama cha kimapinduzi ya kweli na dhihiri mathalani CCM imekuwa daima chama tawala kinachopinga maradhi, ujinga na umasikini. Vile vile CCM kimeendelea kuwa mstari wa mbele kuleta maendeleo ya kiuchumi kijamii na kiutamaduni.

Mathalani katika elimu, kupitia mipango yake MMEM (Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi) na MMES (Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari) kumuwezesha kuwepo kea ongezeko la idadi ya Wanafunzi katika shule.

Hii inatokana na uwepo wa sera safi ya kuhakikisha kuwa kuna shule za Msingi katika kila kijiji na uwepo wa shule za Sekondari katika kila kata. Hali hii imesaidia uwepo wa shule 15,816 shule za msingi na shule 2,171 kwa shule za sekondari

Pia Serikali za CCM zimechakalikia uwepo wa vyuo mbalimbali ambapo mpaka sasa kuna jumla ya vyuo 47 hapa nchini toka vyuo 3 vilivyikuwepo wakati tunapata uhuru. Mfano ya vyuo hivyo ni chuo kikuu cha Dar es salaam “Mlimani” (UDSM) na matawi yake ambayo ni chuo cha Elimu Chang’ombe (DUCE) ;Chuo cha Madaktari Muhimbili; Chuo cha MKWAWA; Chuo cha ardhi (U-class).

Vyuo vingine vikuu ni pamoja na chuo cha kilimo cha Sokoine; Chuo kikuu cha Mzumbe, na chuo kikuu cha Dodoma (U – Dom) ambacho ni chuo kipya chenye uwezo wa kuchukua zaidi ya wanafunzi 40,000.

Upatikanaji wa maji vijijini 1961 ulikua 6% sasa ni 68%. Upatikanaji wa maji mijini 1961 ulikua 25% sasa ni 83%.

Upande wa huduma za kiafya; hospitali 1961 zilikua 48 sasa zipo 109. Zahanati 1961 zilikua 239 sasa zipo 6114.

Upande wa Elimu; Shule za msingi 1961 zilikua 3000 sasa zipo 16538. Walimu wa shule za msingi 1961 walikua 9885 sasa wapo 88905. Shule za sekondari 1961 zilikua 41 sasa zipo 4753. Walimu wa sekondari mwaka 1961 walikua 764 sasa wapo 88908.

Kwa mujibu wa Baraza la Mitihani NECTA ni kwamba mwaka 2016 ufaulu wa jumla umeongezeka kwa asilimia 2.56 kutoka asilimiq 67.53 mwaka 2015 hadi asilimia 70.09 mwaka 2016.

Upande wa Miundo mbinu, tulikua na km za barabara za lami 1300 zenye ukubwa wa kilomita 33,600 mwaka 1961 na sasa kuna kilomita 124,234 na zingine zinaendelea kukamilika kujengwa.

Serikali za CCM zimefanikiwa kuleta unafuu katika elimu na hata kuleta unafuu wa wanafunzi na kwa wazazi ama walezi wao kwa kuhakikisha kuwa elimu ya shule ya msingi ni lazima kila mtoto wa miaka saba na inatolewa bure; kila Mtanzania awe na elimu angalau ya kidato cha nne; kuondoa kero za ada za mitihani kwa shule za msingi na sekondari.

Wakati tunapata uhuru (1961) kulikuwa na Watanzania milioni 9 kati ya hao ni watu wasiozidi laki tatu waliobahatika kupata elimu ya darasani na waliokuwa darasani kipindi hicho hawakufika wanafunzi 1,500.

Takribani miaka 56 sasa baada ya uhuru, CCM imeendelea kuliongoza taifa letu lenye watu wapatao Milioni 45 (kwa mujibu wa sensa ya watu iliyofanyika nchini mnamo mwaka 2012) kwa kuhakikisha wanapatia elimu ya kutosha na yenye viwango. Leo hii asilimia kubwa ya Watanzania wameelimika hadi elimu ya ngazi ya chuo, na kwa mujibu wa takwimu za sasa kuna wanafunzi wapatao milioni 15 wakiendelea na masomo yao kwa ngazi mbalimbali kati ya hao kuna wanazuoni wapatao 120,000.

Hata kwa upande wa mikopo ya elimu ya juu nako CCM ipo bega kwa bega na jamii kwa kuhakikisha kuwa kila Mwanachuo anapatiwa mkopo wa gharama za elimu ya juu kwa kadri uwezo wa kifedha utakavyokuwa.Katika mwaka wa masomo wa 2005/2006 Bodi ya Mikopo ilitoa mikopo kwa  wanafunzi 42,729 iliyogharimu sh.  bilioni 56.1  na mwaka wa masomo wa 2016/2017 bodi ya mikopo ilitoa mikopo  iliyogharimu shilingi bilioni 487 kwa hapa nchini kuna changamoto kubwa cha kiwango hiki lakini tusisahau ya kwamba kiwango hiki na idadi hii ya wanafunzi wanaonufaika ni kikubwa mno ambacho hakiwezi kufikiwa na nchi yeyote ile ya Afrika Mashariki na kati. Nani kama CCM?

Hata kwenye mapambano ya dhidi ya ‘maradhi’ nako jitihada si za kubezwa. Tumeshuhudia ujenzi wa vituo vya afya kwenye kila kijiji na ujenzi wa zahanati kwenye kila kata Kwa mfano jumla ya Zahanati 5,422 na vituo vya afya 663 vimejengwa ndani ya utawala wa CCM. ; pia kuna uwepo wa hospitali kubwa kila mkoa mathalani Muhimbili hapa Dar es salaam, Bugando kule Mwanza na kadhalika.

Serikali za CCM hazina mzaha katika mapambano ya dhahiri dhidi ya Malaria, kifua kikuu, ukoma, matende trakoma, saratani za aina zote. Pia kuna mapambano dhidi ya magonjwa ya milipuko kama vile kipindupindu, kichocho, homa ya mafua ya ndege na yale mafua ya nguruwe.

Licha ya hapo, pia kumekuwa na maboresho ya dhati ya Afya ya mama na mtoto, upungufu wa vifo vya uzazi kwa utoaji wa elimu ya uzazi, kuongeza idadi ya wakunga na utoaji wa huduma ya kujifungua katika kiwango cha hali ya juu.

Katika kuhakikisha kuwa kila mtu maskini na asiyejiweza anapatiwa huduma sawa na sahihi kumekuwa na sera safi ya utoaji wa huduma bure za matibabu kwa makundi maalum kama vile walemavu ,vipofu, wazee wa zaidi ya miaka 60, na watu maskini wasiojiweza ilimradi tu apatiwe uthibitisho kutoka kwa Serikali za mitaa.

Pia kuna utoaji bure wa huduma za matibabu kwa magonjwa ya milipuko ndani ya jamii na hata pia wale wahanga wa majanga mbalimbali hawajasahaulika. Jamani kama haya si mafanikio ya Serikali za CCM ni kitu gani hasa?

Wahenga walisema, ‘Mnyonge mnyongeni, lakini haki zake mpeni’. Licha ya maneno mengi mno yasiyo na tija kusemwa semwa mitaani lakini kwa upande wa Serikali za CCM hawajavunjika moyo na daima wanazidi kusonga mbele kwa mbele. Baadhi ya viongozi kulumbana, ama matokeo ya uchaguzi kuteteleka ni sehemu tu mapito ya chama chochote kile cha kisiasa hapa Duniani ambapo unachukuliwa kama msingi mkuu wa maboresho ya chama husika.

Sote kwa pamoja tumeshuhudia na ujenzi na maboresho ya miundombinu, hakikisho la kilimo safi, mapambano dhidi ya ubadhilifu wa mali za umma, mapambano makali ya rushwa na ufisadi nchini, uanzilishwaji wa vyanzo vya ndani ya mapato ili tuweze kujitegemea wenyewe na kadhalika.

Tawala zote za CCM zilielewa ile dhana ya kuwa nchi haiwezi kuwa na mazingira mazuri ya kiuchumi iwapo miundombinu ya uchukuzi na usafirishaji itakuwa duni na isiyotosheleza mahitaji.

Katika serikali zake zimeendelea na ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya nchi bila ya kujalisha ni nani anaongoza na ni kwa awamu gani. Hata katika utawala wa awamu ya tano ya Rais Magufuli ameendeleza kazi nzuri na safi iliyofanywa na waliomtangulia.

Serikali za CCM hazina mzaha kabisa katika kuhakikisha kuwa rasilimali tulizonazo zinawasaidia Watanzania na kuhakikisha wanakusanya kodi ipasavyo kwa kukuimarisha vyanzo vilivyopo pamoja na kuanzisha vyanzo vipya ambapo mpaka mwaka huu 2017 mapato ya nchi yetu yameongezeka mara dufu hadi kufikia shilingi Trilioni 1.5 kwa mwezi mmoja. Nani kama CCM?

Serikali za CCM zimeendelea kufanya mengi mazuri ambapo kwa upande wa Zanzibar imefanikiwa kuondoa viashirio vya mvunjiko wa mshikamano, amani na utulivu waliokuwa nao kwa kuiondoa ile hali iliyotaka kuwatawala ya kununiana, kutokusalimiana, hadi ilifika kipindi watu walishindwa kuzikana. Leo hii hali ni tofauti kabisa kwani ile hali ya aibu imeshawaondoka na ule umoja wa Kitaifa, upendo, mshikamano na nguvu ya pamoja imerejea tena. Yote hayo yamewezekana chini ya himaya za utawala wa CCM.

Nyakati zote chama cha mapinduzi wameonekana kuguswa na kero na shida za Watanzania kwa kukata kiu ya kwikwi ya umaskini wa watu wake kwa kuwaletea maendeleo ya kweli. Hakika CCM ndio mama na mama ndio ajuaye uchungu wa mwana.

Mathalani kwa upande wa kilimo. Serikali za CCM haziko nyuma kwenye harakati za mapigano ya kilimo bora hapa nchini. Imefahamika kwamba zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania ni wakulima ambao wanategemea kilimo kama nguzo ya maisha yao. Katika kuhakikisha kuwa kilimo kinaboreka zaidi na kuepusha mabalaa ya njaa kumekuwepo na uanzishaji wa kauli mbiu mbalimbali za kilimo.

Kauli mbiu hizo za kilimo ni kama vile, kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa (1967); Siasa ni kilimo (1971); Kilimo cha kufa na kupona (1974); na kilimo kwanza (2009). Hakika matokeo chanya ya harakati za sera hizo zimekuwa zikionekana kwa dhahiri.

Katika idara ya ubadhilifu wa mali za umma nako harakati za mapambano hazikuwa nyuma. Tumeshuhudia idara mbalimbali zikibanwa mbavu kwa uthibiti imara kabisa tofauti na mitazamo hasi ya baadhi ya watu yalivyo. Mifano husika ni katika idara za maliasili, uvuvi, bandari, madini, chakula ambapo kote kumekuwa na uthibiti tulioshuhudia wa mapato na rasilimali za Watanzania.

CCM hii hii imekuwa mstari wa mbele kupambana na mafisadi (hawa ni wahujumu uchumi wanaotafuna rasilimali na mali za umma) Serikali za CCM imeweza kuvipa nguvu idara za kisheria ili kuweza kupambana na aina yeyote ilaya ubadhilifu na uhujumu uchumi. Kwa kutambua mgawanyo wa mihimili ya madaraka vimeachiliwa vyombo husika kufuatilia ili haki ipatikane bila kuhujumu upande wowote. Huu ndio utawala wa kisheria.

Mbali na hayo yapo mambo mengi ambayo CCM imefanya mapinduzi zaidi kupitia sera na ilani ambazo zipo kwa ajili ya kumlinda, kumtetea na kumkomboa mtu wa tabaka la chini na kati ambao ndio , asilimia kubwa ya Watanzania.

CCM inaundwa na Wanadamu ambapo inafahamika vyema kuwa Binadamu si Malaika hajakamilika na kwa kuwa CCM ipo kama Mwanadamu nayo pia haijakamilika, kuna sehemu imefanya vizuri sana, kuna sehemu imefanya vizuri na kuna sehemu pia haijafanya vizuri. CCM kama chama cha kisiasa chchote kile Duniani hakitaweza kumridhisha kila Mtu kwa kiwango kile kinachotaka.

Lakini hali hiyo haitaweza kufuta mazuri ambayo CCM kupitia serikali zake zilizokuwa na iliyopo madarakani kujivunia mafanikio yaliyopatikana toka enzi za kulikomboa Taifa letu toka kwa wakoloni Waingereza mpaka hapa ilipoifikisha.

Wakati CCM ikiadhimisha miaka 40 ya kumbukizi ya kuzaliwa kwake haina budi kubadilika na kuendana na kasi ya Mwenyekiti wake Rais Magufuli, kuendana na kasi ya Hapa Kazi Tu. Heri ya kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi.

Na Emmanuel J. Shilatu

0767488622
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.