Saturday, February 11, 2017

KONA YA SHERIA: HAKI YA MTOTO KUFANYA KAZI


Haki ya  mtoto kufanya kazi imeanishwa katika sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009. Kwanza kabisa Sheria hii inatambua umuhimu wa mtoto kufanya kazi pale inapotamka, ‘Mtoto atakuwa na haki ya kufanya kazi nyepesi na kuwa mtoto ana haki ya kulipwa ujira kulingana na thamani ya kazi aliyofanya’. Kwa mujibu wa Sheria kazi nyepesi kwa mtoto zinajumuisha kazi ambazo hazina madhara kwa afya na maendeleo ya mtoto na hazimzuii mtoto au kuathiri maudhurio ya mtoto shuleni, kushiriki katika programu za mafunzo ya ufundi au uwezo wa mtoto kufaidika na kazi za shuleni.
Ifahamike kuwa umri wa chini wa mtoto kuajiriwa ni miaka kumi na nne, kwa mujibu wa Sheria hapa Tanzania. Hivyo kabla ya kumuajiri mtoto, mwajiri unapaswa ujiridhishe kuhusu umri wake, na pili kama ajira unayompa mtoto huyu ni ‘nyepesi’ kwa mujibu wa Sheria na kama tulivyoielezea hapo juu.

Vilevile, kila mwajiri anapaswa kuhakikisha kuwa kila mtoto aliyeajiriwa au kushughulishwa kulingana na Sheria hii analindwa dhidi ya ubaguzi au vitendo vinavyoweza kuwa na madhara kwa mtoto kwa kuzingatia umri wake na uwezo wake wa kushiriki. Mfano halisi hapa ni kuwa kazi ‘nyepesi’ kwa mtoto wa umri wa miaka 17 inaweza inaweza isiwe nyepesi kwa mtoto mwenye umri wa miaka 14. 

Busara itumike katika kumpangia mtoto majukumu kazini kulingana na uwezo wake/umri wake. Kwa mujibu wa Sheria, kumpa mtoto kazi bila kuzingatia umri wake ni unyonyaji.

Sheria ya Mtoto inasema kuwa kazi itachukuliwa kuwa ya kinyonyaji iwapo inadhuru afya ya mtoto au kuathiri maendeleo yake; inazidi saa sita kwa siku; hailingani na umri wake; au kama mtoto anapata malipo pungufu. Vitendo vya kinyonyaji katika ajira za watoto ni kosa la jinai lenye adhabu isiyopungua miezi sita jela ama faini!

Sheria ya Mtoto inakataza watoto kuajiriwa au kushughulishwa katika mkataba wa huduma ambao utamtaka mtoto kufanya kazi usiku. Hivyo ni kosa la jinai kumpangia mtoto kazi masaa ya usiku! ‘Kazi za usiku” inatafsiriwa na Sheria hii kujumuisha utendaji wa kazi ambao utamtaka mtoto kuwa kazini kati ya saa mbili usiku na saa kumi na mbili asubuhi’.

Vipi kuhusu kumlazimisha mtoto kufanya kazi? Sheria ya Mtoto inatamka kuwa mtu atakayeshawishi, atakayemtuma, atakayemtaka au atakayemlazimisha mtoto kufanya kazi atakuwa ametenda kosa la jinai. ‘Kazi za kulazimisha’ zinajumuisha kazi za kulazimishwa au aina nyingine yoyote ya kazi anayopewa mtu kwa vitisho vya kupewa adhabu lakini hazitajumuisha kazi za kawaida za kiraia, huduma ndogo ndogo za kijamii zinazofanywa na wanajamii zenye maslahi ya moja kwa moja kwa jamii hiyo.

Mtoto hapaswi kupewa kazi hatarishi kwa mujibu wa Sheria. Kazi hatarishi zinajumuisha - kazi za ubaharia; uchimbaji madini au upasuaji mawe; ubebaji wa mizigo mizito; viwanda vya uzalishaji ambamo kemikali zinazalishwa au kutumika; kufanya kazi katika sehemu ambazo mashine zinatumika; na kufanya kazi katika sehemu kama vile baa, hoteli na sehemu za starehe. Kamwe moto asiajiriwe katika kazi au biashara yoyote itakayompelekea kujihusisha na masuala ya kimapenzi kwa malipo au la!

Imeandaliwa na:
Augustino Chiwinga.
Legal Officer.
0756 810804.
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.