Saturday, January 14, 2017

SUMAYE ALIKUWA ANAOTA AU ALIKOSA MANENO YA KUZUNGUMZA?

SUMAYE ALIKUWA ANAOTA AU ALIKOSA MANENO YA KUZUNGUMZA? 
Na Charles Charles
Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye amedai kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kitashinda uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2020. 

Sumaye ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alisema chama hicho pia kinataka kuona mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini ukifanya kazi tofauti na jinsi unavyoonekana hivi sasa. 

Aliyesema hayo jana, Ijumaa Januari 13, 2017 wakati akisalimia kwenye kikao cha ndani cha viongozi wa Chadema mjini Shinyanga. 

MAJIBU YA MADAI YAKE HAYO 
Sumaye aliyesema hayo kutokana na sababu kubwa zifuatazo:
(1) Alisema hivyo kwa vile huo umekuwa ni utamaduni wa kila kiongozi wa kisiasa wa upinzani nchini anapozungumza na wanachama, viongozi ama wafuasi wa chama chake.

Maneno ya kusema CCM itaondoka madarakani yamekuwa yakitolewa kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita, ndoto ambayo hatimaye imechuja. 

Walisema "mwisho wa CCM" ungekuwa mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015, lakini kwa miaka hiyo yote kitashinda na pengine kuwa mwisho wa kisiasa wa walewale waliokuwa wakitangaza kuwa ingeng'oka madarakani.

Yuko wapi Augustine Lyatonga Mrema?  Yuko wapi Mabere Nyaucho Marando na kadhalika ambao wote kwa vinywa vyao wenyewe walisema "mwisho wa CCM" ungekuwa mwaka 1995? 

Yuko wapi Dk. Wilbroad Peter Slaa aliyesema kwamba "mwisho wa CCM" ungekuwa mwaka 2010? 

Badala ya kuwa "mwisho wa CCM" uligeuka kuwa mwisho wao na wafuasi wao. 

Kutokana na hali hiyo, kauli ya Sumaye siyo ya kwanza na haiwezi kuwa ya mwisho ila itaendelea, lakini siku zote itabaki kuwa haina maana yoyote kwa yeyote. 

(2) Mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa nchini upo na utaendelea kuwepo milele yote, lakini utakuwepo siyo kwa jinsi wanavyotaka viongozi wa Chadema isipokuwa kwa kuzingatia Katiba na sheria za nchi hii. 

Hauwezi kuwa kichaka cha kutukana wala kufanyia uchochezi, upotoshaji wa makusudi au wa kuvunjia sheria kwa kisingizio chochote. 

Ushahidi wa kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa nchini ni pamoja na kuwepo kwa Wabunge, Madiwani ama Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji kutoka vyama tofauti ambavyo ni pamoja na Chadema yenyewe. 

Wasiwasi alionao Sumaye ni mmoja tu: kwamba ameshaona mwelekeo wa kuzidi kudhoofika kwa Chadema, hivyo anachofanya ni kuanza kuwajengea mazingira wafuasi wao ya kuja kuwadanganya pindi wakishindwa tena mwaka 2020 kwamba wameibiwa kura zao kama wanavyofanya siku zote. 

Mungu Ibariki Tanzania! 

Charles Charles 
Msaidizi wa Katibu Mkuu wa CCM (Sera) 
Tarehe 14 Januari, 2017
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.