LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 31, 2017

SHIRIKISHO VYUO VYA ELIMU YA JUU-CCM, LAWATAKA VIJANA KUZIDISHA UADILIFU NA UZALENGO KUKIDHI LENGO LA RAIS DK. MAGUFULI

Kaimu Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu, Daniel Zenda akizungumza wakati wa kufungwa Kambi ya Vijana 219,  waliokuwa katika kambi ya kukuza Uzalendo, iliyowekwa Hombolo mkoani Dodoma.

NA MWANDISHI WETU
Shirikisho la vyuo vya Elimu ya Juu nchini, limewahimiza Vijana kuzidisha uadilifu na uzalendo ili kufikia malengo yatakayoakisi CCM mpya na Tanzania mpya, kama anavyotaka Mwenyekiti wa Chama, Rais John Magufuli.

"Ili matakwa haya ya Rais wetu na Mwenyekiti wa Chama, yaweze kufikika, ni lazima  Watanzania  hasa sisi vijana, tubadilike, kifikra na kimtazamo na kuacha kufanya kazi kwa mazoea", alisema Kaimu Katibu Mtendaji wa Shirikisho hilo, Daniel Zenda, wakati wa kufungwa kambi maalum ya siku tatu ya Vijana kutoka  vyuo mbalimbali, nchini, jana, Hombolo, mkoani Dodoma.

Zenda alisema, mabadiliko ya kifikra, mtazamo na kiutendaji, ndivyo vitakavyoonyesha udhati wa vijana na Watanzania kwa jumla katika kuendelea kumuunga mkono, Rais Dk. Magufuli, katika jitihada zake za kuiletea Tanzania mabadiliko makubwa ya kimfumo na kiutendaji kwa kushika misingi ya kuinua uchumi huku akipambana na uzembe na ubadhirifu.

Zenda, aliwapongeza vijana 219, walioshiriki katika kambi hiyo, akisema, mafunzo ya ukakamavu na yale ya kujenga utaifa, waiyopata kwa muda wa siku tatu hadi kufikia jana, yatawasaidia sana, katika kutambua nafasi yao katika kulitumikia taifa kwa uadilifu na uzalendo mkubwa.

Aliwataka Wanashirikisho la vyuo vya Elimu ya Juu katika mikoa mbalimbali kuendelea kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwa ni kutekeleza maagizo  yanayotaka kila mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuhakikisha anashiriki shughuli kama hizo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya miaka 40 ya kuzaliwa kwa CCM.

Zenda aliipongeza Viongozi wa Shirikisho katika baadhi ya mikoa ikiwemo Dar es Salaam, Mbeya, Arusha na Dodoma ambao tayari wamekuwa wakishirikiachama na wanachama na wananchi kwa jumla katika kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kufanya usafi na kujitolea damu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo ya miaka 40 ya CCM ambayo kilele chake ni Februari 5, 2017.

Kambi hiyo ya Hombolo ilifungwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainabu Abdalla Issa, ambaye akifunga kambi hiyo alisema, kwa kuwa CCM imekuwa ikionyesha kuwajali vijana kwa kuweka mipango mbalimbali ya kuwaendeleza sambamba na watanzania wengine, basi hawana budi nao kuhakikisha CCM inazidi kuimarika na kuwa CCM mpya.
HABARI KATIKA PICHA/>BOFYA HAPA

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages