LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 14, 2017

SAMIA: WANAOZINGUA JITIHADA ZA KUIJENGA CCM MPYA WASHUGHULIKIWE KIKAMILIFU

Mlezi wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Kaskazini na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia wakazi wa mkoa wa Kaskazini A, Unguja wakati wa Kufungua Mafunzo maalum ya Viongozi na watendaji wa Chama na Jumuiya zake wa ngazi ya Matawi, Wadi na Majimbo.
Wana CCM wa Kaskazini A wakiwa wamejitokeza kwa wingi kwenye mafunzo ya Uongozi yaliofunguliwa na Mlezi wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Kaskazini na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Makamu wa Rais  Samia Suluhu Hassan. 
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kaskazini A Unguja, Ndugu Juma Haji akihutubia kabla ya kumkaribisha Mlezi wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Kaskazini na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kufungua mafunzo maalum ya Uongozi yaliofanyika Mkokotoni Unguja kwenye Chuo cha Amali.


Na Mwandishi Maalum, Zanzibar
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa CCM katika Mkoa Kaskazini (A) Unguja kuwachukulia hatua stahiki wanachama ambao wanakisaliti na kuhujumu shughuli katika hatua ya kujenga CCM mpya.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo wakati anafungua mafunzo maalum ya viongozi na watendaji wa CCM na Jumuiya zake wapatao 556 katika ngazi ya matawi, wadi/tarafa na majimbo katika Mkoa wa Kaskazini (A) Unguja.

Samia Suluhu Hassan amesema kuwa hatua hiyo itasaidia chama kuimarisha shughuli zake kwa sababu chama kitakuwa na watu waadilifu na wenye nia ya kukisaidia CCM kusonga mbele na kupata ushindi mkubwa katika chaguzi zijazo.

Amesisitiza wanachama na viongozi wa CCM kote nchini waendelee kuweka mipango na mikakati imara itakayowezesha chama kuendelea kupata ushindi mkubwa na kushika dola.

Mjumbe huyo ambaye pia ni Mlezi wa CCM katika mkoa wa Kaskazini A Unguja amesema Umoja na Mshikamano miongoni mwa wananchama na viongozi ndio silaha madhubuti itakayowezesha chama hicho kuimarisha shughuli zake na kuongeza maradufu idadi ya wanachama nchini.

Amesema kwa sasa Viongozi watakiwa kujielekeza katika kufufua na kuimarisha jumuiya za chama ambazo katika baadhi ya maeneo hazifanyi kazi vizuri ili zianze kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia kanuni na taratibu za chama.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi(CCM) Taifa pia ameendelea kuonya baadhi ya viongozi waache tabia ya kutengeneza makundi ya ndani ya chama kwa ajili ya kusaka madaraka bali wawe mstari wa mbele katika kujenga umoja na mshikamano ndani ya chama. 

Kuhusu mafunzo, Samia Suluhu Hassan amewahimiza viongozi wanaopata mafunzo hayo kuyatumia vizuri ili kuhakikisha wanaporudi kwenye maeneo yao wanafanya kazi kwa bidii na kwa uaminifu mkubwa. 

Amesema kwa sababu Serikali iliyopo madarakani inatekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi ni muhimu kwa viongozi wa chama katika ngazi zote washirikiane na viongozi wa Serikali katika maeneo husika ili kuhakikisha miradi ya maendeleo ya wananchi inafanyika kwa ubora unaotakiwa kulingana na thamani ya fedha.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages