RAIS DK. MAGUFULI AOMBOLEZA VIFO VYA WATU 12 WALIOKUFA MAJI KWA BOTI TANGA

Dar es Salaam.
Rais Dk. John Magufuli, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martnine Shigela, kufuatia watu 12 kufa maji kufuatia boti waliyokuwa wakisafiria kutoka Tanga kwenda pemba, kuzama usiku wa kuamkia leo.

Ajali hiyo imetokea katika kisiwa cha Jambe  kilichopo katika bahari ya Hindi umbali mfupi kutoka Tanga Mjini, ambapo pamoja na vifo vya watu hao, wengine 33 wamenusurika na 25 kati yao wamelazwa katika Hospitali ya Bombo Mkoani Tanga.

"Nimeshtushwa na kusikitishwa sana na vifo vya watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali hii ya kuzama boti, tumepoteza wapendwa wetu, watoto wetu na watu wazima ambao kwa hakika familia zao ziliwategemea katika maisha ya kila siku, nakuomba Ndg. Mkuu wa Mkoa unifikishie pole nyingi kwa familia za Marehemu wote na jamaa zao" amesema Dkt. Magufuli katika salamu hizo.

Rais Magufuli amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi na pia amewasihi wote walioguswa na vifo hivyo kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki cha huzuni ya kuondokewa na jamaa zao na ndugu zao.

Pia amewatakia matibabu mema majeruhi wote walionusurika katika ajali hiyo ili wapone haraka, warejee katika familia zao na waendelee na ujenzi wa Taifa.

0 comments:

Post a Comment

Mdau, Uwanja huu ni wako, Toa maoni yako yasaidie kujua wewe unafikiri nini kifanyike kuboresha zaidi maisha ya Watanzania. Maoni yako yasilenge kuchochea mtafaruku katika jamii, kisiasa, kidini, kikabila au kijinsia. Mawasiliano yetu:- simu +255 (0) 712 498008, Email: nkoromo@gmail.com.
Bashir Nkoromo
Msimamizi Mkuu, Blog ya Taifa ya CCM.