LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 13, 2017

RAIS DK. MAGUFULI AKAMIA KUYATUMBUA MAGAZETI MAWILI HAPA NCHINI

Shinyanga, Tanzania
Rais Dk. John Magufuli, ameyaonya magazeti mawili ambayo bila kuyataja ameyashutumu kuwa yamekuwa yakiandika habari za uchochezi na za kupotosha.

Rais Magufuli ametoa onyo hilo leo, alipohutubia wakati akifungua Kiwanda cha cha vinywaji baridi cha Jambo, mkoani Shinyanga. Hotuba hiyo pamoja na ufunguzi vilitangazwa moja kwa moja na kituo cha Televisheni cha Star Tv.


Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, imemkariri Rais Magufuli akisema  kwamba Serikali yake haitayavumilia magazeti hayo kwa kuandika habari za upotoshaji na uchochezi ambazo zinaweza kuhatarisha amani ya nchi kama ilivyotokea katika nchini ya Rwanda na kusababisha mauaji ya kimbari nchini humo.


''Serikali ya kutumbua majipu haiwezi kuacha kutumbua magazeti yanayofanya mambo ya uchochezi. Hatuwezi kuiacha Tanzania ikawa dampo la eneo la kuweka maneno ya uchochezi chini ya utawala wangu hilo halitakuwepo, kuna magazeti mawili tu kila ukisoma wao ni kuchochea tu ikizungumzwa hivi wao wanageuza hivi, nasema na nataka wanisikie siku zao zinahesabika", Taarifa hiyo imemkariri Rais akisema.


Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Rais Magufuli amesema Serikali yake haiwezi kuvumilia kuona amani ya nchi inahatarishwa na magazeti mawili kwani amani ndio chimbuko la maendeleo ya taifa lolote duniani.


Amesema bila kuwepo kwa amani hakuna mwekezaji atakayeweza kuja kuwekeza nchi, hata wawekezaji wa ndani watashindwa na hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.


Rais Magufuli amesema uwepo wa amani nchini ndio uliowezesha wawekezaji wa Kiwanda cha Fresho cha kutengenezea mifuko ya kubebea bidhaa za chakula nchini na kiwanda cha Jambo cha kuzalisha vinywaji baridi mkoani Shinyanga kujengwa mkoani hapo kwani bila amani visingeweza kujengwa.


Taarifa imesema, wakati Rais akiyashutumu magazeti hayo mawili, lakini amevipongeza vyombo vingine vyote vya habari akisema, vimekuwa vikifanya kazi nzuri kwa kuandika habari za kweli zikiwemo za kumkosoa yeye na serikali yake, lakini bila kuingiza uchochezi au uongo.


Aidha ameitaka Benki ya Uwekezaji Nchini TIB na Taasisi nyingine za fedha kutoa mikopo kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika viwanda badala ya kuwakopesha wanasiasa ambao hutumia fedha wanazokopa kwa matumizi yasiyowanufaisha watanzania waliowengi


Rais Magufuli ameupongeza uongozi wa mkoa wa Shinyanga kwa kuanza kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya kutaka Tanzania ya viwanda kwa kujenga viwanda vingi mkoani humo ikiwa ni pamoja na viwanda hivyo viwili alivyovizindua katika siku yake ya mwisho ya ziara mkoani Shinyanga
.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages