Friday, January 13, 2017

MZEE MWINYI, MKAPA KUONGOZA MATEMBEZI YA 'WALK FOR ELPHANT DAR ES SALAAM 2017' KESHO JIJINI DAR ES SALAAM

Na Frank Shija-MAELEZO.
Marais wastaafu Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi, watakuwa wageni mashuhuri katika matembezi ya hiari ya kilomita tano yaliyopewa jina la 'Walk for Elephant Dar es Salaam 2017' yatayofanyika kesho kuanzia saa 12 asubuhi kwenye Ubalozi wa China na kumalizikia hoteli ya Sea Cliff.

Katibu Mkuu wa Chama cha Urafiki wa Tanzania na China (TCFPA) Joseph Kahama, amesema leo jijini Dar es Salaam, kwamba matembezi hayo yana lengo la kuonyesha umoja wa nchi hizo katika kupinga ujangili unaofanywa dhidi ya Tembo.

“Tunatarajia kuwa na matembezi ya kwa ajili ya kupinga ujangili dhidi ya Tembo ambapo wageni wetu mashuhuri wanatarajiwa kuwa Marais wastaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi na Mzee Benjamin Mkapa ambaye ndiye atakayepokea matembezi hayo katika Hotel ya Sea Cliff,” alisema Kahama.

Alisema zaidi ya watu 550 wamethibitisha kushiriki katika matembezi hayo wakiwemo baadhi ya watu maarufu kama vile mwilmbwede wa zamani Jokate Mwigelo na wasanii mbalimbali akiwemo Mrisho Mpoto.

Katibu Mkuu huyo alisema kuwa Chama cha Urafiki baina ya Tanzania na China(TCFPA) kimeanzishwa kwa nia ya kudumisha urafiki na uhusiano baina ya raia wa nchini hizo mbili.

Akijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kujua ni kwanin china imeamua kusaidia katika vita dhidi ya ujangili ili hali inatajwa kuwa miongoni mwa soko kubwa la bidhaa za meno ya Tembo, Kahama alisema kuwa Serikali ya China haiko tayari kuona nchi yake inatajwa kama soko la meno ya Tembo ndiyo maana Rais Xi Jinping wa China na Barrack Obama wa Marekani wamewahi kutoa tamko la pamoja la kupinga ujangili na ni kosa la jinai kwa raia wa China kukamatwa na nyara hizo.

Chama hicho kimekusudia kuifanya tarehe 14 mwezi wa kwanza kila mwaka kuwa siku ya matembezi ya Walk for Elphant Dar es Salaam 2017 ili kujenga utamaduni endelevu wa kupinga ujangili.
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.