LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 21, 2016

POLISI DAR ES SALAAM, WAMTIA MBARONI ANAYEDAIWA KUWA TAPELI SUGU


Msemaji wa Polisi, Advera  Bulimba – ACP
Na Dotto Mwaibale
JESHI la Polisi nchini limefanikiwa  kumkamata mtuhumiwa wa utapeli anayejulikana kwa jina la  Wilfred Masawe (36) mkazi wa  Buza, Temeke jijini Dar es Salaam.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam leo, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Kamishna Msaidi wa Polisi (ACP), Advera  Bulimba amesema  mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia mbinu mbalimbali kutapeli zikiwemo kujitambulisha kama kiongozi wa serikali kwa kutumia mtandao wa Whatsapp,  huku akieleza kuwa yupo nje ya nchi na kuna tatizo la msiba ambao umetokea nchini na unamuhusu na hivyo alikua akitoa maelekezo kwa watendaji wa serikali waweze kusaidia gharama za matibabu hospitalini, gharama za kusafirisha mwili wa marehemu na gharama za mazishi.

Alisema pia alikuwa akitumia mbinu ya kujifanya kiongozi mkubwa wa dini ya kikristo (Askofu) na kuwaambia waumini na viongozi mbalimbali kuhusu maandalizi ya makongamano ya kidini kwa lengo la kuwaomba michango kuweza kufanikisha makongamano hayo.

Alitaja baadhi ya matukio aliyofanikiwa kutapeli ni pamoja na kuwatapeli viongozi wa serikali, wafanyabiashara, mameneja na wakurugenzi wa taasisi za umma, wanasiasa pamoja na waumini wa madhehebu ya dini.

Aidha, matukio yote hayo alikuwa akiyafanya peke yake na alikua akiyaendesha kwa mawasiliano ya njia ya ujumbe mfupi (SMS) bila kuzungumza kwa simu.

Bulimba alisema Jeshi la Polisi linakamilisha taratibu za kisheria ili mtuhumiwa huyo afikishwe mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

Jeshi la Polisi nchini linaendelea kutoa tahadhari kwa wananchi wote kuwa makini na mtandao wa matapeli hao na yeyote mwenye  taarifa za matapeli anaombwa kuzifikisha haraka katika kituo chochote  cha Polisi kilicho karibu ili waweze kushugulikiwa haraka.



No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages