KHATIB: APITISHWA KUWANIA UMEYA WA MANISPAA YA MJINI Z'BAR

Na Is-haka Omar,  Zanzibar
MADIWANI wa Manispaa ya Mjini, wamempitisha Khatib Abdulrahman Khatib , kugombea nafasi ya umeya wa manispaa hiyo.

Uchaguzi huo ulimpendekeza meya huyo na kumpitisha baada ya kupata kura 27 za madiwani wote, hatua ambayo itamfanya kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi wa Meya kupitia Chama Cha Mapinduzi.

Khatib alipitishwa kuwania nafasi hiyo katika Mkutano uliofanyika  Ukumbi wa CCM Mkoa Mjini Amani Unguja ambapo mgombea huyo atachaguliwa kwa kuwa hakuna chama kingine chenye Madiwani ukiachia CCM na inatarajiwa atashika nafasi hiyo kwa mara ya pili. Kwa sasa Khatib ndie Meya wa Manispaa ya Mjini.

Madiwani hao pia walipitisha majina ya Naibu Meya ambaye ni Bimkubwa Said Sukwa aliepata kura 15, akimshinda mpinzani wake , Saleh Fasihi Saleh aliepata kura 12.

Kwa mujibu wa miongozo ya uchaguzi huo Majina hayo ya Meya na Naibu Meya yatapigiwa kura na wajumbe wa Baraza la Madiwani la Mjini.

Kupitia Uchaguzi huo nafasi nyingine zilipigiwa kura ni Mwenyekiti wa Madiwani wa CCM katika manispaa hiyo na kupatikana Omar Mwalimu Juma , aliepata kura 13 na nafasi ya Katibu wa Kamati ya Madiwani iliyochukuliwa na Makame Khamis aliepata kura 27.

Mapema Akifungua Mkutano huo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai aliwataka Madiwani hao kuwachagua viongozi makini na wenye sifa za kujituma  kiutendaji.

“ Endelelezeni utamaduni wa Chama Chetu katika kufanya uchaguzi huru na wa haki ili kupata viongozi watakaoweza kusimamia shughuli za manispaa yetu kwa ufanisi.

Pia epukeni makundi na badala yake kuweni wamoja katika kufanya kazi za maendeleo ili wananchi waweze kunufaika na uwepo wenu katika Manispaa ya Mjini.”, aliwasihi Vuai na kuongeza kuwa Manispaa ya Mjini ndiyo kioo cha Mjini wa Zanzibar hivyo lazima pafanyike kazi ya ziada kuhakikisha panakuwa safi na kung’ara muda wote kama ilivyo Miji mingine Duniani.

Naibu Katibu Mkuu huyo aliwasisitiza Madiwani hao kuwa Chachu ya kuleta maendeleo katika Wadi zao na kubuni miradi inayoendana na matakwa halisi ya wananchi ili kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho kwa vitendo.

Akizungumza na Gazeti hili mara baada ya Uchaguzi huo Meya Mteule wa Manispaa hiyo Khatib Abdulrahman Khatib aliwashukru Madiwani hao kwa kumuamini na kumpitisha tena ili aweze kuendelea kuongoza Manispaa hiyo kwa awamu ya pili.

Aliahidi kuendeleza mikakati ya kimaendeleo ndani ya Manispaa hiyo ikiwemo kushirikiana na viongozi wengine na wananchi kwa ujumla kuhakikisha Manispaa hiyo inakuwa na hadhi inayoendana na historia ya Zanzibar kimataifa.

Aliwakumbusha wananchi kudumisha usafi na utunzaji wa miundombinu mbali mbali iliyomo katika Manispaa hiyo ili kuepuka kuingia katika mikono ya kisheria.

0 comments:

Post a Comment

Mdau, Uwanja huu ni wako, Toa maoni yako yasaidie kujua wewe unafikiri nini kifanyike kuboresha zaidi maisha ya Watanzania. Maoni yako yasilenge kuchochea mtafaruku katika jamii, kisiasa, kidini, kikabila au kijinsia. Mawasiliano yetu:- simu +255 (0) 712 498008, Email: nkoromo@gmail.com.
Bashir Nkoromo
Msimamizi Mkuu, Blog ya Taifa ya CCM.