Saturday, December 31, 2016

EWURA YAIDHINISHA 8.5 % YA ONGEZEKO LA BEI YA UMEME

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeidhinisha asilimia 8.5 ya ongezeko la bei ya huduma za umeme ili kukidhi gharama za uzalishaji wa umeme.


Ongezeko hilo limetangazwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Felix Ngamlagosi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maombi ya kurekebisha bei za umeme ambapo marekebisho hayo yanatarajiwa kuanza kutekelezwa kuanzia Januari Mosi mwaka 2017.

Ngamlagosi amesema kuwa TANESCO iliomba kuidhinishiwa ongezeko la bei ya huduma hizo ili kuliwezesha shirika hilo kupata fedha za kulipia gharama za uendeshaji, kupata fedha za uwekezaji katika miundombinu pamoja na kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia asilimia 75 ya wananchi wote ifikapo mwaka 2025.

”Baada ya TANESCO kuwasilisha taarifa zinazohitajika kwa ajili ya kukamilisha maombi yao, EWURA ilifanya mikutano ya taftishi, matangazo kwa umma pamoja na kushirikisha wadau mbalimbali kutoa maoni juu ya ongezeko hilo ambapo baada ya uchambuzi wa maoni hayo tulilidhia kuongeza asilimia 8.5 tu ya ongezeko la bei hizo ,” alisema Ngamlagosi.

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) ambalo linanunua umeme wa jumla kupeleka Zanzibar limeongezewa asilimia 5.7 ya bei ya umeme badala ya asilimia 19.1 iliyoombwa na TANESCO.

Amefafanua kuwa kulingana na marekebisho yaliyofanyika, jumla ya mapato yanayohitajika kwa mwaka 2017 ni shilingi bilioni 1,608.47 ambayo ndiyo iliyopelekea ongezeko la bei la wastani wa asilimia 8.5 hivyo gharama za umeme zimeongezeka kutoka shilingi 242.34 kwa uniti moja hadi shilingi  263.02 kwa uniti moja.

Aidha, Mkurugenzi huyo ametoa maagizo kwa TANESCO yakiwemo ya kuanzisha tozo ya mwezi ya shilingi 5,520 kwa wateja wa kundi linalohusisha viwanda vidogo, mabango na minara ya mawasiliano, kuboresha huduma kwa wateja pamoja na kuacha kuwaunganisha wateja wadogo kwenye kundi la wateja wakubwa na badala yake kuwaonganishe moja kwa moja katika kundi la wateja wadogo.

Amewataka wananchi kuelewa kuwa kundi linalojumuisha wateja wa majumbani ambao matumizi yao ya umeme hayazidi uniti 75 kwa mwezi hawataathirika na ongezeko hilo la bei.
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.