LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 6, 2016

DAR YASHIKA NAFASI YA SITA KWA MAAMBUKIZI YA UKIMWI BARANI AFRIKA

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mbali na jitihada za makusudi za Serikali na wadau wa mapambano dhidi ya UKIMWI nchini bado hali siyo ya kuridhisha ambapo Jiji la Dar es Salaam linashika nafasi ya Sita barani Afrika kwa maambukizi ya ugonjwa huo.
Dar es Salaam ambalo ni Jiji kubwa kuliko yote Tanzania linakadiriwa kuwa na watu 210,000 wanaoishi na virusi vya UKIMWI ambapo kati yao asilimia 58 ni wanawake, na kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 idadi ya wakazi wa jiji hilo inakadiriwa kuwa Milioni 5.
 Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya UKIMWI duniani kutoka Shirika la Mpango wa UKIMWI la Umoja wa Mataifa - Tanzania (UNAIDS) kwa mwaka 2015, Jiji la Dar es Salaam limekuwa kati ya majiji Barani Afrika yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya UKIMWI.
Afisa wa UNAIDS Tanzania, Fredrick Macha anasema asilimia 16 ya maambukizi yote mapya Tanzania Bara yanatokea katika jiji la Dar es Salaam ambapo kwa wanawake wenye umri mdogo wa miaka 15-24 kiwango cha maambukizi kimefikia asilimia 7%,sababu kubwa ikiwa ni kujiingiza katika ngono wakiwa na umri mdogo pamoja na biashara ya ukahaba.
Anafafanua kuwa maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto Jijini Dar es Salaam ni asilimia sita (6%) licha ya jitihada kubwa za Serikali na wadau mbalimbali wa mapambano dhidi ya UKIMWI,kuelimisha na kuhamasisha wajawazito kupima na kufuata ushauri wa kitaalamu wa jinsi ya kujikinga na VVU.
Takwimu za Wizara ya afya za mwaka (2011-2012), mtu mmoja kati ya watu watano jijini Dar es Salaamana mahusiano ya kimapenzi na zaidi ya mtu mmoja,na mara nyingi wanafanya ngono zisizo salama hivyo hicho ni kiashiria kikubwa cha ongezeko la maambukizi hasa kwa wana ndoa”alisema Macha.
Aidha amevitaja baadhi ya vichocheo na viashiria vinavyochangia uwepo wa ongezeko kubwa la maambukizi katika jiji hilo kuwa ni ukuaji wa kasi wa shughuli za kiuchumi na kibiashara unaosababisha muingiliano wa watu kutoka Mikoa mbali mbali nchini pamoja na mataifa mengine.
Dar es Salaam kama yalivyo majiji mengine duniani yenye muingiliano wa tamaduni na desturi mbalimbali limeathirika pia na makundi yanayoelezwa kuchochea maambukizi mapya ya UKIMWI kama vile wafanya biashara ya ngono, wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja na watumiaji wa madawa ya kulevya na kwa kujidunga.                                                                                 
“Kwa mujibu wa takwimu hizo, kati ya wanawake 4 wanaojihusisha na biashara ya ngono, mmoja ni mwaathirika na virusi vya UKIMWI (sawa na asilimia 26).Vile vile kati ya watu watano wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, mtu mmoja ameathirika, sawa na asilimia 22.3) na kati ya watu sita wanaotumia madawa ya kulevya kwa njia ya kujidunga sindano, mmoja ni mwathirika wa virusi vya UKIMWI (sawa na asilimia 15.5),”alisema Macha.
Aidha Macha alisema pamoja na changamoto mbalimbali, Jiji la Dar es Salaam limependekezwa kuwa moja ya majiji machache ya mfano ulimwenguni katika mkakati wa dunia wa kuimarisha udhibiti wa UKIMWI kwenye majiji (UNAIDS Fast Track Cities Initiative).
Mkakati huo ni kuyafanya majiji makubwa Afrika kuwajibika zaidi katika kuongeza ufanisi kwenye mapambano dhidi ya UKIMWI katika maeneo ya mijini kwani kasi ya maambukizi na wingi wa maambukizi yapo mijini.
Pamoja na majiji kuwa na rasilimali nyingi, mifumo ya utoaji huduma za afya bado inaandamwa na changamoto mbalimbali, hususani katika kuandaa na kutekeleza mipango mizuri yenye kuhakikisha ushirikishwaji wa watu wote hasa makundi maalumu katika jamii, ambayo kiwango cha maambukizi ni kikubwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye ulemavu, Jenista Mhagama anasema takwimu zilizopo sasa zinaonyesha kuwa asilimia 6.2 ya wanawake  nchini wameambukizwa ugonjwa wa ukimwi ikilinganisha na asilimia 3.8 ya wanaume,jambo ambalo linahitaji jitihada zaidi kujikinga.
  
“Kwa mujibu wa Utafiti wa Viashiria vya Virusi vya UKIMWI (VVU) na Maralia (THMIS) wa mwaka 2011/2012 kwa upande wa Tanzania Bara vinaonyesha kuwa idadi kubwa ya wanawake wameambukizwa ugonjwa huo kuliko wanaume.
  
Waziri Mhagama anasema kuwa kutokana na utafiti huo, maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa upande wa Tanzania Bara ni asilimia 5.3 na inakadiriwa  kuwa  jumla ya watanzania 1,538,382 wanaishi na VVU ambapo vijana wenye umri kati ya 15-24 ni asilimia 10.6 na watoto walio chini ya miaka 15 ni 11.8.

 Aliongeza kuwa UKIMWI bado ni janga kubwa nchini Tanzania kwani takwimu zinaonyesha kuwa  maambukizi mapya yanakadiriwa kufikia watu 48,000 kwa mwaka hali ambayo  inaashiria kupoteza  nguvu kazi kubwa katika nchi yetu hivyo Tanzania itendelea kushirikiana na nchi nyingine Duniani,pamoja na mashirika ya kupambana na UKIMWI kuhakikisha janga hilo linatokomezwa  ifikapo mwaka 2030.

Alisema Serikali inaendelea kuwahamisha wananchi waendelee kujitokeza kupima afya zao kwa hiari ili wajitambue na kujua namna ya kujilinda kwani Shirika la Afya Duniani (WHO) linasisitiza nchi wanachama kuwaanzishia dawa mara moja watu wote watakaopima na kugundulika kuwa na VVU,bila kusubiri hadi kinga zao zipungue.

 Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dr. Leonard Maboko alisema kuwa kwa mwaka 2015 walioambukizwa VVU walikuwa Watanzania 2,100,000 ambayo ni idadi kubwa ukilinganisha na idadi ya sasa lakini  pamoja na kushuka kwa idadi hiyo wananchi wanatakiwa kuendelea kujilinda mara dufu.

”Ingawa maambukizi ya VVU yameshuka kutoka Watanzania 2,100,000 hadi 1,538,382, Watanzania hatutakiwi kubweteka bali tunatakiwa tufanye jitihada za pamoja kuhakikisha janga hili linafikia mwisho,”alisema Dr. Maboko.
  
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu alisema wataalam wa afya wametuambia UKIMWI unapungua nchini Tanzania, suala hilo linatokana na misaada mbalimbali tunayoipata kutoka nchi wahisani  kwahiyo ili kutokomeza kabisa suala la upungufu wa dawa na misaada kwa waathirika wa ugonjwa huo Watanzania wanahitaji kujichangia wenyewe na sio kutegemea fedha za wahisani peke yake.
 Alifafanua kuwa ili kuwezesha suala hilo,Sheria Na. 5 ya mwaka 2015 imeitaka Wizara yenye dhamana kuwa na Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI pamoja na Bodi yake hivyo, kuanzishwa kwa Mfuko huo kutaleta chachu kwa Watanzania kuungana kuzuia maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI (VVU) pamoja na kuwahudumia wananchi wanaoishi na virusi hivyo.
 “Kwa kawaida fedha zinazotoka kwa wahisani huwa zina mwisho wake hivyo Tanzania tunazindua Bodi rasmi itakayosimamia Mfuko huo ili na sisi tuongeze nguvu pale wahisani watakapoishia,”alisema Mama Samia.
 Naye muathirika wa UKIMWI, (jina limehifadhiwa) ameishkuru Serikali kwa kuwasaidia kwa hali na mali watu wenye ugonjwa huo kwani sio wote wenye ugonjwa huo wameupata kwa kujitakia.
 “Kitendo hiki kinatufanya tusijione wanyonge wala kukata tamaa kwani Serikali yetu haitutengi inatupa ushirikiano sawa na watu wengine wasio na maambukizi ya ugonjwa huu,”alisema muathirika huyo.
 Tarehe 1 Disemba kila mwaka ni siku maalumu ambayo tunaadhimisha Siku ya UKIMWI duniani, siku ambayo kwa pamoja tunaungana na watu wote wanaokadiriwa kufikia milioni 78 ambao tayari wameshapata mambukizi na watu milioni 35 ambao tayari wamefariki ulimwenguni kote kutokana na athari zitokanazo na maambukizi ya UKIMWI.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages