LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Nov 1, 2016

TANZANIA: NI MUHIMU ICC NA AFRIKA KUZUNGUMZA

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,Balozi Tuvako Manongi  akizungumza  wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  lilipopokea na kujadili Ripoti ya  Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ( ICC)  jana, jumatatu.  
Na Mwandishi Maalum, New York
 Jamhuri ya Muugano wa Tanzania  imeishauri Mahakama ya Kimataifa ya  Makosa ya Jinai ( ICC) kukaa meza moja   na  nchi  wanachama wa  Mkataba wa Roma     hususani  zile za  Afrika  ili kutafuta    suluhu ya  changamoto  na tofauti  zilizopo kati ya  mahakama hiyo  na wanachama wake.

Tanzania  imetoa mwito huo siku ya  jumatatu kupitia  Mwakilishi wake wa Kudumu   wa  Tanzania katika  Umoja wa Mataifa,  Balozi Tuvako Manongi,  wakati  Baraza  Kuu la Umoja wa Mataifa,  lilipopokea na kujadili Taarifa ya  Utendaji ya  Mahakama ya Kimataifa  ya  Makosa ya Jinai.

 Taarifa   ICC  imewasilishwa na  Rais   wa mahakama hiyo  Jaji Slivia Fernandez de  Gumendi  katika  kupindi  ambacho  Jumuiya ya Kimataifa  imekumbwa  na taharuki baada ya  wanachama  wawili  wa Mkataba wa Roma, Afrika ya Kusini na  Burundi kuwasilisha rasmi     katika Umoja wa Mataifa  kusudio la kujiondoa    huku  Gambia nayo ikitangaza kutaka kujitoa ingawa   bado haijawasilisha rasmi  nia yake hiyo. 

Mwakilishi  huyo wa Tanzania katika  mchango wake amesema,   uwepo au kuanzishwa kwa ICC kulitokana kwa kiasi kikubwa na uungwaji  mkono  kutoka Afrika.

Akasema  uungwaji  mkono huo  ulitokana hasa baada ya  nchi  hizo za Afrika kukatishwa  tamaa na kuvunjika   moyo baada ya   kutokea  kwa mauaji ya kimbari nchini  Rwanda.

“Baada ya  kukatishwa tamaa na kuvunjwa moyo,  Mahakama   hii, ilikuja  kuwa chombo cha kutenda haki dhidi ya watu  waliojihusisha na  vitendo vya kikatili vikiwamo  vya  ukatili  dhidi ya  binadamu, uhalifu  kivita na  ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Madhira yasiyoelezeka yaliyotokea Barani Afrika   yakaifanya  mahakama hii kuwa  chombo cha matumaini dhidi ya wale ambao  hawakuweza kuguswa  au  walikuwa  juu ya sheria”. Akasema  Balozi Manongi

Na kuongeza. “  Kama nchi mwanachama wa Mkataba  wa Roma wa Mahakama ya Kimataifa  ya Makosa  ya Jinai na Mwanachama wa Umoja wa Afrika. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua  kwamba,  uhusiano  kati ya mahakama   na Afrika  ni ule wa  misuguano, na ni uhusiano  ambao  umeleta hofu ya   Afrika kujitoa”.

Balozi Tuvako Manongi  akaeleza zaidi kwamba, hofu hiyo ya kujitoa kwa Afrika katika  mahakama hiyo, haipaswi kuwepo kutokana na  mambo  kadhaa ambayo  Afrika imejipanga  kuyatekeleza kwa manufaa ya   bara hilo na  watu wake.

 Baadhi ya  mipango hiyo  ni utekelezaji wa ajenda  ya Maendeleo  ya Umoja wa Afrika  maarufu kama agenda 2063 ambayo pamoja na mambo mengine inachagiza katika  utawala  bora,  demokrasia,  usawa wa jinsia,  kuheshimu haki za binadamu,  haki na utawala wa sheria..

“Viongozi wa  wakuu wa nchi na serikali wa  Afrika wameutangaza  mwaka 2016 kuwa   mwaka wa haki za binadamu   huku mkazo ukielekezwa katika haki za wanawake. Na katika kutambua kuwa Amani na  Haki ni vitu ambavyo haviwezi  kutenganishwa, kwa sababu hizo,  tunachotakiwa  kuhimiza leo sana sana ni  majadiliano”.Akasisitiza Balozi.

Tanzania   pia  ikaeleza kwamba ni  vema Mahakama hiyo katika utekelezaji wa majukumu yake  ikajenga mazingira ya kuaminiana kati  yake na wanawachama wake.

Tanzania pia kupitia  Mwakilishi wake, imezitaka nchi hususani zile za mataifa yaliyoendelea  kuacha  kuzihubiria nchi zinazondelea kama vile zenyewe ni  adilifu sana. Na kusisitiza kwamba, kinachotakiwa  wakati  huu  si kunyosheana vidole au kulaumiana bali  kufanya kazi  kwa  pamoja  ili  kuifanya mahakama hiyo iendelee kutekeleza majukumu yake kwa  uwazi ,  haki na kuaminiwa.

Akasisitiza pia kuwa hata kama matatizo yaliyopo  baina ya  ICC na Africa yatapatiwa ufumbuzi. Bado kuna  haja na umuhimu kwa nchi za  Afrika  kuziimarisha na   kuzijengea uwezo  Taasisi zake  na vyombo  vinavosimamia  utoaji wa haki na utawala wa sheria ili  viweze kushughulikia  makosa ya jinai yakiwamo  ya ukatili dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita badala ya  kusubiri   au kutegemea  mahakama za kimataifa kama ICC.

Akabinisha    kuwa     nchi zinatakiwa  kuwajibika kikamilifu   siyo kwa  kuhofia  kuingiliwa mambo yao ya ndani na ICC bali kwa sababu zinaowajibu  wa kwanza wa kuwalinda  raia wao.

“Kwa Afrika matukio kama yale ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Cote d’ Ivore, Rwanda na Sierra-Leone ni    kielelezo cha  hatari  ambayo tunatakiwa kujikinga nayo.

Vile vile Tanzania   imelitaka  Baraza la  Usalama la Umoja wa Mataifa,  kutopeleka ICC rufaa zenye  malengo wa kisiasa  kwani kwa kufanya hivyo kunachangia kuharibu sifa ya ICC na kuifanya isiaminiwe na kuonekana inatumiwa na  wakubwa kutimiza malengo yao.

Pamoja na  kulitaka   Baraza la Usalama kutoingiza siasa katika  rufaa zake,  Tanzania pia imewashangaa baadhi ya wajumbe wa Baraza hilo na ambao si wanachama wa Mkataba wa Roma kuwa mstari wa mbele  katika kupeleka rufaa kwenye  Mahakama hiyo dhidi ya  mataifa mengine.

Wazungumzaji wote zaidi ya 50 walioomba kuchangia  Taarifa hiyo ya ICC pamoja na kuzungumzia utendaji  kazi na changamoto zinazoikabili  Mahakama hiyo, walijielekeza zaidi  katika  kuelezea masikitiko yao  juu ya uamuzi wa Afrika ya Kusini na Burundi  kujitoa.

Wasemaji  hao  kama ilivyokuwa kwa Tanzania walisisitiza sana   umuhimu wapande zinazopingana kukaa  mezani na kuzungumza  huku baadhi yao   wakizitaka  Afrika ya Kusini na Burundi  kufikiria upya uamuzi huo.  


No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages