Wednesday, November 16, 2016

KIMETA CHAUA NYUMBU 90 MONDULI

Image result for MNYAMA NYUMBU 
Na Woinde Shizza,Arusha
Zaidi ya nyumbu 90 na swala 15 wamekufa katika eneo la mapito ya wanyamapori, lililopo kwenye kata ya Selela wilayani Monduli mkoani Arusha.

Inadaiwa kuwa wanyama hao wameangamia kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kimeta ulioibuka katika ushoroba huo wa Selela, unaoziunganisha mbuga za Tarangire na Hifadhi ya Ziwa Manyara, pia umeangamiza idadi kubwa ya wanyama wa kufugwa hasa ng'ombe, mbuzi na kondoo wapatao 60, huku idadi ya vifo ikitarajiwa kuongezeka.

Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Idd Kimanta amesema baada ya matukio ya wanyamapori kuanguka ghafla na kufa kwa wingi na baadaye mifugo pia kuanza kuangamia, uongozi wa wilaya ulipeleka sampuli za mizoga hiyo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi na ambaye alithibitisha uwepo wa kimeta.

“Tunahofia kuwa kimeta sasa kitakuwa kimesambaa maana wanyama kama nyumbu wana tabia ya kuhamahama kutoka sehemu moja hadi nyingine, hivyo si ajabu wamepeleka ugonjwa huu maeneo mengine," alisema.
Ofisa Mifugo wilayani Monduli, Salum Omar amethibitisha kufa kwa ng'ombe, mbuzi na kondoo kadhaa katika eneo lake na kuongeza kuwa hivi sasa wameanza taratibu za kutoa chanjo dhidi ya maambukizi ya kimeta kwa mifugo iliyobaki.

“Lakini kuna haja pia ya kuhakikisha kuwa wafugaji, wengi wakiwa ni wa jamii za Kimasai, wanapewa elimu juu ya mlipuko wa ugonjwa huu, maana wengi wanakula mizoga ya mifugo yao iliyokufa,” alionya ofisa mifugo huyo. 

Kwa kawaida binadamu akigusa mzoga wa mnyama aliyekufa kwa kimeta, huweza kupata maambukizo hayo. Sasa wafugaji wa Monduli wanakwenda mbali zaidi, kula nyama iliyoathirika.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Selela, Julius Loiboseki ameomba msaada kwa serikali iwasaidie kuzuia mifugo kutoka maeneo ya jirani ili isiingizwe kwenye maeneo yao hadi pale tatizo litakapotatuliwa.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Diwani wa Kata hiyo ya Selela, Cuthbert Meela ambaye alifafanua kuwa wilaya ya Monduli haijawahi kukumbwa na mlipuko wa kimeta au ugonjwa wowote ule mkubwa wa kutishia maisha ya watu na wanyama.
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.