LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 5, 2016

TANZANIA YATAKA DUNIA IWEKEZE KWENYE MAENDELEO BADALA YA ULIMBIKIZAJI WA SILAHA

Mwakilishi wa Tazania Kudumu UN
Tuvaco Manongi akizungumza
katika kikao hicho
Na Mwandishi  Maalum, New York
Tanzania  imeitaka  Jumuiya ya Kimataifa  kupunguza   matumizi makubwa  katika kujilimbikizia silaha zikiwamo za maangamizi na badala  yake fedha hizo zielekezwe katika kusaidia  utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ( agenda 2030).

Wito  huo umetolewa  siku ya jumanne na  Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, wakati Kamati ya Kwanza  ya  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  inayohusika  pamoja na mambo mengine, usalama wa kimataifa  likiwamo  suala ya  upokonyaji wa silaha ilipokuwa ikijadilia ajenda ya  upokonyaji  silaha.

 “ Kila Septemba   26 ya kila mwaka,  tunaadhimisha siku ya kimataifa ya kumaliza kabisa silaha za nyukilia. Lakini  wakati Kamati hii  ikianza mijadala yake hakuna  hatua yoyote ya maana iliyochukuliwa ya  kulimaliza tatizo hili” akasema  Balozi Manongi na kuongeza,   badala yake  dunia inashuhudia   nchi ambazo zinazomiliki silaha za nyukilia zikiendelea na kasi ya  kuziongeza ikiwa ni pamoja na  kuwekeza mabilioni  ya dola katika kuzifanyia  marekebisho na  kuziimarisha.

“Kwa Tanzania, upokonyaiji wa  silaha na  maendeleo ni mambo yanayohusiana. Kiasi cha fedha ambacho kinaelekezwa katika matumizi ya  kijeshi yangeweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa  malengo  ya maendeleo endelevu. Ni kwa sababu hiyo tunaona  umuhimu wa kazi za  Kamati hii”.Amesisitiza  Balozi.

Akizungumzia   nafasi ya Umoja wa Mataifa katika  kusimamia suala na  upokonyaji wa silaha kupitia   Taasisi zake, Balozi   amesema licha ya  ugumu na changamoto  katika  eneo  hilo. Tanzania bado inamatumaini ya  Umoja wa Mataifa   kama chombo muhimu  kinachoweza kudhibiti usambaaji wa  silaha za maangamizi  zikiwamo silaha ndogo ndogo, za kati na nyepesi.

Pamoja na  kuelezea namna   Nchi zenye silaha za maangamizi zinavyoendelea kujilibikizia silaha hizo ikiwani  ni  pamoja na kuziimarisha ili ziwe za kisasa.  Balozi pia ametumia fursa hiyo  kutahadharisha  dhidi ya  hasara za kibinadamu zinazoweza kutokea dhidi ya  matumzi ya silaha hizo.

Na kwa sababu hiyo, Tanzania imezisihi  nchi  zinazomiliki  silaha za nyukilia  kutumiza wajibu wao  kisheria ikiwa ni pamoja na  kuchukua hatua za  kuangamiza silaha hizo kwa uwazi na bila  kuchelewa na  kwa kuzingatia makubaliano ya  Mkataba wa Kimataifa wa  upokonyaji wa  silaha.

Tanzania pia imekumbushia  haja na umuhimu wa nchi ambazo hazina silaha  za nyukilia  kutonyimwa fursa ya kutumia  teknolojia  ya nyukilia  kwa shughuli  salama  zikiwamo za    utafiti na shughuli nyingine za  maendeleo na ustawi wa nchi zao.

Kuhusu  Ukanda Huru  zisizokuwa na silaha za nyukilia,  Tanzania  ambayo  ni nchi mwanachama wa   Mkataba wa  Palendaba   (Africa Nuclear Free Zone)  inaunga mkono uwepo wa Kanda huru ambazo hazina silaha za nyukilia.

Katika  hatua nyingine ,  Tanzania imekaribisha  kuanzishwa kwa  Benki ya  Teknolojia kwa nchi   zilizonyuma kimaendeleo  ( Technology Bank for  Least Developing Countries).

Kuanzishwa  kwa bank hiyo  kunalenga pamoja  na mambo mengine kuzisaidia nchi za   LDC’s  kuwa na fursa  na uwezo wa kutumia  teknolojia sahihi kutoka kwa mataifa yaliyoendelea.

Hayo yameelezwa na  Bw. Songalieli Shilla,  Afisa Mkuu  Mambo ya Nje  katika Uwakilishi wa kudumu wa Tanzania  wakati  alipochangia kwa niaba ya Tanzania majadiliano ya Kamati ya Pili ya  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ilipokuwa  ikijadili masuala mtambuka yakiwamo ya ukuaji wa uchumi na maendeleo.

Tanzania  ikasisitiza kwamba    kuanzishwa kwa  Banki hiyo  kutazisaidia  nchi za  LDC’s kuingia katika ushindani  na mataifa yalioendelea.  Na kwamba   Tanzania inafarijika pia kwamba  Benki hiyo itaendelea kuzisaidia     hata zile  nchi ambazo zitakuwa  zimefunzu kutoka  nchi  zenye uchumi wa chini na kwenda kwenye uchumi wa kati.

Benki  hiyo ambayo chimbuko lake ni mkutano  uliofanyika mwaka 2011  nchini   Uturuki na ambayo tayari maandalizi ya awali  yamekwisha kufanyika inatarajiwa kuzinduliwa mwakani.

Kamati ya  Pili ya  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inahusima na masuala ya Uchumi na Fedha, na  katika mkutano  huo, pamoja na  kukaribisha uanzishwaji wa Benki hiyo, pia Tanzania imezungumzia changamoto mbalimbali ambazo zinakweza kukwamisha utekelezaji wa ajenda  ya maendeleo endelevu  hususani kwa nchi zinazoendelea.

Amezitaja baadhi ya changamoto hizo  kuwa ni  pamoja na   mabadiliko ya tabia nchi,  upatikanaji wa  raslimali  fedha  kutoka vyanzo vya ndani na kutoka kwa wadau  na washirika wa maendeleo. 

 Baada ya kukamilika kwa   Mkutano na Majadiliano ya jumla  ya  Baraza Kuu la  71 la Umoja wa Mataifa,     mkutano uliowakutanisha  viongozi wakuu wa  Nchi na  Serikali  kutoka mataifa mbalimbali duniani.  Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa,   kupitia  Kamati Sita zinazounda  Baraza  Kuu la   Umoja wa Mataifa,  zimeingia katika ngwe nyingine muhimu ambapo sasa  wajumbe  wanakutana  kupitia Kamati hizo  kujadiliana agenda na maazimio  mbalimbali    kuanzia yale yanayohusu uchumi,  fedha na maendeleo, haki za binadamu,  ustawi  wa jamii, Amani   na  usalama,  umalizwaji wa ukoloni,   utawala wa  sheria ,  sheria  za kimataifa  na bajeti na utawala.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages