LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 7, 2016

RAIS DK MAGUFULI AWATAKA MABALOZI WANAIWAKILISHA TANZANIA NJE ZA NJE KUJIKITA KATIKA DIPLOMASIA YA UCHUMI

Rais Dk Magufuli
Dar es salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 07 Oktoba, 2016 amekutana na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani ambapo pamoja na mambo mengine ametaka utekelezaji wa diplomasia ya uchumi utiliwe mkazo katika uwekezaji kwenye sekta ya viwanda.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam, imesema, katika Mkutano huo uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Rais Magufuli aliyehutubia na kuongoza majadiliano juu ya masuala mbalimbali ya shughuli za mabalozi, amesema Tanzania imeweka dhamira ya kuikuza sekta ya viwanda kutoka ukuaji wa asilimia 7.3 hadi kufikia asilimia 15 ifikapo mwaka 2021 na kuzalisha ajira kwa asilimia 40.

"Sasa nimeona niwaite waheshimiwa Mabalozi ili tuelewane, mjue mwelekeo tunaoutaka na mjue ni namna gani mtakavyoshiriki kuhamasisha uwekezaji wa viwanda.

"Nataka badala ya kubaki mmejifungia ofisini, mtoke mwende mkawatafute wawekezaji waje wawekeze katika viwanda ili nchi yetu inufaike kwa watu wetu kupata ajira, Serikali kukusanya kodi na tuinue maendeleo yetu" Taarifa hiyo imemnukuu Rais Magufuli.

Imesema, maeneo mengine ambayo Rais Magufuli ametaka Mabalozi wayafanyie kazi ni kutangaza na kuwavutia watalii kuja hapa nchini, kufanyia kazi fursa zote zenye manufaa kwa Tanzania katika nchi wanakowakilisha, kulinda mali za nchi zilizopo katika nchi hizo na kufuatilia utekelezaji wa mikataba ya biashara na uwekezaji inayofanywa kati ya Tanzania na nchi wanakowakilisha.

Pia Rais Magufuli amewataka waheshimiwa Mabalozi wote kufanya kazi kwa juhudi, kuondoa kasoro za utendaji kazi ambazo zimekuwa zikilalamikiwa katika ofisi zao na kubana matumizi ya fedha yasiyokuwa ya lazima.

Dkt. Magufuli ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kujipanga na kudhibiti mianya yote ya matumizi mabaya ya fedha za umma ambazo zimekuwa zikitumika katika safari za nje ya nchi na matumizi mengine yasiyo ya lazima, pamoja na kuhakikisha watumishi wote ambao wapo katika ofisi za ubalozi kwenye nchi mbalimbali bila sababu za msingi wanarejeshwa nchini ili kupunguza mzigo wa gharama kwa Serikali.

"Kuna wafanyakazi wapo kwenye Balozi zetu wakati hata sifa za kuwa katika nafasi wanazoshikilia hawana, ilifika mahali mtu akiharibu hapa nyumbani anapangiwa ubalozini.

"Wakati mwingine unakuta ubalozi wa Tanzania kwenye nchi fulani una idadi kubwa ya wafanyakazi kuliko mahitaji ya ubalozi huo, haiwezekani" amesisitiza Rais Magufuli.
Hata hivyo Dkt. Magufuli amewapongeza Mabalozi wote wa Tanzania kwa kazi wanazozifanya kwenye nchi wanazowakilisha na amewahakikishia kuwa Serikali ina matumaini nao na inawategemea kuwa wataendelea kuiwakilisha na kuitangaza vizuri Tanzania.

Mkutano huo pia umehuduriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, Viongozi wa Taasisi mbalimbali na Wakurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages