LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 13, 2016

RAIS DK MAGUFULI AOMBOLEZA KIFO CHA DK. MASABURI, ATUMA SALAM ZA RAMBIRAMBI

Dar es Salaam
Rais Dk. John Pombe Magufuli ameitumia salamu za rambirambi familia ya Meya wa zamani wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi, aliyefariki dunia jana, Oktoba 12, 2016, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa  leo na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam, imesema, Katika salamu hizo Rais Dk. Magufuli amesema amepokea taarifa ya kifo cha Dk. Didas Masaburi kwa mshituko na masikitiko makubwa na kwamba anaungana na familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki katika kipindi hiki kigumu cha huzuni ya kuondokewa na mpendwa wao.

"Poleni sana familia ya Dk. Didas Masaburi, najua huu ni wakati mgumu sana kwenu, lakini niwahakikishie kuwa sote tumeguswa sana na msiba huu kwa kuwa tumempoteza mtu muhimu, msomi mzuri, kiongozi aliyelitumikia Taifa la Tanzania kwa moyo wake wote na aliyesimamia kile alichokiamini" taatifa hiyo imemkariri akisema Rais Magufuli katika salamu hizo.

Taarifa imeongeza kuwa Dk. Magufuli amewapa pole wanachama na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao wamempoteza Mwana CCM mwenzao pamoja na Viongozi na watumishi wa Jiji la Dar es Salaam ambao walifanya nae kazi alipokuwa Meya wa Jiji.

Rais Dk. Magufuli katika salam hizo, amemuombea kwa Mwenyezi Mungu ampumzishe mahali pema peponi na kusema "Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. Amina." 

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages