Thursday, October 20, 2016

MKUU WA WILAYA YA MALINYI KUTUMIA POSHO ZA MWENGE ZILIZOOKOLEWA NA DK. MAGUFULI, KUJENGA MADARASA KWENYE SHULE YA JAMII WAFUGAJI

NA MWANDISHI WETU MALINYI
Mkuu wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro, Majura Kasika, ameagiza posho ya zaidi ya sh. milioni 2, zilizookolewa kwa agizo la Rais Dk. John Magufuli, kufuta mialiko ya safari za viongozi kwenda kwenye uzimaji Mwenge mkoani Simiyu, zitumike katika ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na matundu sita ya vyoo katika shule ya msingi Lumbanga wilayani humo.

Kasika alisema,  fedha hizo ni kiasi cha sh. 2,080,000, ambazo zilikuwa zitumike kwa ajili ya gharama ya posho ya safari za viongozi watatu na madereva wawili ambao wangeenda kwenye sherehe hizo za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, kilichofanyika mkoani Simiyu,  Mapema Mwezi huu.

Mkuu huyo wa wilaya aliahidi kutolewa fedha hizo, wakati akizungumza na wananchi wa kitongoji cha Lumbanga kijiji cha Misegese kata ya Malinyi, wilayani hapa,  wakati akiendesha uhamasishaji wa michango ya maendeleo kwa ajili ya kupata fedha za kuanza kufyatua matofali ya ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa na matundu ya vyoo.

Pamoja na ahadi ya Mkuu wa wilaya kutoa fedha hizo sh. 2,080,000, pia Mbunge wa jimbo la Malinyi, Dk. Haji Mponda naye ameahidi kutoa sh. 500,000 kupongeza na kuunga mkono jitihada na nguvu za wananchi ambao waliahidi kuchangia sh.30,000 kwa kila kaya.

 Kwa mujibu wa mbunge huyo, kaya zilizopo katika kijiji hicho 400, hivyo uchangiaji huo ukitekelezwa na kila Kaya zinatarajiwa kupatikana jumla sh. milioni 12, ambazo zikichanganywa na sh. 2,580,000 alizoahidi mkuu wa wilaya na sh. 500,000 za  mbunge, jumla zitapatikana sh. milioni 15.08, zitakazoingizwa katika mradi huo.

Shule ya Lumbanga ni moja ya shule zilizoanzishwa kwa jitihada za Wazazi wa watoto wa jamii ya wafugaji ambao wamekuwa wakiishi mbali na shule zilizosajiliwa na hivyo kuanzisha vyumba viwili vya madarasa vilivyoezekwa kwa nyasi na  mabua ya zao la ufuta.

Licha ya kuwa na mazingira duni, lakini shule hiyo yenye wanafunzi wapatao 250  kwa miaka miliwili mfululizo imekuwa ikitoa wanafunzi bora wa darasa la nne wilayani Malinyi.

 Pamoja na michango ya wazazi,  Mkuu wa wilaya amewataka wananchi kufyatua matofali ya ziada ili kupata ya kuanzisha ujenzi wa nyumba ya mwalimu hapo baadaye na kumwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Malinyi,  Marcelin Ndimbwa kuipatia shule hiyo ruzuku ya maendeleo itokanayo na fedha za makusanyo ya ndani, pindi watakapokuwa wamefika hatua ya kuezeka na umaliziaji. 

Alisema, shule hiyo ni mojawapo ya shule za wafugaji ambazo amedhamiria kuzikamilisha na kuzitafutia usajili. Shule zingine ni Mipapa na Likea ambazo zinaendeshwa kwa kutumia walimu wanaojitolea.
Mkuu wa wilaya ya Malinyi Majura Kasika, akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi na baadhi ya walimu wa shul ya msingi Lumbaga kijiji cha Misegese wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro alipotembelea shule hiyo hivi karibuni
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.