LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 29, 2016

WAZIRI MKUU:WATUMISHI WALIOHAMISHIWA KIBITI NDANI YA MWEZI MMOJA WAWE WAMESHARIPOTI

WAZRI MKUU KASSIM MAJALIWA
Na Nassir Bakari

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka  watumishi waliohamishiwa wilaya mpya ya Kibiti mkoani Pwani kuripoti katika kituo chao cha kazi ndani ya mwezi mmoja kutoka sasa na watakaoshindwa kutekeleza watakuwa wamejifukuzisha kazi. 
 
"Tayari nimemuagiza ndugu Zuberi Samatabu Katibu Tawala wa mkoa wa Pwani kuhakikisha anasimamia watumishi wote wa wilaya hiyo wanaoishi nje ya wilaya hiyo waishi Kibiti na si Ikwiriri," amesema Waziri Mkuu. 
 
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo baada ya  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo Alvera Ndabagoye kumueleza  Waziri Mkuu kuwa ni watumishi wanane pekee kati ya 74 waliopangiwa kufanya kazi kwenye wilaya hiyo wameripoti katika kituo cha kazi 
 
Pia Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo kuzungumza na watendaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii kwenda wilayani huko kuwekeza katika miradi ya ujenzi wa nyumba za watumishi. 
 
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana Jumatano, Septemba 28, 2016 wakati akizungumza na watumishi wa wilaya hiyo katika ziara yake ya kukagua shughuli za maendeleo,utendaji wa serikali na kutoa msimamo wa serikali kuhusu utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku 
 
Wakati huo huo Waziri Mkuu amewataka madiwani wa halmashauri hiyo wawe wakali katika kusimamia miradi ya maendeleo na kuacha tabia ya kuomba omba kwa wakuu wa idara ili kuepuka kujishushia hadhi zao na kupelekea kuhujumiwa kwa miradi mbalimbali ya jamii 

Aidha aliwataka viongozi wa wilaya hiyo kutengeneza mazingira ya kukaribisha wawekezaji na wahakikishe kwamba uwekezaji utakaofanyika hausababishi migogoro ya ardhi kwa wananchi. 
 
Pia Waziri Mkuu amewahamasisha wananchi kuhakikisha wanapeleka watoto shule kwa maana Serikali imebeba mzigo wote wa gharama za ada na uendeshaji wa shule hizo. 
 

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages