Saturday, September 17, 2016

RAIS MUSENI, UHURU KENYATTA WAICHANGIA TANZANIA MSAADA JANGA LA TETEMEKO LA ARDHI LA BUKOBA

RAIS YOWERI MUSEVENI
DAR ES SALAAM
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 17 Septemba, 2016 amepokea taarifa ya maafa yaliyosababishwa na tetemoko la ardhi lililotokea katika Mkoa wa Kagera na mikoa jirani ya Mwanza, Geita na Mara kutoka kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Pamoja na kupokea taarifa hiyo Rais Magufuli amepokea mchango wa fedha taslimu kiasi cha Dola za Kimarekani laki mbili (USD-200,000/-) sawa na takribani Shilingi za Kitanzania Milioni Mia nne na therathini na saba (Tshs-437,000,000/-) kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni na pia amepokea taarifa ya mchango wa mabati, blanketi na magodoro vyenye thamani ya Shilingi za Kitanzania milioni 115 kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi Mkoani Kagera.

Katika taarifa yake Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema tetemeko hilo limesababisha vifo vya watu 17, majeruhi 440, nyumba 2063 zimeanguka, nyumba 14,081 zipo katika hali hatarishi na nyumba 9,471 zimepata uharibifu mdogo, huku watu 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.

"Mhe. Waziri Mkuu ameongeza kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali zikiwemo kupeleka chakula, huduma za matibabu na hifadhi za dharura kwa waathirika na pia inaratibu ukusanyaji wa michango kutoka sehemu mbalimbali ambapo mpaka sasa kiasi cha Shilingi za Kitanzania Bilioni tatu nukta sita (Tshs Bilioni 3.6) zimepatikana", imesema taarifa ya Ikulu.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya maafa na michango kwa ajili ya waathirika wa maafa hayo, Rais Magufuli amewashukuru wote waliojitoa kusaidia waathirika wakiwemo Marais Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, Mhe. Uhuru Kenyatta wa Kenya na Paul Kagame wa Rwanda ambao wamempigia simu za kumpa pole na tayari wametoa misaada yao, na pia nchi mbalimbali, mashirika, wafanyabiashara, watumishi wa umma na watu binafsi na amesema michango hiyo ina umuhimu mkubwa katika kukabiliana na athari za maafa haya.

Dkt. Magufuli ametoa wito kwa Watanzania na wote walioguswa na maafa haya kuendelea kutoa misaada kwa waathirika kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, huku akionya na kuvitaka vyombo vya dola kuwafuatilia watu wanaotaka kutumia maafa haya kukusanya michango kwa lengo la kujinufaisha.

Rais Magufuli amebainisha kuwa Serikali itahakikisha inarekebisha miundombinu iliyoharibika zikiwemo shule, vituo vya matibabu, barabara na huduma nyingine za kijamii na pia ametaka wananchi waliokumbwa na madhara ya tetemeko hususani nyumba zilizobomoka, wajipange kurekebisha nyumba zao kwa kuwa Serikali pekee yake haitaweza kujenga nyumba zote zilizobomoka.

Aidha, Rais Magufuli amewasihi Watanzania kuwapuuza watu wanaotaka kutumia maafa haya kueneza uchonganishi na chuki dhidi ya Serikali na ameweka wazi kuwa mpaka sasa hakuna teknolojia ya kutabiri kutokea kwa tetemeko la ardhi na kwamba tetemeko hili halikuletwa na Serikali.

Dkt. Magufuli amesema hata mataifa makubwa yenye maendeleo makubwa ya uchumi na teknolojia yanakumbwa na tetemeko la ardhi na kusababisha vifo vya idadi kubwa ya wananchi na uharibifu mkubwa wa mali.

"Nilikuwa najaribu kuangalia kwa mfano nchi kama China kwenye mwaka 2014 watu 617 walipoteza maisha, Mwaka 2013 walipoteza watu 193, Mwaka 2010 walipoteza watu 2,998 Mwaka 2008 China ilipoteza watu 98,712.

Ukijaribu kuangalia Japan, nchi ambayo imeendelea na ina utaalamu wa hali ya juu sana, kwenye mwaka 2016 tarehe 14 mwezi wa nne ilipoteza watu 6, baada ya siku mbili tarehe 16 mwezi wa nne 2016 tetemeko likatokea tena na likaua watu 35, mwaka 2012 likaua watu 3, mwaka 2011 likaua watu 15,904 mwaka 2008 likaua watu 12, mwaka 2007 likaua watu 11, mwaka 2004 likaua watu 40, mwaka 1923 liliua watu 142,800 na hiyo ni Japan.  Taarifa imesema ikimkariri Rais Magufuli.

Imesema, shughuli ya kupokea taarifa ya Waziri Mkuu na michango kwa ajili ya waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea Mkoani Kagera na Mikoa jirani imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Augustine Mahiga, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt Suzan Kolimba, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Balozi wa Uganda nchini Tanzania Mhe. Dorothy Hyuha na Naibu Balozi wa Kenya nchini Tanzania Mhe. Boniface Muhia.
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.