LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 20, 2016

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA KUANZA ZIARA YA KIKAZI LEO MJINI KATAVI

Na: Nasri Bakari 0713 311 300
Waziri mkuu wa serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa leo mchana anatarajiwa kuwasili mjini Mpanda kuanza ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Katavi,akiwa mkoani humo Waziri mkuu atafanya shughuli mbalimbali za kiserikali zikiambatana na kukagua na kutembelea baadhi ya miradi ya maendeleo na kuhutubia mikutano ya hadhara kwa wakazi wa mji huo na maeneo ya jirani.

Ikumbukwe kwamba ii itakuwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa juu wa kitaifa kutembelea mkoa wa Katavi tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani, ziara ambayo itamfikisha pia katika mkoa jirani wa Rukwa.

Akizungumza na vyombo Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Katavi, Lauteli Kanoni amesema ziara ya Waziri Mkuu mkoani humo itaanza leo na kutarajiwa kuhitimisha ziara yake Agosti 23, mwaka huu.

Kwa mujibu wa ratiba, Waziri Mkuu atawasili leo mchana kwenye Uwanja wa Ndege wa Mpanda kisha ataelekea Ikulu Ndogo ambako atasomewa taarifa ya mkoa na kuzungumza na watumishi wa serikali katika viwanja vya ikulu ndogo.

Siku itakayofuata atakwenda katika Kijiji cha Majalila, kunakojengwa Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda na kutembelea mradi wa maji kijijini humo kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara.

Kwa mujibu wa ratiba yake, anatarajiwa kuhutubia mikutano ya hadhara katika kijiji cha Ndui kilichopo kwenye makazi ya wakimbizi ya Katumba na katika uwanja wa Azimio, Manispaa ya Mpanda.

Aidha, Agosti 22, mwaka huu Waziri Mkuu atafanya ziara ya siku moja katika wilaya ya Mlele ambapo atawahutubia wananchi wa Inyonga katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlele kabla ya kuelekea katika Kijiji cha Majimoto, Halmashauri ya Mpimbwe atakapokagua ujenzi wa daraja la mto Kavuu na baadaye kuhutubia mkutano wa hadhara.
 Baada ya  kumaliza ziara yake ya kikazi Mh Waziri Mkuu anatarajiwa kufanya majumuisha ya ziara hiyo mnamo tarehe 23/8/2016,baada ya hapo anatarajiwa kwenda mkoani Rukwa katika wilaya ya Nkasi

Mungu ibariki Tanzania


No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages