Tuesday, August 23, 2016

UMOJA WA VIJANA WA CHAMA CHA MAPINDUZI(UVCCM) WAITISHA MAANDAMANO YA AMANI NCHI NZIMA AGOSTI 31


Na Nasri Bakari 0713311300
 
Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM)
kwa kushirikiana na wananchi wote wanaopenda amani nchini ,wanatarajia kufanya maandamano ya Amani nchi nzima siku ya Jumatano ,Agosti 31 kwa ajili ya kueleza utendaji kazi wa Rais Dk.John Pombe Magufuli kwa Watanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari jana,yalipo makao makuu ya UVCCM jijini Dar es Salaam,Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja huo, Shaka Hamdu Shaka amesema kuwa wameshamwandikia barua mkuu wa jeshi la Polisi kwa ajili ya kupata ulinzi siku hiyo.
 
"Kwa upande wetu makao makuu tumeshamwandikia Mkuu wa Jeshi la Polisi tokea Ijumaa 19 August 2016 barua Kumb.Na.VMM/U.40/28/Vol.II/159 na tumewaagiza Makatibu wote wa Wilaya na Mikoa ili kupata vibali vya kisheria,kupatiwa ulinzi hatimaye kufanikisha maandamano hayo" alisema .

Amesema kuwa wasipopata ulinzi watafanya kwa kujilinda wenyewe ikiwa ni lengo la kufikisha ujumbe kwa wananchi juu ya utendaji kazi wa Rais Dk. John Pombe Magufuli.
 
"Ikitokea polisi hawatakubali na kuyaruhusu maandamano hayo yafanyike katika Wilaya au Mikoa yao,UVCCM tutalazimika kuandamana kwa kujilinda wenyewe kwa mintarafu ya kuhakikisha tunafikisha ujumbe tunaokusudia ufike kwa Rais,Serikali na kwa jamii" aliendelea kusema.

Shaka amesema kuwa Rais Dk.John Pombe Magufuli amefanya watendaji kuwa na utii pamoja na maadili katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Aidha amesema kuwa katika maandamano hayo wanaawalika na vijana wa vyama vingine kushiriki kwa lengo moja tuu,la kuunga mkono utendaji wa Rais Dkt.John Pombe Magufuli.
 
"Vijana wote wa UVCCM na wananchi wapenzi wa Amani na utulivu nchini, wataruhusiwa kushiriki kwenye maandamano hayo na hawatazuiliwa kwa sababu aidha za kisiasa au kiitikadi ,kwa kuwa dhamira yetu ni kuwasilisha ujumbe wa pamoja wenye manufaa na tija endelevu kwa nchi yetu ,hatimaye tujiletee sisi wenyewe maendeleo ya kiuchumi,kisiasa,kijamii na kiutamaduni"alimaliza ndugu,Shaka Hamdu.
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.