Thursday, August 18, 2016

UFISADI MKUBWA WA FEDHA ZA ELIMU BURE WAGUNDULIKANa Nasri Bakari 0713 311 300
FEDHA zilizotengwa na Rais John Magufuli kwa ajili ya kugharimia elimu ya bure nchini, zimeanza kutafunwa baada ya kubaini kuwapo kwa udanganyifu unaofanywa na walimu wakuu kwa kuongeza idadi ya wanafunzi hewa ili kupata fedha zaidi.

Zoezi la kuhakiki wanafunzi limekuja baada ya Rais Magufuli aliwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote, kushughulikia udanganyifu unaofanywa na walimu wakuu wanaotafuna fedha kwa kuweka wanafunzi hewa katika suala la elimu bure baada ya serikali kuanza kutoa elimu bure Januari mwaka huu, ikitenga Sh bilioni 18.7 kila mwezi.

Kutokana na hali hiyo, Mkoa wa Simiyu, Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam na Manispaa ya Arusha, zimebaini udanganyifu huo na kuanza kuchukua hatua za awali kwa kusimamisha walimu wakuu wa shule husika na pia kuziagiza mamlaka husika kuwavua uongozi walimu hao.

Taarifa za awali zimeonyesha mpaka sasa katika Mkoa wa Simiyu wamebainika kuwepo wanafunzi hewa 2331 ambapo zaidi ya milioni 10 kila mwezi zikipokelewa kwa wanafunzi hewa.

Mkoa wa Simiyu una jumla ya shule za msingi za serikali 516 na shule za sekondari za serikali 140, ambapo jumla ya walimu wakuu wa shule zote wapatao 656 watavuliwa madaraka yao kuanzia sasa na kutakiwa kurudisha pesa hizo.

Uongozi wa Wilaya ya Kinondoni umemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa manispaa hiyo, kuwavua vyeo walimu wakuu 68 wa shule za msingi kwa tuhuma za udanganyifu wa takwimu juu ya elimu bure na pia umeandika barua kwa Katibu Tawala wa Mkoa ili kumuomba awavue vyeo walimu wakuu 22 wa shule za sekondari. Zaidi ya Sh milioni 70 zimepokelewa kwa wanafunzi hewa.

Kila Mwalimu Mkuu aliyehusika kusababisha ubadhirifu huo wa fedha, atatakiwa kulipa fedha zote kutoka katika mshahara wake huku hatua nyingine zikichukuliwa na Tume ya Utumishi wa Walimu.

Hadi kufikia jana, Wilaya ya Kinondoni imebaini wanafunzi hewa 3,462 kutoka shule 68 za msingi na wanafunzi 2,534 kutoka shule 22 za sekondari. Baadhi ya shule za msingi zilizokutwa na wanafunzi hewa ni Msisiri B, Msewe, Golani, Kibangu, Kimara Baruti, Ubungo Kisiwani, Shekilango, Tandale, Makoka, Mbezi Luis, Kijitonyama, Kinondoni, Mburahati, Makumbusho, Makongo, Kawe A na Ubungo Plaza.

Shule za sekondari ni Boko, Bunju A, Kambangwa, Kawe Ukwamani, Kigogo, Kiluvya, Mbweni, Matosa, Maramba Mawili, Mburahati, Salma Kikwete, Saranga, Temboni, Mabibo, Makoka, Luguruni na Mtakuja.

Katika Mkoa wa Arusha, Walimu Wakuu wa shule za msingi 11 na sekondari 12 wamesimamishwa kazi kwa sababu ya kuongeza idadi ya wanafunzi hewa ili kupata fedha nyingi katika mgawo wa fedha za elimu bure.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mrisho Gambo ameunda timu maalumu kwa ajili ya kuhakiki tena kwa mara ya pili, idadi ya wanafunzi hewa katika shule mbalimbali za serikali walioisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh milioni 26.12.

Baadhi ya shule za sekondari zilizoongeza idadi ya wanafunzi ni Arusha Day, Baraa, Kaloleni, Kimaseki, Kinana, Morona, Moshono, Naura, Ngarenaro, Oloirieni na Suye ambapo wamesababisha serikali hasara ya Sh milioni 23.3.

Baadhi ya shule za msingi ni Azimio, Kimandolu, Magereza, Maweni, Moshono, Naura, Njiro Hill, Olkeryani, Salei, Sokon 1, Terrat na Wema na kwa shule hizo za msingi wameisababishia serikali hasara ya Sh 3,940,008
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.