Sunday, August 21, 2016

BURIANI SHAKILA SAIDI- MALKIA ‘NZINGA-MBANDE’

MAREHEMU SHAKILA SAIDI
NA HEMEDI KIVUYO
Hakika kila Nafsi itaonja Mauti.Sikupata hofu pale nilipopata ujumbe mfupi kutoka kwa Swedy Mwinyi  kwasababu ni kawaida yake kunitumia ujumbe kujuliana hali na kujuzana haya na yale.

Lakini ujumbe wake wa juzi  Usiku ilikuwa tofauti kwani ulielezea  Kifo cha Malkia wa taarab asilia,Mwanakupona,al-hanisa Malkia Nzinga –Mbande Shakila said ( Tatu Said) Mtu niliyempenda kupindukia.

Nimeshindwa kuhimili,na inanipasa kuweka wazi ukimwacha Malika na Mwanahela mwengine ambaye mimi hupenda tungo zake ni Bi Shakila ambaye hatunaye tena.( Mola amrehemu).

Hakuna Msiba mwepesi lakini Miongoni mwa misiba iliyonitoa machozi ni huu wa Bi Shakila said,Mwimbaji asiyezeeka sauti,aliyepangilia mashairi bara-abara,Mwerevu wa lugha ya Kiswahili na Mpigania Uhuru kwa Nchi za Afrika kwakutumia  sanaa ya Uimbaji.( Rejea wimbo viva Msumbiji)

Muziki wa Taarab ( siyo taarab ya sasa) Ndiyo Muziki uliyotajwa kuwa Muziki halisi wa Mwambao Mwa Afrika. Ina historia Ndefu lakini kwa Ufupi ilianzia Mwambao mwa Afrika baada ya kutoka Misri kupitia kwa Omy-Kuruthum na ndipo ilipofika Pwani ya Mombasa .

Siti Binti saad Aliyezaliwa 1880  ambaye pia aliitwa Mtumwa alipokea  ughani huo na kueneza na kisha kuanza kutandawaa mwanzoni mwa miaka ya 1891 pale alipoungana na kundi la mtu mmoja aliyeitwa Mukhsin alii. 

Mpaka kufikia mwanzoni mwa Miaka ya 1928 siti bint saad alikuwa ameongeza wigo wakuimba taarab kiasi cha kupewa hidaya ya kwenda Nchini India kurekodi Nyimbo za Taarab kwa lugha ya Kiswahili tena Kiswahili fasaha.

Waimbaji wengi wa Taarab akiwamo Marehemu Bi Kidude waliimba Nyimbo ambazo zilishaimbwa na Siti Bint Saad na walizirudia ili kumuenzi na kuenzi Nyimbo zake sambamba na kukuza Lugha ya Kiswahili.

Moja ya Tungo za Siti iliyorudiwa na Bi Kidude ni `Kijiti` tazameni tazameni alichikifanya kijiti,kumchukua Mgeni kumchezesha foliti,kenda nae magogoni,kamrejesha maiti.

Kwa hilo utaona Waimbaji wengi wa Taarab Asilia ambayo ndiyo Taarab halisi wanatokea Mwambao wa Pwani kama Lamu Mombasa Kenya ,Tanga na kutumia `’Lahaja` kimtang’ata.

Nyimbo hizo zilikuja kupokewa na akina Juma Bhalo,Maulid Juma,Yusuph Tenge,Abas,Mzee,Bi Kidude,Aisha Abdully maarufu Malika pamoja na kuwa Msomali aliloweya Mombasa na kuchukuliwa hata na kina  Issa Matona ,osman Soud kwa Afrika mashiriki .

Kwa Jitihada za Siti Bint Saad na ndiyo maana akaibuka mahiri kama Shakila said,ambaye nathubutu kusema sauti yake haijawahi kuzeeka mpaka mauti yanamfika.
Ni sauti iliyogoma kwenda sambamba na Umri wake. Nilitamani aendelee Kuimba kutokana na ghani zake zihusuzo mapenzi.

Simwishi hamu ninapokaa kitako ndani kwangu na kweka Tungo za Bi Shakila kwani yeye hunitibu kwa maradhi niliyokuwa nayo.

Mwanzoni Taarab haikuimbwa bali ilighaniwa, na ndiyo maana waimbaji wake walikuwa wanakaa `kitako` na kutulizana huku wakifikisha ujumbe.

 Miaka inavyokwenda na ndivyo taarab inavyozidi kupoteza Mwelekeo na kuichafua jamii badala ya kuijenga kama ilivyoasisiwa kufikisha ujumbe na kukuza lugha ya Kiswahili.

Shakila Said alizaliwa 1949,alianza Muziki wa Taarab wakati Tanganyika inapata uhuru mwaka 1961 na aliolewa mwaka mmoja kabla yakuanza shughuli za muziki yaani 1960.
Alianza Kuvuma zaidi mwanzoni mwa Miaka ya 1980 hasa pale alipotoa wimbo wake `Macho yanacheka`.

Wimbo huo Mpaka leo naamini siyo mimi pekee hata wewe bado unatamani kuusikiliza kutokana na mashairi yake na maudhui yanayokwenda mbele ya hadhira. Aliitumikia Bendi ya JKT kwa zaidi ya Miaka 40 . 

Hakuimba Nyimbo za Mapenzi pekee bali hata za ukombozi kwa Nchi za Frika na Nchi marafiki wa Tanzania,Rejea Wimbo wa `’Viva Samora,viva Msumbiji. ‘Leo twakuvika taji mpendwa Ndugu Samora`Msumbiji kukomboka sisi twaona fahari,umeuleta uhuru si jambo la masikhara, viva Frelimo ,viva Samora”.

Mwalimu Nyerere alikuwa ni mmoja wa viongozi wenye kuvutiwa na uimbaji wa Marehemu Shakila Said naha ta Rashid Mfaume Kawawa. Katika Mikutano ya hadhara Bi Shakila alikuwa akitumbuiza kabla ya Mwalimu Nyerere ama Kawawa Kuongea na hawakuisha kumsifu Bi Shakila.

Mwaka mmoja kabla ya kifo chake yaani 2015 Bi Shakila alikiri kuchoshwa na mahojiano ya Vyombo vya Habari .

 Hiyo ilitokana na umaarufu wake na mchango wake mkubwa katika Tasnia ya sanaa Nchini Tanzania. 

Ingawa hakufaidika na jasho lake na hata kama alifaidika siyo faida inayolingana na jasho lake kwani aliiishia kuuza vitumbua mbagala chalambe.

Ni Miongoni mwa wasanii wasiyofaidika na jasho lake kama ilivyo kwa wasanii wengi wa zamani kutokana na mfumo mbovu.

Bi shakila hatofautiani sana na Bi Malika anayeishi Nchini Marekani kwasasa kwa sauti na Tungo zao na hata Bi Mwanahela anayeishi Mkoani Tanga.

Msikilize Bi Shakila katika baadhi ya Tungo zake tu, kama Macho yanacheka,mapenzi yamepungua,kifo cha mahaba na nyingine utaamini hakubahatisha katika Tungo zake na kwa kizazi hiki sidhani kama pengo lake litazibika.

Kwa kizazi hiki kilichotekwa na fikira za kimagharibi sitarjii kuona mfano wa bi shakila tena.

Tumebaki na Taarab inayokwenda kama kuku aliyokatwa shingo,taarab isiyotazamwa na watoto na wazazi wao.

Nenda Malikia wangu Shakila Said,umenifunza Mengi na Mola wetu atakulipa mema ulotenda.Sitokusahau wala kuacha kukuombea mpaka nitakapokufuata wakati wowote kuanzia sasa.

Mtu aliyekuwa akiniondoa hofu kwa sauti yake muruwa na kunipa nuru na uchangamfu. Nitakuwa nakuskiza ukiwa hauna uhai tena bi Shakila.

Inna lilahy-wa innailahy rajuun)
HEMED KIVUYO ANAPATIKANA KWA SIMU:-
0655 250157/ 0752 250157
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

CCM Blog. Powered by Blogger.