LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 26, 2016

JOHN CHEYO APINGA MAANDAMANO YA CHADEMA YA SEPTEMBA MOSI, ASEMA NI KUKIUKA KATIBA YA NCHI

Mwenyekiti wa Chama cha United Democratic Party (UDP) John Momose Cheyo akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu hali ya kisiasa nchini katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari – Maelezo leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari – Maelezo Tiganya Vicent.
Mwenyekiti wa Chama cha United Democratic Party (UDP) John Momose Cheyo akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu hali ya kisiasa nchini katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari – Maelezo leo Jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari – Maelezo Tiganya Vicent na Kaimu Katibu Mkuu wa Chama hicho Goodlucky Ole Medeye.
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika mkutano na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha United Democratic Party (UDP) John Momose Cheyo (hayupo pichani) leo Jijini Dar es Salaam.

Picha na: Frank Shija
Habari na: Lilian Lundo 
Mwenyekiti  wa Chama cha UDP John Cheyo amewataka Watanzania kupaza sauti na kukataa maandamano ya Septemba Mosi mwaka huu ambayo yameandaliwa na Chama cha Demokrasia (CHADEMA).

Cheyo ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu msimamo wake juu ya  maandamano hayo.

“Watanzania wenzangu jambo la kuwaacha watoto wetu kwenda kupambana na Polisi si jambo zuri, wote tupaze sauti zetu na kusema hapana kwa maandamano ya Septemba Mosi,” alisisitiza Cheyo.

Alisema kuwa, ziko njia mbalimbali ambazo Chadema wanaweza kuzitumia kutatua migogoro, kama vile meza ya mazungumzo na kuachana na maandamano ambayo yanachochea vurugu na hata kutishia amani ya nchi.

Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linapotoa katazo la maandamano ni lazima utii uwepo, kwani Polisi wapo kwa mujibu wa Sheria na  Katiba. Ikiwa Chama hicho hakikuridhika na katazo hilo basi wanatakiwa kuonana na Waziri anayehusika na Jeshi la Polisi.

Akifafanua zaidi alisema kuwa Rais Magufuli amekuwa akichukua hatua za makusudi za  kutatua matatizo mbalimbali kama vile kupambana na ufisadi, ambapo viongozi wengi wa Serikali wamesimamishwa kazi au kufukuzwa  kutokana na kujihusisha na masuala ya rushwa.

Mwenyekiti huyo wa UDP amewataka watanzania kumuunga mkono Mhe. Rais Magufuli ili aweze kutimiza ndoto zake na yale ambayo ameyaahidi kwa ajili ya nchi ya Tanzania.

Aidha Cheyo aliwasifu viongozi wa Dini ambao walikaa na Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)  na kukubali kurudi bungeni bila pingamizi lolote. Amewataka viongozi hao wa dini kuendelea kuzungumzia suala la amani kwa Watanzania na Viongozi wa kiasa ili kudumisha amani ya nchi.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages