LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 27, 2016

CAG ASSAD AONGOZA KIKAO CHA 70 CHA BODI YA UKAGUZI YA UMOJA WA MATAIFA

Mwenyekiti wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa
 Mataifa, Prof. Mussa Assad akizungumza
 wakati wa hafla ya  kuiaga  Ofisi yaMkaguzi
na Mdhibiti wa Hesabu  za Serikali ya
Uingereza ambaye amemaliza ujumbe
 wake wa miaka sita katika   Bodi.
Na Mwandishi Maalum, New York
Bodi ya  Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa,   ambayo   Mwenyekiti wake ni   Mkaguzi na Mdhibiti  n  Mkuu  wa  Hesabu za Serikali, ( CAG) Profesa Mussa J. Assad jana  ( Jumanne)  imerejea  na kuidhinisha  ripoti  kumi na moja za  Mashirika, Mifuko  na shughuli  mbalimbali za Umoja wa Mataifa.

Katika kikao hicho cha   70 kilichofanyika  hapa  Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa,  pamoja na kuidhinisha ripoti za  Mashirika  na  Mifuko  iliyochini  chini ya Umoja wa Mataifa,  pia Bodi ilipokea  taarifa mbalimbali za kiutendaji zinazohusiana na   majukumu ya  Bodi hiyo.

Wajumbe wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa, ni    Mkaguzi na  Mdhibiti  Mkuu wa Hesabu wa Serikali ya India,  Bw. Shashi Kant Sharma,    Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Uingereza, Sir Amyas Morse, na Mkaguzi na  Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof. Mussa J. Assad.

Pamoja na  kupitia na kuridhia ripoti hizo kumi na Moja, na  kupokea  taarifa za kiutendaji, shughuli nyingine iliyofanywa na  Bodi ya  Ukaguzi ilikuwa ni pamoja na  kuiaga Ofisi ya Ukaguzi ya Uingereza  baada ya  kumaliza  kipindi chake cha miaka sita ya uhudumu katika Bodi hiyo.
Hafla ya  kuagwa kwa   Ofisi  ya Ukaguzi ya Uingereza ilihudhuriwa  na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Bw. Ban Ki Moon pamoja na wadau mbalimbali ambao ni wateja wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa.

 Nafasi ya  Ofisi ya Ukaguzi ya Uingereza  imechukuliwa na Ofisi  ya Ukaguzi ya Ujerumani ambayo  imekaribishwa  rasmi kuwa mjumbe wa Bodi  hiyo.

Akizungumza katika hafla  hiyo ya kuiaga  ofisi ya Ukaguzi ya  Uingereza na  kuikaribisha Ofisi ya Ukaguzi  ya Ujerumani,  Mwenyekiti wa Bodi,  Prof.  Mussa Assad amemshukuru Sir. Amyas Morse  kwa mchango wake yeye binafsi na Ofisi yake kwa uwajibikaji mkubwa na weledi wa hali  ya  juu ambao umefanikisha utekelezaji  wa mamlaka na  majukumu ambayo Bodi hiyo imekabidhiwa na Umoja wa Mataifa.

Akiikaribisha   Ofisi ya   Mkaguzi  na Mdhibiti Mkuu wa Ujerumani,  Prof. Assad  ameelezea matumaini yake  ya kufanya kazi kwa karibu na ushirikiano wa hali  ya juu na  mjumbe huyo ili  kwa pamoja waweze kutekeleza majukumu na mamlaka  waliyokabidhiwa na  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Bodi ya Ukaguzi  ya Umoja wa Mataifa, ilianzishwa   mwaka 1946  na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa lengo la kukagua hesabu za Mashirika,  Mifuko na Taasisi nyingine zilizo chini ya Umoja wa Mataifa,   ili  pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba Taasisi hizo zinatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa kanuni na taratibu za  Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na matumizi yenye tija na adilifu ya   bajeti  kulingana na  mamlaka ya   Mashirika na Taasisi hizo.
Bodi ya Ukaguzi inatekeleza majukumu yake  kama chombo huru na taarifa zote za ukaguzi huwasilishwa kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pamoja na wateja  ambao  wanakaguliwa  na  Bodi hiyo.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages