Saturday, May 14, 2016

UN YAIPONGEZA TANZANIA KWA UHARAKA WA KUCHUNGUZA TUHUMA ZA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA

Na Mwandishi Maalum
Umoja wa Mataifa  umeipongeza Tanzania  kwa namna  ambavyo imechukua hatua za haraka za kukabiliana na  tuhuma za udhalilishaji wa kijinsia zinazowahusisha baadhi ya  walinzi wa amani  wanaohudumu katika Misheni ya Kulinda Amani katika  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo( DRC).

“Tanzania  imeweza  ndani ya siku tano tangu kupokea tuhuma dhidi ya  walinzi wake wa amani kuunda   timu ya kitaifa ya uchunguzi kwajili ya kuzifanyika kazi tuhuma hizo.  Hatua hii na utashi ulioonyeshwa na Tanzania ni hatua nzuri na inayopashwa kupongezwa na inaonyesha namna gani inavyochukulia kwa uzito wa hali juu  tuhuma hizo”.

Pongezi hizo  zimetolewa  mwishoni wa wiki ( Ijumaa) na Bw. Atul Khare,  Naibu Katibu Mkuu  Mwandamizi anayeongoza Idara ya Field Support katika Umoja wa Mataifa.

Mwishoni  mwa wiki ,  Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,   aliandaa mkutano  ambao ulikuwa na lengo la kutoa taarifa  ya maendeleo na  mwelekeo wa Umoja wa Mataifa katika kukabiliana na  tuhuma za udhalilishaji wa kijinsia  zinazowakabili walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa,   walinzi wa Amani wa Kimataifa,  na wafanyakazi raia.

Katika  taarifa yake,Bw. Khare amesema, utaratibu uliopo unaitaka nchi ambayo walinzi wake wametuhumiwa kujihusisha na vitendo vya udhalilishaji pamoja na   hatua nyingine, kuunda timu yake ya  kitaifa ya uchunguzi ndani ya  siku kumi, lakini  Tanzania  iliunda timu hiyo ndani ya  siku tano  na kuanza kazi jambo ambalo amesisitiza linapashwa kuigwa na nchi nyingine.

Akabainisha kwamba kinachosubiriwa sasa  kutoka Tanzania ni  taarifa rasmi ya kukamilishwa kwa uchunguzi huo na hatua ambazo zitakuwa zimechukuliwa kwa walinzi ambao watakuwa wamethibitika kujihusisha na vitendo hivyo.

Tuhuma  za udhalilishaji   wa kijinsia  dhidi ya  baadhi ya walinzi hao wa Amani wa Tanzania  ziliibuliwa na Umoja wa Mataifa  mwezi March mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako  Manongi, amesema utovu wa nidhamu  uliofanywa na walinzi wachache hauwezi kuchafua kazi nzuri na sifa  ya kutukuka  ya  Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika Misheni mbalimbali za kulinda Amani chini ya Umoja wa Mataifa.

Akasema  Balozi, ni kwa kutambua  kazi hiyo ya kutukuka na  ambayo pia imepelekea  baadhi ya wanajeshi wa Tanzania kupoteza maisha yao kishujaa wakati wakiwasaidia wananchi wa mataifa mengine kuwa na amani. Tanzania inalichukulia kwa uzito  wa  kipekee   tuhuma za udhalilishaji wa  kijinsia na kwamba wale wote wataokabainika  hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Akaongeza kwamba Tanzania  imeamua kuwaalika wataalamu  kutoka Umoja wa Mataifa kwenda nchini Tanzania  ambapo watashirikiana na wakufunzi wa JWTZ katika kuimarisha mitaala ya ufundishaji inayohusiana na  masuala ya ulinzi wa raia hususani eneo la udhalilishaji wa  kijinsia.

Vilevile Balozi Manongi amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na  Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha kwamba vitendo  hivyo  viovu  dhidi ya raia wasiokuwa na hatia vinakomeshwa ili pamoja na  mambo mengine kurejesha heshima ya  Umoja wa Mataifa na heshima ya nchi zinachochangia  wanajeshi  na polisi katika misheni za kulinda Amani. Lakini kubwa zaidi  kurejesha imani kwa wananchi wanaohitaji ulinzi.

Akielezea kwa ujumla kuhusu kadhia hiyo ya udhalilishaji wa kijinsi, Bw. Khare amesema, nchi nyingine  zinazochangia  walinzi wa Amani  na ambazo  pia  walinzi wao wametuhumiwa   zinaendelea  ushirikiano kwa kuchukua hatua mbalimbali ingawa pia zipo  zinazosuasua. Nchi ambazo zimetoa ushirikiano  ukiacha Tanzania ni Afrika ya Kusini, DRC, Misri na Bangladesh.

Amezitaja  hatua hizo kuwa ni pamoja na  kuwafikisha katika mahakama za kijeshi wale wanaokutwa na hatia, kufungwa,  kufukuzwa kazi na kutoshiriki kabisa katika misheni za  kulinda Amani na kutoa misaada kwa  wahanga.

Akaongeza pia kwamba nchi  nyingi  zimeimarisha mitaala ya ufundishaji kwa walinzi wa amani, kuandaa timu za  uchunguzi ambazo zinakuwa tayari wakati wowote  zitakapohitajika, huku nyingine  zikihakikisha kwamba zinakuwa na wataalamu  wa  masuala  ya  sheria miongoni mwa walinzi wa Amani.


Bw. Khare amesisitiza Umoja wa Mataifa unatambua mchango mkubwa wa walinzi wa Amani pamoja na mazingira magumu ya utekelezaji wa mamlaka  yao. Hata hivyo anasema vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia havipashwi kuvumiliwa wala kufumbiwa  macho na kwamba kila nchi inaowajibu wa kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria  watuhumiwa wanaothibitika  kuhusika na  ukatili huo na kwamba  ushirikiano na misaada  kwa waathirika ni jambo la muhimu sana.
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.