LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 22, 2016

TANZANIA YATAKA WAATHIRIKA WA DAWA ZA KULEVYA WASIFUNGWE JELA

Na Mwandishi Maalum, New York
                                 Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesema,    waathirika wa   dawa haramu za kulevya wanatakiwa kusaidiwa   badala ya kuwafunga jela.
                                 Hayo yameelezwa jana ( Alhamis) na   Balozi Tuvako Manongi,  Mwakilishi wa  Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  katika   Mkutano  Maalum wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  uliokuwa ukijadili mafanikio, juhudi na changamaoto za kukabiliana na  tatizo la  dawa  za kulevya  duniani.
                                 Balozi Manongi ameongoza  ujumbe wa Tanzania katika  mkutano   huu  wa  siku tatu na  ambao umewashirikisha Viongozi  Wakuu  wa Nchi, Serikali na Mawaziri kutoka mataifa  mbalimbali.
                                 “Tunapoangalia mbele,  mkazo wetu uwe katika kuhakikisha  tunapunguza  idadi ya watu wanaojihusisha na matumizi ya dawa haramu za kulevya na   tunapunguza idadi ya watu wanaofariki kutokana na  matumizi ya dawa hizo” akasema Balozi
                                 Na  kusisitiza “ Lazima tuhakikishe wale wenye makosa madogo  hawaishii jela ambako matatizo yao yatokanayo na  dawa za  kulevya yatazidi kuwa  makubwa zaidi. Lakini pia tunao wajibu wa kuhakikisha huduma  wanazopewa zinazingatia afya   na haki za binadamu.”
                                 Mwakilishi huyo wa Tanzania,   amewaeleza washiriki wa mkutano  huo kuwa Tanzania,  kama ilivyo kwa mataifa mengine  Tanzania haijapona na balaa hilo la dawa za kulevya.
                                 “Tanzania hatujasalimika na balaa hili, nchi yetu,  imekuwa sehemu ya kupitisha dawa za kulevya kuelekea nchi nyingine. Lakini  kiasi  fulani cha dawa hizo kina baki  nchini  na hivyo  kuathiri wananchi wetu ambao wengine wao tayari wameshaathirika kwa umaskini na matatizo mengine”.akaeleza  Balozi
                                 Akasema, ni kweli kwamba, tatizo la  dawa  za kulevya, ni  kubwa na lenye changamoto nyingi,  na ni tatizo ambalo halina   ufumbuzi wa mara moja, lakini pia ni tatizo ambalo lisiifanye  jumuiya ya kimataifa kukata tamaa.
                                 Akasema Jumuiya ya Kimataifa inatakiwa kupitia mkutano huo  kuhakiksha kwamba inakuja na mikakati  mipya ikiwa ni pamoja na kutekeleza yale  yaliyopendekezwa kwenye tamko lililopitishwa kwenye mkutano huo.
Balozi Manongi ameongeza kuwa hapana shaka sera na  sheria zilizopo hivi sasa zimeshindwa kudhibiti wimbi la athari za dawa za kulevya. Na  kwa kutambua ukubwa na changamoto za tatizo hilo na athari zake kwa wananchi wa Tanzania , Serikali imejiwekea mipango na mikakati mbalimbali  ya kulikabili.
                                 Baadhi ya  mikakati hiyo ni  pamoja na kuwasaidia waathirika wa dawa za kulevya  na ambao wapo katika hatari kubwa ya kuambukizwa na kuambukiza  magonjwa mbalimbali  yakiwamo ya  virusi vya ukimwi na Hepatitis B na  C,  
                                 Akaelezea  pia  juhudi zinazofanywa na  serikali katika utungaji na uboreshaji wa sheria zinazolenga kuwabana wasafirishaji, wauzaji na wasambazaji wa dawa hizo,  ikiwamo mikakati  ya kufuatilia kwa makini  mwenendo mzima wa  biashara ya dawa za kulevya , matumizi na  matumizi   ya  madawa mengine ya aina  hiyo.
                                 Balozi  Manongi amesema pia kwamba tatizo la dawa za kulevya linarudisha nyuma juhudi za pamoja na kuwapatia watanzania  maisha yenye hadhi na  inaathiri nguvu kazi ambayo inahitajika kufikia malengo ya  kiuchumi  na maendeleo ya jamii.
                                 “ Kama  hiyo haitoshi dawa za kulevya zinachochea   uhalifu na vitendo vya jinai vikiwamo  vinavyohusisha    ujagili wa wanyamapori na misitu, na    kuongeza  kazi ya ziada kwa vyombo vya sheria na mfumo wa kitaifa wa utoaji  huduma za afya”. Amesisitiza Balozi
                                 Katika  vita hivyo dhidi ya  dawa za kulevya na  umuhimu wa kuwasaidia waathirika, Balozi  Manongi amesisitiza kwamba ushirikiano wa pamoja baina ya mataifa,  taasisi za kimataifa na  asasi  zisizo za kiserikali  unahitajika sana kwa kile alichosema  hakuna  nchi inayoweza  kukabiliana na tatizo hilo peke  yake.
                                 Akaongeza pia kwamba  utekelezaji wa mikataba mbalimbali  ya kimataifa,  utasaidia  sana  katika kuyakabili  makundi na mitandao ya  kihalifu na rushwa.
                                 Hoja zilizopewa  msisitizo na wazungumzaji wengi  ni pamoja na  hiyo ya kuwapatia waathirika matibabu na kutowafunga kwa kile walichosema hakuna mzazi anayependa kuona mtoto wake akifungwa na badala yake angefurahi kuona  anasaidiwa.
                                 Pamoja na  kuzungumzia adhabu ya kuwafunga waathirika wa dawa za kulevya, wazungumzaji wengi pia wamepinga au kukemea  adhabu ya kuwanyonga wanaokamatwa  kuhusika na  masuala ya mihadarati.
                                 Aidha viongozi wengine  walieleza kwamba  wameanza  mikakati ya kuwapatia wananchi wao hasa maskini utalaamu wa kulima  mazao  mbadala badala ya kutegemea kulima mazao yanayotumika kutengeneza dawa za kulevya  kama sehemu ya kuendesha maisha  yao.
                                 Wengine wameeleza  juhudi  ambazo serikali zao zinafanya katika kukabiliana na  mitandao  na magenge wafanyabiashara wa dawa za kulevya , juhudi   zinazohusisha pia kukamata na kutaifa mali zao.
                                 Wako waliokwenda mbali Zaidi kwa kutaka nchi ambazo kwa namna moja ama nyingine zimelegeza sheria zao na kuruhusu  matumizi ya dawa za kulevya kama vile bangi basi nazo ziwajibike kwa kutoa ushirikiano  na kuonyesha utashi wa kisiasa.
                                 Marais wanaotoka katika nchi ambazo  zimeathirika zaidi na   biashara za dawa za kulevya na mitandao ya kihalifu inayojihusisha na  biashara hiyo,  walikwenda  mbali zaidi   kwa kueleza kuwa,  ikiwa    nchi zilizoendelea na ambazo ni wadau wakubwa hazitaonyesha ushirikiano ni wazi kwamba vita dhidi ya  dawa za kulevya itashindikana.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages