LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 31, 2016

MONUSCO YAONGEZEWA MUDA WA KUENDELEA KULINDA AMANI DRC

Na Mwandishi Maalum . New York
Baraza  la Usalama la Umoja wa Mataifa,   limepitisha  azimio jipya ambalo pamoja na mambo mengine  limeiongezea   kwa mwaka mmoja Misheni ya kulinda Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( MONUSCO ).
Sambamba na kuiongezea mwaka MONUSCO,  Baraza la Usalama pia limesitisha zoezi la kupunguza  walinzi wa Amani 1,700 kama ilivyopendekezwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Huku Azimio  hilo likitamka  bayana kuwa  MONUSCO inatakiwa kuwa na  walinzi wa Amani wasiopungua 19,815, waangalizi 760,  pamoja na polisi 1,050. 
Ndani ya MONUSCO  kuna Brigedi maalum  ijulikanayo  kama Force Intervention  Brigade (FIB) yenye mamlaka nguvu ya kuyashughulikia makundi ya waasi yenye silaha. Brigedi hii  inaundwa na walinzi wa amani kutoka Tanzania, Afrika ya  Kusini na Malawi.
Kwa mujibu wa Azimio hilo jipya lililopitishwa  na wajumbe 15 wa Baraza  la  Usalama,  uamuzi wa   kuiongezea muda wa mwaka mmoja   MONUSCO  hadi Machi 31,2017, pamoja na kutotoa baraka za kupunguzwa kwa walinzi  wa Amani kunatokana na  taarifa za kuzorota kwa hali ya usalama hususani katika kipindi  hiki cha mpito kuelekea uchaguzi mkuu.
Jamhuri  ya Kidemokrasia ya  Kongo inatarajiwa kufanya uchaguzi wa Rais mwezi Novemba mwaka huu na tayari kuna taarifa za kuwapo kwa  sintofahamu  miongoni mwa makabila kutokana na tofauti za kisiasa, kuongezeka kwa makundi ya waasi wenye silaha,  kuzorota kwa hali ya kibinadamu  hali inayoitia wasiwasi Jumuiya ya Kimataifa kwamba   kunauwezekano  wa  kutokea machafuko.
 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,  kupitia  Azimio hilo,  limeionya  Serikali ya DRC  kuhusu kuchelewa kwa maandalizi ya  uchaguzi wa rais, huku likitoa wito kwa serikali  wa kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria wale wote wanaotuhumiwa kuhusika na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, na makosa ya uhalifu wa kivita  na ukatili dhidi ya  binadamu.
Vile vile  Baraza la Usalama limetoa wito kwa serikali na wadau wengine pamoja na Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi ( CENI) wa kuhakikisha uwazi   kuhusu mchakato wa uchaguzi ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa kalenda ya uhakika  ya uchaguzi.
Aidha   serikali imetakiwa kutenga bajeti ya kutosha kwaajili ya  uchaguzi na kuweka maadili ya uchaguzi na kuchukua hatua za kuboresha daftari la wapiga kura pasipo kuchelewa.
 Kuhusu makundi  ya waasi wenye silaha,  wajumbe wa Baraza la  Usalama wametoa wito wa kutaka kurejeshwa mapema  iwezekanavyo   operesheni ya  pamoja kati ya MONUSCO na Jeshi la DRC ( FARDC) dhidi  ya makundi  hayo ya waasi hususani kundi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda ( FDLR).Makundi mengine ya waasi na ambayo yameendeleza matukio ya mauaji  ya raia wasio na hatia na ambayo pia yanatakiwa kushughulikiwa ni  pamoja na kundi la ADF, Mai Mai  na LRA
Azimio hilo lenye kurasa  15 pia limetilia mkazo kuhusu ulinzi wa raia,  ulinzi wa watoto na  linakemea  vikali  kuhusu  vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages