Thursday, March 17, 2016

JAFO ATUA SOKO LA SAMAKI FERRY KUKAGUA UTEKELEZAJI WA MAAGIZO YAKE.


JAFO ATUA SOKO LA SAMAKI FERRY KUKAGUA UTEKELEZAJI WA MAAGIZO YAKE.Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI  Mh. Selemani Jafo leo asubuhi ametembelea soko la samaki la Ferry ili kukagua utekelezaji wa maagizo yake aliyoyatoa kwa Mkurugenzi wa manispaa ya Ilala na wasaidizi wake hivi karibuni.
Mh. Jafo hivi karibuni alipotembelea soko hilo aliagiza uongozi wa manispaa ya Ilala kufanya mambo makuu yafuatayo:-

 -Kukomesha matumizi ya majiko kuni katika eneo la kukaangia samaki ambayo yalikua yanasababisha Moshi na harufu mbaya katika eneo hilo la samaki.
-Kuanza kutumia haraka majiko ya kisasa ya kutumia gesi asilia ambayo ni rafiki kwa mazingira
-Kufanya ukarabati wa miundombinu ya soko ili kuweka soko katika hali ya usafi
-Kuunda Bodi ya Soko kwa ajili ya usimamizi na uongozi wa soko.

Akikagua utekelezaji wa maagizo hayo Mh. Jafo alitembelea soko la samaki na eneo la majiko ya kukaangia samaki akiwa ameandamana na Mwenyekiti wa bodi ya Soko bwana Sato Massaba,  Mkurugenzi wa manispaa ya Ilala bwana Isaya Mguluni na watendaji wa manispaa ya Ilala na kushuhudia majiko yote ya kuni yakiwa yameondoshwa na kuwekwa majiko ya gesi yanayotumika katika kukaangia samaki.

Aidha akitoa maelezo kwa naibu Waziri wa TAMISEMI, Mkurugenzi wa manispaa ya Ilala alieleza kuwa majiko ya gesi tayari yameanza kutumika,  miundombinu imekarabatiwa na Bodi ya Soko imeshaundwa. Mkurugenzi alimtambulisha kwa Mh. Jafo Mwenyekiti wa bodi ya soko la samaki bwana Sato Massaba.

Mh. Jafo alieleza kuwa ameweka utaratibu maalum wa kufuatilia maagizo yote yanayotolewa na ofisi yake ili kuhakikisha kuwa yanatekelezwa kwa wakati.

" Nimeweka utaratibu wa kufuatilia maagizo yote yanayotolewa na ofisi yangu. Nafurahi kuona mmekamilisha kwa wakati. Leo hii maagizo yale yangekua hayajafanyiwa kazi, Mkurugenzi na timu yako mngekua kwenye hali ngumu..." alisema Mh. Jafo.

Mwisho Mh. Jafo alisisitiza kuwa soko la Ferry linapaswa kuwa safi wakati wote ili kuithibitishia jamii yote kuwa watanzania tunaweza kujisimamia na kufanya mambo yetu vizuri. Jafo alisema kuwa soko la Ferry liko karibu na Ikulu na hivyo si taswira nzuri likiwa katika hali ya uchafu na kutoa Moshi na harufu mbaya.
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.