LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 12, 2016

KIPANGA SHERIA,SHERIA,SHERIA




SHERIA, SHERIA, SHARIA
(Dr. Muhammed Seif Khatib)

Labda tukubaliane kuwa kila jambo huwa na utaratibu wake ili likamilike.  Mfano mzuri  ni wa taratibu za mchezo wa kabumbu au  wengine huiita kandanda, mchezo unaongozwa kwa kupendwa duniani. Una  muda wake wa kucheza. Dakika  tisini. Una  idadi yake ya wachezaji, ishirini na mbili.  Wengine husema hata refaa naye ni mchezaji.  Unao mwamuzi na wasaidizi wake wawili. Unao  muda wa kupumzika.  Lakini pia unao sheria zake za kuongoza mchezo huo.  Ingawa unaitwa mpira wa miguu, lakini golikipa yeye anaruhusiwa kutumia mikono yake!  Ingawa unaitwa mpira wa miguu, lakini mchezaji akitumia kichwa  kufunga goli siyo kosa.  Lakini  lenye uzito zaidi ni kuwa mwamuzi ndiye mwenye kauli ya mwisho akiwa uwanjani.  Kwa hali hii, wale wote wanaocheza mchezo huo hutakiwa wafate sheria, kanuni na maamuzi ya mwamuzi.  Na kwamba maamuzi yake hayawezi kutenguliwa. 

Hayo ndiyo yaliyojiri huko Zanzibar mwaka 2015 mwezi wa Oktoba.  Ulikuwepo  Uchaguzi Mkuu ambao ulishirikisha vyama vya siasa ambavyo vina usajili wa kudumu.  Zipo taratibu za kuendesha uchaguzi unaohusika.  Vyama  vya siasa na viongozi wake wote waliweka saini kukubali kushiriki katika uchaguzi. Wote  walikubaliana kuwa chombo kinachosimamia ni Tume na siyo mtu aitwaye Jecha.  Na kwa bahati mbaya ndani ya Tume wamo pia wawakilishi wa vyama vikuu vya siasa vya Zanzibar.  Nao wote walikubaliana kuwa Tume ndiyo mwamuzi halali na kwamba uamuzi wake wowote hauwezi kuhojiwa na mtu yeyote au mahakama  yeyote.  Aidha Tume haitakiwi kuingiliwa na mtu yeyote. Si Sheikh si Askofi. Si Jaji si Rais.  Ni Tume huru Tume baada ya kutanabahi kuwa uchaguzi umefanyiwa hujuma, takwimu za kura zimechezewa, wapiga  kura hasa Pemba wamenyimwa haki yao ya kupiga kura, ikaamua uchaguzi ufutwe.  Baya na kubwa kuliko yote ni kule kwa mgombea wa Rais mmoja kunyakua mamlaka ya Tume ya kujitangazia matokeo yake ya ushindi wa urais.  Hili ni kosa kubwa la kijinai ambalo lingeweza kuzua maafa makubwa na kusababisha umwagaji wa damu.  Huyu  aliyetenda kitendo hiki hapaswi kuacha bila mkono wa sheria kuchukua mkondo wake.  Zanzibar hakuna mgogoro na wala hakuna kosa kwa mtu aitwaye Jecha.  Uchaguzi umefutwa na chombo halali. Uchaguzi  umefutwa na Tume kwa kufata taratibu, kanuni na sheria. Uchaguzi haukufika hatima yake hivyo hakuna mshindi wa Uraia wala hakuna wawakilishi au madiwani. Utaratibu  wa kutangaza mshindi wa urais wa Zanzibar unajulikana.  Mwenyekiti wa Tume anaweza kwa Jecha au Mazurui, muhimu ni mamlaka siyo jina, nasaba au dini ya mtu. Mwenyekiti  hakukamilisha kazi ya kukusanya matokeo halali na kuyatangaza yote.  Hivyo hakupata jumla ya kura  halali za wagombea wote.  Ili  mgombea wa urais wa Zanzibar ashinde kihalali yafuatayo yafanyike.  Kura  halali za wagombea wa urais zikusanywe zijumlishwe, zihakikiwe na baada ya kuridhika, zitamkwe rasmi na Mwenyekiti wa Tume.  Atamkwe rasmi nani ameshinda kwa kura ngapi.  Hilo bado  halikufanyika.  Pia  aliyetajwa kama ameshinda apewe cheti cha uthibitisho ya ushindi wake.  Hakuna aliyetajwa wala aliyepewa cheti cha uthibitisho wa ushindi.  Hatua nyingine ingafata kwa aliyeshindwa ni kuwekwa siku maalum ya kuapishwa huyu Rais mteule.  Siku hiyo haikuwekwa kwa sababu Jaji hajapewa jina la mgombea aliyeshinda.  Hatua ya mwisho ingekuwa Rais Mteule wa Zanzibar kuapishwa hadharani na Jaji Mkuu wa Zanzibar.  Nalo hilo halikufanyika kwa vile hakuna mgombea urais aliyetangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.  Hivi basi kwa kufata taratibu na utawala wa sheria uchaguzi wa Zanzibar haukufika mwisho.  Kurejewa siyo kosa, dhambi wala kuvunjwa kifungo chochote cha sheria au Katiba.  Urais ni kazi ya heshima.  Ikulu ni pahapa patakatifu.  Huwezi kukabidhi vitu hivi kwa mtu mmoja kinyume na sheria.  Utawala bora ni kufata sheria na taratibu ambazo watu wenyewe wamejiwekea. Watu waungwana na wastaarabu hufata sheria.  Rudini Wazanzibar katika uchaguzi ili muwapate viongozi halali akiwemo Rais.  Sheria, sheria, sheria!

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages