Wednesday, January 27, 2016

TANZANIA YATAKA UMOJA WA MATAIFA KUZINGATIA MISINGI ILIYOJIWEKEA

Na   Mwandishi Maalum, New  York
Wakati  Tanzania ikipongeza, kusifu na kushukuru uhusiano na ushirikiano wake na Umoja wa Mataifa kupitia  Mifuko  na Mashirika yake ya  Maendeleo,  imeutaka pia Umoja  huo kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia, kanuni, taratibu, sheria na misingi iliyojiwekea ili iendelee  kujijenga heshima.
 Hayo yameelezwa jana jumatatu na  Mwakilishi wa  Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa  Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, wakati  wa mkutano wa Bodi   za   Mashirika ya  Umoja wa  Mataifa UNDP, UNFPA na  UNOPS.    Tanzania ni mjumbe wa  Bodi  katika Mashirika hayo.
 Katika  siku ya kwanza ya  mkutano ,  mkutano uliofunguliwa na Mtendaji Mkuu wa UNDP, Bi Helen Clark,    Balozi  Manongi  amesisitiza kwamba,   ili  Umoja wa Mataifa  uendelee kujijenga heshima na  kuheshimika,  unapashwa kutoruhusu watendaji  wenye ajenda na maslahi binafsi kufanya kazi katika  Mashirika ya Umoja wa  Mataifa.
“ Umoja wa Mataifa  wakati wote  umekuwa sehemu na  mdau mkubwa katika uimarishaji  na ujenzi wa  utawala  bora katika nchi nyingi , Tanzania  ikiwamo. Wajibu wa Umoja wa Mataifa utabaki kuwa  halali na wenye nguvu  endapo wale ambao wamepewa  dhamana ya kutenda kwa niaba yake watatambua na kuheshimu imani na  wajibu uliotukuka ambao wamepwa kuutekeleza ” akasisitiza Balozi Manongi
Akaongeza kwamba, mashabiki  hawapaswi kupewa nafasi, wala kuvumiliwa na kuwa sehemu ya miongoni mwa watendaji wa chombo hicho wasipewe nafasi,  wala wasivumiliwe  kuwa miongoni mwa watendaji wa chombo hicho.
Akizungumzia kuhusu  rasimu  ya  Taarifa ya  Mpango wa Utekelezaji  kuhusu  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Country report) kwa kipindi cha 2016-2021) ambayo imewasilishwa mbele ya Wajumbe wa Bodi wa UNDP,  Balozi Manongi amesema,  mapendekezo  yaliyomo kwenye  rasimu na ambayo imeshirikisha wadau mbalimbali  inajumuisha mawazo na mapendekezo kutoka pande zote za  Muungano na imetokana na misingi ya ushirikiano kati ya UNDP na Serikali ya Tanzania.
Vile vile akasema rasimu  hiyo imejumuisha vipaumbele vinavyoainishwa  katika Dira ya  Taifa ya 2025 kwa upande wa Tanzania Bara ,  Dira ya  2020 kwa upande wa  Zanzibar,  mkakati wa  kupunguza umaskini kwa pande zote za Muungano  pamoja  na Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano.
“ Tunaishukuru UNDP- Ofisi ya Tanzania kwa ushirikiano wake katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwano mikakati ya  kupunguza umaskini, ushirikiano huu   umekuwa mzuri ingawa unachangamoto zake” akasisitiza Balozi Manongi
Akaeleza kwamba, kutokana  na umuhimu wa mwaka huu wa 2016 ambao pamoja na mambo mengine  ni  kuanza kwa utekelezaji wa Agenda ya Maendeleo Endelevu ( Agenda 2030) Tanzania itaendelea kushirikiana  kwa  karibu na  UNDP katika utekelezaji wa  Agenda hiyo huku mkazo ukiwa ni katika  kupungua ama kuondoa umaskini   uliokithiri kwa makundi ya mbalimbali ya  jamii  hususani wanawake.
Akasema , Serikali imejipanga vema katika utekelezaji wa mipango mbalimbali inayolenga katika kuboresha maisha  ya wananchi  wake. Ikiwa ni pamoja na  kutatua tatizo la uhamaji wa  wananchi wake  kutoka  vijijini na kwenda katika miji mikuu hususani vijana kwa lengo la kutafuta ajira na hali bora  ya maisha.
Akasema kuwa wajibu au  madhumuni  ya msingi   UNDP ni kupunguza umaskini, ni kwa sababu hiyo Tanzania ingependa kuiona UNDP ikijielekeza zaidi katika jukumu lake hilo la msingi kama  inavyoelekezwa katika  maazimio  mbalimbali ya Baraza Kuu la Umoja wa  Mataifa.
Kwa upande wa ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu zinazohusu maeneo  mbalimbali,  Balozi Manongi amesisitiza kwamba  UNDP inapashwa kufanya kazi kwa karibu na kwa ushirikiano na  Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kile alichosema ndicho chombo cha serikali chenye dhamana juu ya  masuala yote  yahusuyo takwimu.
Na kwa sababu hiyo akasema Tanzania inaridhishwa na taarifa ya kwamba UNDP itashirikiana na  Ofisi  hiyo ya Taifa ya  Takwimu katika Nyanja mbalimbali zikiwamo za uwezeshaji kwa lengo  la kusaidia katika  uhuishaji wa takwimu.

Aidha  Tanzania  imesisitiza kuhusu  umiliki  katika uendeshaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo pamoja na kiushauri   UNDP kuhakikisha kwamba fedha zinazotengwa kwaajili ya   miradi ya maendeleo zinakwenda kufanya kazi iliyokusudiwa na si vinginevyo. 
Share:

Select Language

CCM Blog VIEWERS

All posts in this blog

General comments/advise

Google+ Followers

Powered by Blogger.