LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 16, 2015

RAIS KIKWETE KUELEZEA UMOJA WA MATAIFA MAENDELEO YA KAZI YA JOPO ANALOLIONGOZA

Na  Mwandishi Maalum, New York
Rais Jakaya Mrisho Kikwete,  ambaye ni Mwenyekiti wa Jopo la Ngazi ya  Juu kuhusu  Mwitikio wa Kimataifa wa   Majanga ya Kiafya, anatarajiwa Ijumaa wiki hii, kueleza mbele ya  wajumbe wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo ya kazi  ya jopo  hilo tangu kuundwa kwake.

Jopo la Ngazi ya juu kuhusu mwitiko wa Kimataifa wa majanga ya kiafya  liliundwa mwezi wa  nne mwaka huu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Ban Ki  Moon, ambapo  Rais Kikwete  amepewa jukumu  la  kuongoza jopo hilo.

Taarifa ambazo zimeufikia  Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika  Umoja wa Mataifa, zimebainisha kuwa  Mhe. Rais atawazungumza  wajumbe wa  nchi  wanachama wa Umoja wa Mataifa  mara  baada ya kumalizika  kwa  mkutano wa tatu wa jopo  hilo  unaofanyika hapa  Makao Makuu ya Umoja wa  Mataifa.

Wajumbe  wengine  wa Jopo hili   ni  Bw.    Celso Amorim ( Brazil), Micheline Calmy ( Switzerland), Marty Natalegawa  ( Indonesia) Joy Phumapi ( Botswana) na  Rajav Shah ( USA).

Jukumu  kubwa ya  jopo hilo  kwa mujibu wa hadidu za rejea,  pamoja na mambo mengine,  ni kutoa mapendekezo ya  namna ya  kuimarisha mifumo  ya kitaifa na kimataifa katika   kuzuia na kukabiliana na  majanga ya kiafya ikiwa ni pamoja na  kujifunza   kuhusu   mwitikio wa Jumuiya ya Kimataifa kufuatia  kuibuka kwa   janga la ugonjwa wa Ebola.

Katika utekelezaji wa majukumu yake  Jopo limekuwa likikutana na kufanya majadiliano ya kina na makundi mbalimbali yakiwamo ya  wataalamu,   wawakilishi wa  nchi tatu ambazo  zimeathirika sana na ugonjwa wa ebola (  Liberia,  Siera Leone na Guinea),Mashirika ya Kimataifa na Kikanda , Taasisi za Fedha za kimataifa, wahudumu wa Afya, Wasomi , Watafiti,  Sekta Binafsi na wataalam wa  fani  na kada mbalimbali.

Pamoja na kuhudhuria na kuongoza mikutano ya  Jopo, Mhe,  Rais   Kikwete  akiwa hapa  Makao  Makuu ya Umoja wa Mataifa, pia atahudhuria  Mikutano Mikubwa  miwili ambayo  ni,  Mkutano wa Kilele wa Kisiasa, ambao Wakuu wa Nchi na Serikali watapisha  Malengo  ya  Maendeleo Endelevu ( SDGs). Mhe. Rais atazungumza  katika  mkutano huu muhimu  kwa mstakabali wa maendeleo na ustawi wa binadamu kwa miaka 15 ijayo.

Malengo Mapya ya Maendeleo yanachukua nafasi ya   Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs) yanayomaliza muda wake   mwishoni mwa mwaka.

 Aidha Mhe. Rais atashiriki na kuhudhuria Mkutano wa  70 wa  Baraza Kuu la   Umoja wa  Mataifa.  Na anaratajiwa kulizungumza  Baraza Kuu na hii itakuwa ni hotuba yake ya   mwisho akiwa ni  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Vile vile Mhe. Rais atahudhuria mikutano  mingine  kadhaa.   Baadhi ya mikutano hiyo ni  ule  ambao umeandaliwa kwa pamoja  baina ya   Kansela wa Ujerumani  Mhe. Angela Merkel ,  Waziri Mkuu wa  Norway   Mhe. Erna Solberg na Rais wa Ghana Mhe.   John Dramani Mahama.

Mhe Rais anahudhuria mkutano  huu kwa mwaliko rasmi aliopewa na Kansela Angela Markel. Washirika  na waandaji  wengine wa mkutano huu ni  Mfuko wa Bill na Melinda Gates, Shirika la  Afya Dunia ( WHO) na Bank ya Dunia.

Mkutano huu unatarajiwa  kuzindua  misingi  na  hatua muhimu ambazo kwayo   zitaratibu  ufanisi na   upimaji  wa matokeo ya juhudi  za  kuimarisha mifumo ya afya.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages