LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 1, 2015

MEMBE: SUBIRINI KWA HAMU SIKU YANGU YA KUTANGAZA NIA YA KUWANIA URAIS WIKI HII

Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
 WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa  Kimataifa, Bernard Membe, amewaomba Watanzania kusubiri kwa hamu siku ya kutangaza nia ya kuwania urais kwa tiketi ya CCM, katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Membe amesema, amepanga kutangaza nia hiyo,  Juni 6, mwaka huu,  na kuwaomba wananchi wamsikilize kwa makini siku hiyo kwakuwa ataeleza kwa kina nini anataka kufanya nchi iweze kuondoka ilipo ikiwemo kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo.

Waziri Membe ambaye hajatangaza rasmi nia yake ya kuwania Urais, lakini ambaye ni miongoni mwa wanaotarajiwa kutikisa katika kuwania kiti hicho, alitoa mwito huo jijini Dar es Salaam jana,  katika Tamasha la Qaswida lililofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Benjamini Mkapa.

“Mkae tayari siku hiyo, naamini uongozi mzuri wa nchi ni ule wa kudumisha amani na utulivu na ili nchi iweze kusonga mbele, suala la uadlifu ni lazima kupewa kipaumbele kwa viongozi alisema,” alisema Waziri Membe

"Ninawapongeza sana, kwa kuamua kuwajenga vjana katika maadili ya dini, msingi huu ndio unaoweza kuifanya Tanzanaia kuwa na viongozi walio bora kutokana na hofu ya Mungu, maana mtu asiye mchamungu hawezi kukosa kuwa mla rushwa, fisadi na mtumiaji mbaya wa madaraka" alisema Membe.

Membe alitumia nafasi hiyo kuwatahadharisha kuwa makini katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu, kuacha kuchagua viongozi ambao kwa nje, wanajinadi  kuwa wachamungu, lakini matendo yao hayaendani na maadili ya  dini zao.

Alisema moja ya dalili za viongozi wasiokuwa waadilifu kwa kutokuwa na uchamungu huwa ni kusaka uongozi kwa kutumia fedha nyingi hivyo amewasihi wasiwachague viongozi wa aina hiyo wanaosaka uongozi kwa kutoa rushwa.

“Msikubali kuwa na viongozi ambao kwa nje, wanaojinadi kuwa na dini kinyume na matendo yao, lazima mchague wenye hofu ya Mungu jambo ambalo limekuwa likisisitizwa na dini zote. Uongozi wa heshima ni ule unaochukia rushwa ambayo ni adui wa haki", alisema Membe.

Kuhusu tamasha hilo, Waziri Membe alipongeza uwepo wake ambapo ni kuwalea vijana katika maadili mema ya kumjua Mungu na kusema anajivunia Taasisi za aina hiyo.

Tamasha hilo lililodhaminiwa na Kampuni ya Dira ya Mtanzania chini ya Mkurugenzi wake Alex Msama, zaidi ya vikundi 50 vimeshiriki tukio hilo la aina yake.

Akizungumza katika Tamasha hilo, Mkurugenzi wa Ulamaa Promotion Center ya jijini Dar es Salaam, Jumanne Ligopora, alihimiza umuhimu wa kila mtu kuwa sehemu ya ulinzi wa amani na utulivu.

Mwishoni mwa Tamasha hilo, Membe,  alikabidhi tuzo kwa watu mbalimbali na pia Membe mwenyewe kupewa tuzo kutokana na kutambua mchango wake katika masuala ya kijamii.

HABARI KATIKA PICHA
 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimatifa, Bernard Membe akimkabidhi tuzo ya heshima ya kujitolea kwa ajili ya madrasa hapa Tanzania, hajjat Tatu Kazuga wakati wa tamasha la kwanza la Qaswida lililofanyika jijini Dar es Salaam na kudhaminiwa na Kampuni ya Dira ya Mtanzania.
 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimatifa, Bernard Membe akimkabidhi Sheikh Ismail Mohamed tuzo ya heshima katika shughuli na masuala ya Qaswida hapa Tanzania. 
  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimatifa, Bernard Membe akimkabidhi Bi. Shamim Khan tuzo ya heshima ya kujishughulisha na kazi za kijamii hapa Tanzania.
 Sheikh Ismail Mohamed akizungumza waati wa tamasha la kwanza la Qaswida lililofanyika jijini Dar es Salaam na kudhaminiwa na Kampuni ya Dira ya Mtanzania.
 Baadhi wa waumini waliohudhuria tamasha hilo.
 Washiriki wa tamasha hilo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimatifa, Bernard Membe akizungumza katika tamasha hilo.
 Waimbaji wa Kaswida kutoka kikundi cha Muumini cha Buguruni jijini Dar es Salaam wakiimba kwenye tamasha la kwanza la Kaswida lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa. Tamasha hilo lilidhaminiwa na Kampuni ya Dira ya Mtanzania.  
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe akipokea tuzo maalumu kutoka kwa Sheikh Ismail Mohamed wakati wa tamasha la kwanza la Kaswida lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa na kudhaminiwa na Kampuni ya Dira ya Mtanzania.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages