LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

May 15, 2015

WAZIRI NYALANDU ADAI NASSARI MWONGO, ANATAPATAPA, AZUNGUMZIE MASLAHI YA WAPIGAKURA WAKE

Na Mwandishi wetu
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema kauli zilizotolewa Bungeni na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, ni za kutapatapa na zimejaa ukosefu wa busara na uzushi.

Amesema mbunge kusimama bungeni na kutoa kashfa badala ya kueleza masuala ya kisera au kiutendaji ni kupungukiwa busara na jamii haina budi kumpuuza.

Akichangia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu bungeni juzi, Nassari alisema Nyalandu kazi yake kubwa ni kuzunguka katika mapori ya akiba na kupiga picha na askari pamoja na kushangaa mbwa wa kizungu na kupokea ndege, helkopta za msaada. Alisema utendaji huo na mawaziri wengine unaweza ukawa ni ishara ya serikali iliyochoka.

Hata hivyo, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Nyalandu alisema Nassari anapaswa kuwakilisha na kutetea wapigakura wake kwa hoja badala ya kuropoka masuala ambayo hayana tija.

Alisema kauli zinazotolewa na wapinzani bungeni akiwemo Nassari kuishutumu serikali kuwa imechoka na kujaribu kuichonganisha na wananchi, kamwe hakuwezi kuikatisha tamaa kwa kuwa uzushi kwa upinzani ni jambo la kawaida.

Alikumbusha kuwa mapema mwaka huu alifanya ziara wilayani Arumeru ikiwemo jimbo la Nassari kutatua mgogoro baina ya wananchi na hifadhi, ambapo mbunge huyo alimtia moyo na kumtaka kupuuza kauli za kukatisha tamaa zinazotolewa dhidi yake.

“Hizi kauli za Nassari ni za kitoto na haziwezi kuleta tija kwa wapigakura wake…asimame kuzungumzia utendaji na masuala ya kisera sio kashfa ambazo hazipo…Namshauri awatumikie wapiga kura wake.

Nilifanya ziara jimboni kwake kutatua mgogoro na alinitia moyo kutokata tamaa na kauli za watu wanaonibeza na kunipongeza kwa utendaji kazi wangu,” alisema Nyalandu katika taarifa yake.

Taarifa hiyo pia ilikariri kauli ya Nassari aliyoitoa katika mkutano wa viongozi wa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, ambapo mbunge huyo na Aggrey Mwanry (Siha) walihudhuria akisema: “Naomba kukutia moyo kwani anayefanya kazi ya Mungu atapata nguvu, nikisikia mtu bungeni anasema wewe ni waziri mzigo, mimi nitaruka juu na kumwangukia vibaya.”

Imeeleza kuwa mafanikio makubwa ambayo wizara hiyo imepata kwa kumaliza migogoro ya ardhi mingi kwa muda mfupi wakati alipotembelea mapori ya akiba na hifadhi za taifa zenye migogoro ya ardhi na wananchi na kuipatia ufumbuzi.

Akiwa huko amekuwa na utaratibu wa kuzungumza na askari wa wanyamapori pamoja na wananchi kusikiliza kero zinazowakabili.

Miongoni mwa maeneo ambayo Nyalandu ametembelea ni wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, ambako kulikuwa na mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa vijiji 21 na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, uliodumu kwa miaka zaidi ya mitano bila kupatiwa ufumbuzi.

Nyalandu alimaliza mgogoro huo kwa kuruhusu wananchi wa vijiji hivyo kuendelea na maisha kama kawaida na kuagiza kufanyika kwa ukaguzi wa mipaka ya eneo hilo upya.

Awali, wananchi wa Mbarali waliishitaki serikali kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, ambaye aliitaka serikali kumaliza mgogoro huo kwa maslahi ya wananchi.

Maeneo mengine yenye mgogoro ambayo Nyalandu alifanya ziara kwa lengo la kutoa ufumbuzi ni Pori la Burigi wilayani Biharamulo, Iringa, Masasi, Lamadi ambako alikutana na wafugaji kutoka mikoa yote nchini pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Saadani wilayani Bagamoyo ambako pia kulikuwa na mgogoro wa ardhi.

“Ninapofanya ziara natekeleza majukumu yangu kama waziri, siwezi kukaa ofisini wakati kuna mgogoro baina ya wananchi na hifadhi za taifa na mapori ya akiba…nina dhamana ya kushughulikia mambo haya hivyo, kauli za kitoto kamwe haziwezi kunikatisha tamaa,” aliongeza Nyalandu.

Aidha, aliongeza kuwa katika kuhakikisha serikali inashinda vita dhidi ya ujangili, amekuwa mstari wa mbele kushirikiana na wadau wa uhifadhi na kwa jitihada zake amefanikisha kupatikana kwa ndege, helkopta na vifaa vingine ili kukabiliana na majangili.

Alisema vifaa hivyo ikiwemo ndege, magari, helkopta, silaha na vitendea kazi vingine hukabidhiwa kwake na baadaye huvikabidhi kwa watendaji wake kwa ajili ya kukagiwiwa kwenye hifadhi za taifa na mapori ya akiba.

“Tumeanzisha vita dhidi ya majangili hivyo ni lazima tuwe na vitedea kazi vya kutosha, nimefanya jitihada za kupata helkopta, ndege, silaha za kisasa, magari na juzi Marekani imetupa mbwa maalumu ambao tutawatumia pia kwenye viwanja vya ndege na bandarini kwa usalama zaidi.

“Sasa Nassari anaumia kuona hizi jitihada zetu kama serikali katika kulinda rasilimali zetu au alitaka akabidhiwe yeye,” alihoji Nyalandu.

Akizungumza kupiga picha na askari wa wanyamapori, Nyalandu aliwapuuza watu wenye mawazo tofauti akisema si jambo baya kufurahi na wapiganaji wake, ambao wamekuwa wakitumia muda mwingi wa maisha yao msituni.

Alisema amekuwa na utaratibu wa kufurahi pamoja, kula na kunywa na askari wa wanyamapori pindi anapofanya ziara zake katika hifadhi na mapori ya akiba.

“Watu wenye nia mbaya siku zote ndio wamekuwa na imani potofu, ninapofanya ziara kwanza nawafikiria wapiganaji wetu wanaoishi msituni kukabiliana na majangili hatari…siwezi kwenda huko na kukunja sura kama tuna ugomvi bali baada ya kupeana maagizo ya kazi tunakuwa kitu kimoja, tunafurahi na kutiana moyo ili kuongeza ari ya kulinda rasilimali za taifa. Kauli zingine zinasikitisha mno,” alisema.
HABRI KATIKA PICHA
 WAZIRI Nyalandu akikagua gwaride la askari wa wanyamapori wakati akiwa
kwenye moja ya ziara zake.

 Waziri Nyalandu akikagua nyara a serikali zilizokamatwa kutoka kwa majangili alipokagua moja ya mbuga za wanyama kwenye moja ya ziara zake hivu karibuni
 NYALANDU akiwa kwenye picha ya pamoja na askari wa wanyamapori, maofisa na wafanyakazi wa Pori la Selous, muda mfupi baada ya kuzungumza nao na kupeana mikakati ya kiutendaji.

 Waziri Nyalandu akikagua meno ya tembo yaliyokamatwa kutoka kwa majangili kufuatia operesheni zinazofanywa na askari wa wanyamapori.
  WAZIRI Nyalandu (katikati) akiwa amezungukwa na wananchi wilayani Chemba alipokwenda kutatua mgogoro wa ardhi baina ya wananchi wa kijiji na hifadhi ya misitu.
 WAZIRI Nyalandu akiwa na wanafunzi wa Sekondari ya Selous wakati alipokuwa kwenye ziara ya kukagua shughuli za uhifadhi na vita dhidi ya ujangili, ambapo alipata fursa ya kuzungumza na wanafunzi shuleni hapo.
 WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, akila chakula cha mchana na wanafunzi wa sekondari ya Selous, iliyopo Kijiji cha Lukuyu Sekamaganga wilayani Namtumbo, Ruvuma.
 WAZIRI Nyalandu akiwa katika picha ya pamoja na vijana wanaounda vikundi vya ulinzi kwa lengo la kukabiliana na ujangili kwenye maeneo ya Pori la Akiba la Selous wilayani Namtumbo.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages