LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

May 10, 2015

HOJA MTAMBUKA: UKAWA KUTI KAVU WALILOKALIA CHADEMA, CUF

*Hauna ubavu kuteua wagombea kupambana na CCM Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
*Prof. Lipumba ataweza kupumzika kugombea Urais mwaka huu na kumwachia mgombea wa Chadema?
*CUF wapo tayari kuwapa Chadema jimbo walau moja Pemba?

NA BASHIR NKOROMO
Licha ya hali halisi kuonyesha wazi, kuna ambao bado wanaamini kuwa 'muungano' wa baadhi ya  vyama vya upinzani unaiotwa UKAWA unaweza kuwa nyenzo ya kuvifanya vyama hivyo vifanye  vizuri katika Uchagu Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Ukweli ni kwamba  hadi sasa imeshadhihirika wazi kwamba muungano huo ambao chimbuko la  lake ni kilichoitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi ulioundwa na vyama kadhaa vikiwemo Chadema,  CUF na NCCR Mageuzi, mwanzoni mwa mchakato wa Katiba mpya, ambao sasa umefikia hatua ya  Katiba inayopendekezwa, hauwezi kufua dafu.

Hii ni kutokana na sababu nyingi ikiwemo hali halisi za kimazingira ya kisiasa ya vyama husika  na vilivyounda Ukawa na asili yenyewe ya kuanzishwa kwake huo Ukawa.

Kwa wale wanaofuatilia mambo ya siasa za Tanzania, wanakumbuka namna ambavyo, Ukawa  ulianza. Harakati za mwanzoni kabisa zilianza kwa Chadema kususia bunge kwa kutoka ukumbini  mara kadhaa wakati wa vikao vya bunge la Katiba.

Ikumbukwe pia kwamba wakati wa michakato kama hiyo ya Katiba hasa katika nchi za Kiafrika,  ndiyo wakati ambao baadhi ya Taasisi binafsi za kitaifa na kimataifa hutafuta kutambuliwa uwepo  wake, kwa kujitokeza zenyewe kukosoa au kuchangia masuala mbalimbali kwenye mchakato na  nyingine kufanya hivyo kimya kimya.

Taasisi ambazo hujitokeza waziwazi hizo ndizo kupewa nguvu hasa kifedha kutoka kwenye taasisi  zile ambazo kufanya kazi kimya kimya. na uchunguzi unaonyesha kuwa taasisi ambazo hutoa  fedha mara nyingi ni zile za nje ya nchi.

Mara kadhaa imekuwa ikielezwa kwamba Taasisi ambazo hujiingiza katika michakato, hufanya  hivyo kwa lengo la kuimarisha Utawala Bora na uimarishaji Demokrasia katika nchi inayokuwa  katika pilika hizo za kutengeneza katiba mpya.

Zipo taasisi ambazo hufanya hivyo kwa lengo hilo, lakini nyingine kufanya kwa lengo la kuvuruga  huku nyingine zikijiingiza kwa kuwa viongozi wake huona kuwa ni msimu au fursa ya kujipatia  mamilioni ya fedha kutoka kwa 'wahisani'.

'Wahsani' hao ndio wanaoaminika kuwa chanzo cha vyama Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi  kuamua kuunda kilichokuja kuitwa UKAWA, kwa kuwa 'wahisani' hao inadaiwa waliwalazimisha  kuungana na kwa kuwa inaelezwa kuwa kulikuwa na fungu, Kina Freeman Mbowe  (Mwenyekiti wa  Chadema)na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF,  wakalazimika kujaribu kuwa kitu kimoja katika  huo ukawa.

Usemi wa 'tumikia kafiri upate mradi wako' ukatimia, wakamua kutoka kwa muda katika uhasama  uliokuwepo wakati Chadema ilipokuwa ikiishambulia CUF kuwa ni CCM B baada ya kukubali  kuingia katika Serikali ya Umoja Visiwani Zanzibar, hatimaye viongozi wa vyama hivyo sasa  wakakaa kwenye meza moja kwa kapu la Ukawa.

Kwa hiyo, kulingana na mtazamo huo, Ukawa ni umoja unaonekana kuwa ulianzishwa kwa lengo la  kimaslahi ya viongozi wa vyama husika zaidi na siyo kweli ya dhahiri kuwa lengo lilikuwa kupata  kinachodaiwa kuwa ni Katiba ya Wananchi.

Pamoja na kwamba dodoso zinaonyesha kwamba Ukawa ulianzishwa kimaslahi zaidi, lakini bado  pia Ukawa unaonekana kutokuwa chombo cha maana kuweza kuwaunganisha wapinzani kufanya  vizuri Uchaguzi Mkuu kwa kuwa kuanzishwa kwake hakuhusiani na kuweza kufanya kazi kwa  uhakika wakati wa uchaguzi mkuu huo.

Japokuwa vyama kadhaa vinavyotaka uongozi wa nchi huanza na harakati za Umoja, lakini wakati  siku zinazidi kuyoyoma bado viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa wameendelea kufanya bla  bla tu, badala ya kujenga misingi itakayowafanya asiwepo moja wapo wa kukiuka makubaliano  kama yapo.

Mfano mdogo ni wakati wa Uchaguzi uliopita wa Serikali za Mitaa, ambapo vyama vya upinzani   vilitangaza kushirikiana kupitia Ukawa kwa kupishana nafasi kwenye uchaguzi huo kulingana na  nguvu aliyonayo mgombea wa upinzani katika eneo mojawapo.

Lakini wakati wa matokeo, ilikuja kuonekana kwamba yapo maeneo mengi ambayo kama Chadema  na CUF peke yake wangeachiana wangepata viti vingi. Lakini ilishuhudiwa kwamba kuna maeneo  mengi tu, CCM iliibuka na ushindi ambao usingeweza kupatikana kirahisi kama kura za wagombea  Chadema na CUF zingekuwa za mmoja wapo.

Na unafiki unajidhihirisha zaidi pale, wanapotangaza viongozi wa Ukawa hasa Mwenyekiti wa  Chadema Freeman Mbowe kwamba, katika Uchaguzi Mkuu, mgombea wa upinzani atakayekuwa na  nguvu zaidi ndiye atapitishwa peke yake kugombea.

Hii ni hadidhi ngumu sana kufanyika ili iweze kusimulika baadaye, kwanza kwa sababu ni vigumu  dhana ya Umoja (Ukawa) kushinda dhana ya chama wakati wa mchakato wa kupata wagombea,  hivyo si rahisi Ukawa ukaibuka kumwambia mgombea pengine wa CUF kuwa ni dhaifu kwa  mgombea wa Chadema au wa Chadema ni dhaifu kwa mgombea wa CUF  wakati kila mmoja  amejipima kupitia wapambe wake akajiona ananguvu.

Ni vigumu kwa nguvu ya Ukawa tu, kumshawishi mgombea wa chama fulani ampishe wa chama  kingine, tena kwa kumpa kigezo kuwa ameshindwa nguvu na anayehitaji kupishwa. Hii ni ngumu  sana kwa sababu kila mgombea anajipima nguvu kutokana na wapambe wa chama chake, sasa  itakuwaje mgombea anaona wanachama wa chama chake wanamuunga mkono halafu umwabie  hatoshi, bora wa chama kingine?

Shughuli hii ya mgombea mmoja kumpisha mwingie kwa kushindanisha nguvu inawezekana  kufanyika ndani ya Chama, kwa wagombea kushindanishwa nguvu na mwanachama mwenzake  lakini si ndani ya Umoja kama ulivyo Ukawa.

Kuthibitisha hili, unaweza kurejea namna ambavyo huwa changamoto vyama kuchuja wagombea  kupata mmoja atakayepeperusha bendera dhidi ya wagombea wa vyama vingine. Licha ya kuwepo  taratibu sheria na utii ndani ya chama husika lakini kumpata mgombea huyo huwa ni kazi ambayo  huacha mashimo wakati mwingine ya hatari sana ndani ya Chama.

Kila unapotajwa utaratibu wa kupishana majimbo, lazima kutafakari kwamba CUF ndiyo bado kina  nguvu kubwa katika Kisiwa cha Pemba na majimbo yote kisiwani humo yapo chini ya chama hicho,  lakini wakati huo huo, CUF haina mbunge wa kuchaguliwa hata mmoja Tanzania Bara, huku  Chadema nao wakiwa hawana kiti hata kimoja cha kuchaguliwa Zanzibar yote,  lakini ndicho  chama cha upinzani chenye wabunge wengi Tanzania Bara.

Je, ikiwa hali ni hivyo kupitia UKAWA, CUF wapo tayari kuwapisha Chadema waweke wagombea  katika majimbo walau mawili tu Pemba?,  Au, kupitia Ukawa huo, Chadema wapo tayari kuwaachia  CUF kugombea katika majimbo walau matano Tanzania Bara ambako wana nguvu?.

Kwa sababu ikiwa ni kufuata kigezo cha mgombea kuwa na nguvu, hali itabaki kama ilivyo sasa,  kwa kuwa mahali ambako CUF wanakubalika Chadema haina chake, na kule Chadema  wanakokubalika, CUF hawana chao.

Na uzoefu kupitia chaguzi zilizopita ni kwamba, pale ambako CUF inakubalika mgombea wa  Chadema amekuwa akipata kura za chini sana, na hali kadhalika pale ambako mgombea wa  Ubunge wa Chadema anapokubalika wa CUF amekuwa akiambulia kura za chini sana.

Kinachoweza kuonekana hapa ni kwamba mchezo huu wa UKAWA ni njama za baadhi ya vyama  kujenga mazingira ya kuhakikisha vyama vingine havigusi majimbo  wanayodhani wananguvu  nayo.

Kuweka wazi ni kwamba, chama kinachojihami zaidi ni Chadema, kwa sababu kinajua kwamba  CUF wakiweka wagombea katika majimbo wanayodhani wanakubalika, kuna uwezekano  wakagawana kura ikashinda CCM.

Lakini Chadema hata wakiweka wagombea Pemba yote, na hata Zanzibar kwa ujumla bado CUF  inaweza kushinda, na pale itakaposhindwa itashinda CCM lakini Chadema si rahisi.

Lakini hata upande wa Urais, kutokana na uzoefu uliojitokeza katika miaka iliyopita, jiulize, je,  Profesa Lipumba ambaye hajawahi kukosa kugombea Urais katika Uchaguzi Mkuu wowote tangu  mfumo wa vyama vingi uanze hapa nchini, atakuwa tayari safari hii, kumwachai mgombea kwa  mfano wa Chadema au wa NCCR Mageuzi, yeye abakie kuwa mpiga debe?

Au, je, ni rahisi Chadema wanaojitazama kuwa chama cha upinzania chenye nguvu hapa nchini  kuliko vyama vingine, watakuwa tayari kujiweka pembeni, wasiweke mgombea wa Urais  kuunemesha Ukawa, bila shaka ni ngumu sana, na kama ni rahisi tusubiri wakati utasema.

Sana sana Chadema, katika kujaribu kuwatega CUF, wanaweza kuwaambia kwamba hawataweka  mgombea Urais wa Zanzibar, ili chama hicho cha CUF kiwaachie wao Urais wa Muungano, lakini si  rahisi CUF kukubali kwa sababu itakuwa sawa na kujichimbia kaburi chama hicho kitoweke  Tanzania Bara.

Na ni wazi CUF hawawezi kukubali kwamba waache kugombea Urais wa Muungano kwa kuachiwa  Zanzibar, kwa sabau kulingana na mazingira ya Zanzibar, Chadema hata wakiweka mgombea  Urais wa Zanzibar hawaiathiri chochote CUF. kwa maana nyingine, Chadema iweke mgombea  Urais au isiweka matokeo ya CUF katika urais hayabadliki sana.

Hata hadi sasa tayari CUF wameshateua watakaowania Ubunge na Baraza la Wawakilishi kwa majimbo yote Zanzibar, na katika kuthibitisha kuwa Ukawa ni kwa ajili ya kuwalinda viongozi, jimbo moja tu la Kikwajuni  ambalo CUF wameamua kufumba mamcho na kuwaachia Chadema, wamesema wanaliacha kwa ajili' ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Salum Mwalim na si kwa ajili ya mwanachama yeyote atakayetaka!

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages