LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 30, 2015

CCM ZANZIBAR: VIONGOZI NA WATENDAJI CCM MSIBEBE WATANGAZA NIA

CHAMA Cha Mapinduzi Zanzibar kimesisitiza haja kwa Viongozi na Watendaji wake kuacha tabia ya kuwabeba wana CCM wenye kutangaza nia ya kugombea nafasi za uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa dola ujao, kwani kufanya hivyo ni kukiuka kanuni na miongozo ya Chama hicho.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC  wa Idara ya itikadi na Uenezi (Z) Bibi Waride Bakari Jabu, ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa akizungumza na Wajumbe wa Halmashauri Kuu za Matawi na Wadi za Jimbo la Dole, Wilaya ya Kichama ya Mfenesini.

Amesema CCM inaongozwa kwa kanuni na taratibu zinazotambulika Kikatiba, hivyo hakitomvumilia mwanachama yeyote anayevunja  kanuni hizo kwa maslahi yake binafsi kwani kila jambo limewekewa utaratibu wake ambao unapaswa kufuatwa na kila Mwana CCM.

Amesema ni marufuku kwa mwana CCM kuanza kutangaza nia ya kugombea nafasi yoyote hasa  Ubunge, Uwakilishi au Udiwani,  kwani muda wa kufanya hivyo bado haujawadia.

Ametoa wito kwa Viongozi hao wa Jimbo la Dole la Wilaya ya kichama ya Mfenesini kuelekeza nguvu zaidi katika kubuni mbinu na mikakati madhubuti kwa  kuwaandaa watu wenye sifa za kupiga kura, ili waweze kuleta ushindi wa kishondo wa Chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Dola wa Oktoba, mwaka huu (2015).
Nao, Wajumbe wa Halmashauri Kuu za Matawi na Wadi za Jimbo la Dole, wamesisitiza haja ya kuendeleza suala zima la umoja na mshikamano miongoni mwao, kwa maslahi ya Chama na Taifa kwa ujumla.

Katibu huyo wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar wa Idara ya Itikadi na Uenezi, tayari ameshafanya ziara katika majimbo ya 19 ya Mikoa ya Kichama ya Kaskazini, Kusini na Magharibi, Unguja.
 
Imetolewa na :-
                           Idara ya Itikadi na Uenezi - CCM, 
                                       ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages