LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 18, 2015

WAZIRI NYALANDU AZIMA MARUFUKU MAGARI YA TANZANIA JKIA

Na mwandishi wetu
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema serikali ya Kenya imekubali kuyaruhusu magari ya abiria na watalii kutoka Tanzania, kuingia ndani ya Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi.
Awali, Serikali ya Kenya iliyazuia magari hayo kuingia uwanjani hapo huku ukiyatoza ushuru kwa yale yanayoingia, jambo ambalo lililalamikiwa na wafanyabiashara wa Tanzania.
Marufuku hiyo ya Kenya kwa magari ya Tanzania, ilidumu kwa zaidi ya wiki mbili, ambapo katika kusaka suluhu hiyo Nyalandu alikutana na wafanyabiashara hao jijini Arusha kisha kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Biashara na Utalii wa Kenya, Phyllis Kandie.
Katika mazungumzo yake na Kandie, Nyalandu alisema kwa sasa magari ya Tanzania yataendelea kuingia uwanjani hapo wakati ufumbuzi wa kudumu ukitafutwa.
Alisema kutakuwa na vikao vya kazi baaina ya Wizara ya Utalii ya Kenya na wizara yake, ambapo vitaanzia ngazi ya watandaji, watalaamu, makatibu wakuu na mawaziri.
Alisema katika mikutano hiyo masuala mbalimbali kuhusiana na biashara ya utalii yatazungumzwa baina ya nchi hizo mbili.
Hata hivyo, alisema katika vikao hivyo suala la mpaka wa Bolongoja halitajaliwa wala kuwepo kwenye ajenda.
“Kwa sasa wafanyabiashara wetu wataingia Jomo Kenyatta kama ilivyokuwa awali. Tumezungumza na kupanga kuwa na vikao kujadili na kuzipatia ufumbuzi changamoto zote kuhusiana na sekta ya utalii.
“Niwahakikishie tu katika vikao hivyo maslahi ya pande zote yatazingatiwa, lakini suala la mpaka wa Bolongoja halitajadiliwa wala kuwemo kwenye ajenda za vikao vyetu.
“Wataalamu na watendaji wa wizara yangu watakutana na wenzao jijini Arusha na maofisa wa Jumuia ya Afrika Mashariki watashiriki ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu,” alisema Nyalandu.
Kupatiwa ufumbuzi kwa tatizo hilo kumekuwa faraja kubwa kwa wafanyabiashara na wadau wa utalii katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, ambapo walipongeza jitihada za haraka zilizofanywa na Nyalandu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wadau hao wa utalii walisema Nyalandu ameonyesha utendaji kazi kwa vitendo na kwamba, hilo linapaswa kuwa mfano kwa viongozi wengine.
Walisema waziri huyo baada ya kupata taarifa za wafanyabiashara wa Tanzania kuzuiwa kuingiza magari Jomo Kenyatta, aliwafuata kwenye maeneo yao na kuwasikiliza kero zinazowakabili kisha kufunga safari kukutana na waziri Kandie jijini Nairobi.
“Hawa ndio aina ya viongozi ambao Tanzania ya sasa na inayokuja inawahitaji, wanaposikia wananchi wana kero na wananyimwa haki ama kunyanyaswa wanakwenda kuwasikiliza na kutafuta ufumbuzi wa haraka. “Kwa hili Waziri Nyalandu anastahili pongezi na viongozi wengine waige mfano huu, wangekuwa wengine wangeanza kuleta siasa na tatizo kuchukua muda mrefu kupata ufumbuzi,” alisema John Mlay, ambaye ni mmoja wa wafanyakazi kwenye kampuni za usafirishaji watalii.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages