LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 28, 2014

PSPF YACHANGIA MABATI YA UJENZI WA MAABARA WILAYA YA KILOLO


Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Gerald Guninita akizungumza mara baada ya kupokea msaada kutoka PSPF
Amelia Rweyimamu, Muwakilishi wa PSPF makao makuu Dar es salaam akizungumzia lengo la kushiriki ujenzi wa maabara
Afisa Mfawidhi wa PSPF mkoa wa Iringa, Baraka Jumanne akifafanua jambo
Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Wawakilishi wa PSPF, na Waaandishi wa habari wakizungumza wakati wa hafla

Na Mathias Canal, kilolo
Mfuko wa Penseni (PSPF) umechangia bati 200 zenye geji 28, kwa ajili ya kusaidia Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Mkoani Iringa, ili kukamilisha adhma ya ujenzi wa maabara kwa shule za sekondari Wilayani humo.

Akizungumza baada ya kupokea bati hizo,Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Gerald Guninita, alisema kuwa hakutarajia kupokea zawadi kama hiyo pamoja na kwamba alituma maombi PSPF, hivyo bati hizo zitatumika kwa kazi maalumu ya ujenzi wa maabara Wilayani humo kufuatia agizo lililotolewa na Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, la kujenga maabara ambapo hadi kufikia tarehe 30 Novemba ujenzi huo unatakiwa kuwa umekamilika.

Guninita alisema kuwa kukamilika kwa maabara hizo kutahamasisha watoto wengi kupenda masomo ya sayansi kwani watasoma kwa vitendo na uhakika zaidi, huku akizungumzia ufaulu mzuri wa kidato cha nne mwaka jana ambapo Halmashauri ya wilaya hiyo ilishika nafasi ya kwanza kimkoa huku ikiwa imeshika nafasi ya tisa kitaifa.

"Ninawashukuru PSPF kwa kujitolea bati hizi kwa ajili ya Wilaya yangu ya Kilolo, naamini hakutakuwa na kigugumizi katika utekelezaji wa agizo la Rais kwani wadau kama ninyi mnapojitolea sisi hatuna budi kushukuru na kufanyia kazi inayokusudiwa ya ujenzi ndani ya muda mwafaka". Alisema Guninita

Guninita aliongeza kuwa Wilaya ya Kilolo ina jumla ya shule 20 za Sekondari ambazo kwa asilimia kubwa ujenzi wa vyumba vya maabara umekamilika hivyo kwa sasa wamejikita katika ujenzi wa meza.

Kwa upande wake Amelia Rweyimamu ambaye ni Muwakilishi wa PSPF makao makuu Dar es salaam, akizungumza wakati wa kukabidhi bati hizo alisema kuwa PSPF inatambua umuhimu wa kuwepo kwa maabara hapa nchini hivyo ofisi yake imeona vyema kushiri katika ujenzi huo kwa kutoa bati hizo.

Rweyimamu alisema PSPF inatoa mafao mbalimbali ikiwa ni pamoja na fao la uzeeni, fao la ulemavu, fao la kifo, fao la mazishi, fao la wategemezi lisilo na kikomo, fao la kujitoa, fao la uzee, fao la kufukuzwa kazi, na fao la ujasiriamali.

Aidha aliongeza kuwa PSPF inatoa fao la elimu ambapo mfuko hudhamini mikopo katika bodi ya mikopo ya wanafunzi, lengo kubwa ikiwa ni kujenga uwezo wa kuhudumia wanafunzi wengi katika taaluma mbalimbali ikiwemo pia taaluma ya sayansi, Teknolojia na Afya.

Naye Afisa Mfawidhi wa PSPF mkoa wa Iringa, Baraka Jumanne, alisema kuwa PSPF imetoa bati 200 kwa Wilaya ya Kilolo ambazo zina thamani ya shilingi milioni sita za kitanzania ili kusaidia ujenzi wa shule Wilayani humo.

Jumanne alisema maabara ya sayansi ni muhimu katika maendeleo ya wanafunzi kujifunza kwa nadharia na vitendo kutokana na umuhimu huo, kunahitajika ushirikiano kama ule ulioonyeshwa wakati wa ujenzi wa shule za sekondari za kata.

Hata hivyo hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, aliwaagiza wakuu wa mikoa na wilaya nchini, kujenga maabara kwa kila shule ya sekondari katika kipindi cha miaka miwili, kuanzia sasa ambapo alitoa agizo hilo wakati akihutubia maelfu ya wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi mkoani Singida, waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika katika Mji mdogo wa Itigi.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages