LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 17, 2014

UMOJA WA MATAIFA KUJADILI UGONJWA WA EBOLA-BAN KI MOON

Na  Mwandishi Maalum, New  New York 
Viongozi  Wakuu wa Nchi na Serikali  zaidi ya 140 kutoka mataifa mbalimbali duniani  wamethibitisha  kuhudhuria na  kushiriki  majadiliano ya  jumla wakati wa Mkutano  wa  69 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoanza wiki ijayo.

Akizungumza na  waandishi wa habari hapo siku ya  Jumanne, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Ban Ki Moon, amesema,  viongozi hao pamoja na  kujadili  changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia hivi sasa,  watautumia mkutano huu kujadiliana kwa kina kuhusu  mchango na ushiriki wa jumuiya ya kimataifa katika kuukabili  mlipuko wa ugonjwa hatari wa Ebola.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete  ni miongoni wa viongozi hao 140 na anaongoza  ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huu.


 Akizungumzia zaidi kuhusu mlipuko wa ugonjwa hatari wa Ebola na athari zake kwa uhai wa mwanadamu na kwa maendeleo ya  kiuchumi na kijamii,   Ban ki  Moon amewaeleza  waandishi hao, kuwa Jumuiya ya kimataifa haiwezi kuendelea kuufumbia macho na kwamba kadiri inavyochelewa kuutafutia ufumbuzi ndivyo  hatari yake inavyozidi kuongezeka.


“Tutatoa kipaumbele cha peke kuhusu ugonjwa wa Ebola ambao umeleta athari kubwa kwa baadhi ya nchi za Afrika ya Magharibi na maeneo mengine. Siku mbili zijazo ( Alhamisi) Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana kwa dharura kuzungumzia mlipuko wa Ebola. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Margaret Chan na Mimi tutazungumza katika mkutano huo” akasema Ban Ki Moon.


Akaongeza kwa kusema wiki ijayo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa litakuwa na mkutano wa kilele kuhusu mahitaji ya watu na nchi zilizokabiliwa na ugonjwa wa Ebola.


Pamoja na  kujadili  na kutafuta mkakati wa pamoja wa kukabiliana na Ebola,  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  anasema  viongonzi hao wakuu wa nchi na serikali pia wanatarajiwa  kujadili na kubadilishana  mawazo kuhusu  changamoto za mabadiliko ya tabia nchi katika  mkutano utakaofanyika septemba 23.


Mhe. Rais Jakaya  Kikwete ni kati ya  Viongozi  walioalikwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  kuhudhuria na kuzungumza katika mkutano huu muhimu kuhusu  suala zima la mabadiliko ya tabia nchi na  athari zake.


Akielezea zaidi kuhusu mkutano huo wa mabadiliko ya tabianchi, Ban Ki Moon anasema  mkutano huo utakuwa na malengo mawili, kwanza ni kukusanya utashi wa kisiasa  ili kufikia makubaliano ya pamoja hapo mwakani katika mkutano utakaofanyika huko Paris , Ufaransa. Na pili kuchukua hatua madhubuti za kupunguza  uzalishaji wa gesi chafu.


Akiainisha zaidi  kuhusu ajenda mbalimbali zitakazojadiliwa wakati wa Mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa,  Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, amesema,   majadiliano ya Baraza Kuu ( General Debate) yatakayoanza septemba 24   yatatumika  kukusanya nguvu za pamoja za  kuushinda umaskini, na kupitisha ajenda za malengo mapya ya maendeleo endelevu .


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya  Mrisho Kikwete atalihutubia Baraza Kuu Septemba 25.


Masuala mengine ambayo pia  yanatarajiwa kutawala mkutano huo wa Baraza  Kuu la Umoja wa Mataifa  kwa mujibu wa  Ban Ki Moon, ni pamoja na  migogoro na machafuko yanayoendelea katika nchi za Syria,  Iraq, Libya, Mali,  Jamhuri ya Afrika ya Kati, Ukraine, Sudan ya Kusini ukiwamo pia  mgogoro  kati ya Palestina na Israel.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages